Na Mwandishi Wetu, Pretoria – Afrika Kusini

Tasnia ya habari nchini imepata heshima mpya baada ya Veronica Mrema, Mwanzilishi wa M24 Tanzania Media na mwanachama wa Tanzania Bloggers Network (TBN), kuteuliwa kuwa miongoni mwa wachangiaji wa jopo la mdahalo katika Mkutano wa 13 wa Kimataifa wa Waandishi wa Habari za Sayansi (WCSJ2025) unaofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Uteuzi huo unaonekana kuwa ishara ya kutambuliwa kwa kasi inayoongezeka ya uandishi wa habari za kidijitali na kisayansi nchini Tanzania, na umepokelewa kama fahari kwa TBN na tasnia nzima ya habari.

Mrema, ambaye pia ni Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR-PC) na Afisa Habari wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Selimundu Tanzania (SCDPCT), amewasili nchini Afrika Kusini kwa udhamini maalum wa safari (Travel Grant) uliotolewa na Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ya Afrika Kusini (DSTI). Udhamini huo umetokana na utambuzi wa mchango wake katika uandishi wa habari za sayansi na afya, huku akitajwa kuwa miongoni mwa wachache kutoka barani Afrika waliopata nafasi hiyo ya kipekee.

Kupitia nafasi yake katika jopo hilo, Mrema anatarajiwa kuwasilisha hoja kuhusu umuhimu wa uandishi wa habari za kisayansi barani Afrika, ikiwemo haja ya kuimarisha ubunifu, weledi na uwasilishaji wa taarifa zenye ushahidi ili kusaidia jamii kufanya maamuzi sahihi yenye tija kwa maendeleo.

WCSJ2025 ni mkutano mkubwa unaowakutanisha waandishi wa habari za sayansi, watafiti na wataalamu kutoka nchi mbalimbali duniani, ambapo washiriki wanajadili mustakabali wa tasnia hiyo, changamoto, fursa na mbinu za kuboresha mawasiliano ya kisayansi.

Kwa mujibu wa TBN, hatua ya Mrema kukaa jukwaa moja na wataalam wakubwa wa kimataifa ni uthibitisho kuwa Tanzania inaendelea kupiga hatua katika anga za habari za kisasa, na kwamba mchango wa wanahabari wa kidijitali nchini unatambulika na kuthaminiwa katika majukwaa ya kimataifa.

Mkutano huo unatarajiwa kuendelea hadi Desemba 5, 2025.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: