Dar es Salaam Desemba 18, 2025: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza waandishi wa habari za mtandaoni na bloga wanaounda Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA), na kuagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwalea vizuri na kuwapa fursa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Pongezi na maelekezo hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, alipokuwa akifunga kikao cha pamoja cha wanachama wa TBN na JUMIKITA kilichoandaliwa na TCRA jijini Dar es Salaam, Desemba 18, 2025.

Bw. Msigwa alisema Rais Samia anatambua mchango mkubwa wa waandishi wa habari za mtandaoni katika kusambaza taarifa na kuimarisha mawasiliano kati ya serikali na wananchi, hivyo akaagiza wapewe malezi, miongozo na fursa zitakazowawezesha kufanya kazi zao kwa weledi.

“Mheshimiwa Rais amewapongeza sana na anatambua kazi zenu nzuri. Ni maelekezo yake kwamba kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Idara ya Habari MAELEZO na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia TCRA, waandishi wa habari za mitandaoni na bloga walelewe vizuri na wapewe fursa ili wafanye kazi zao vizuri,” alisema Msigwa.

Alisisitiza kuwa maelekezo hayo ni maagizo ya moja kwa moja kutoka kwa Rais na kwa utaratibu wa kiserikali, yanapaswa kutekelezwa bila mjadala.

“Haya kwetu ni maelekezo. Kwa utaratibu wa serikali, ukishapewa maelekezo kinachofuata ni utekelezaji. Ndiyo maana tupo hapa kuhakikisha maagizo ya Mheshimiwa Rais yanatekelezwa,” alisema Msigwa huku akishangiliwa na washiriki wa kikao hicho.

Aidha, alisema mwelekeo huo unaendana na falsafa ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayosisitiza ushirikiano kati ya serikali na wadau mbalimbali kwa manufaa ya taifa.

Aliitaja Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA) kuwa ni wadau wakubwa wa serikali katika tasnia ya habari, akibainisha kuwa mchango wao ni muhimu katika kusambaza taarifa sahihi na kujenga mawasiliano yenye tija kati ya serikali na wananchi.

“Serikali imewaamini waandishi wa mitandaoni. Sasa ni wajibu wenu kuendeleza imani hiyo kwa kuzingatia maadili, ukweli na uzalendo katika kazi zenu. Ushirikiano wetu umeendelea kuimarika na changamoto zinazojitokeza tunazitatua kwa pamoja,” alisema Msigwa.

Kikao hicho kililenga kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wadau wa habari za mtandaoni pamoja na kujadili masuala ya maendeleo ya tasnia ya habari katika mazingira ya kidijitali.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: