Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Benki ya Exim Tanzania imezindua kampeni kubwa ya matumizi ya kadi katika msimu wa sikukuu, iitwayo “Chanja Kijanja, Dili Ndio Hili,” ambayo itadumu kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia 1 Desemba 2025 hadi 31 Januari 2026. Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha Watanzania kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kujenga utamaduni wa kufanya malipo ya kidijitali, hususan kwa wateja wanaotumia kadi za Exim Mastercard.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Exim, Andrew Lyimo, alisema kampeni hiyo imeandaliwa ili kutoa suluhisho la malipo lililo rahisi, salama na lenye manufaa kwa wateja katika kipindi ambacho matumizi ya ununuzi huongezeka kutokana na sikukuu.

“Lengo ni kufanya malipo ya kila siku kuwa mepesi zaidi na kuwapa wateja nafasi ya kujishindia zawadi kemkem. Hii inaendana na dhamira ya benki katika kukuza matumizi ya malipo ya kidijitali nchini,” alisema.

Katika kipindi cha kampeni, wateja watakaofanya malipo kwa kutumia kadi za Exim Mastercard kupitia mashine za POS au mtandaoni watapata nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali, ikiwemo:

●Zawadi za kila wiki: TZS 100,000 kwa washindi watano (5).

●Zawadi za kila mwezi: TZS 200,000 kwa washindi kumi (10).

●Cashback maalum katika siku za Black Friday (28 Nov 2025), Cyber Monday (1 Des 2025), na Krismasi (25 Des 2025).

●Zawadi kubwa mwishoni mwa kampeni: TZS milioni 5, TZS milioni 10 na zawadi kuu ya TZS milioni 15.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala na Mabadiliko ya Kidijitali wa Exim, Silas Mtoi, alisema kampeni hii ni hatua muhimu katika safari ya taifa kuelekea uchumi unaotumia malipo ya kidijitali.

“Mteja akitumia kadi dukani au mtandaoni anapata usalama, kasi na urahisi. Tunataka kuchochea matumizi ya malipo ya kisasa na kupunguza utegemezi wa fedha taslimu nchini,” alisema Mtoi.

Wateja wa Exim pia watanufaika na zawadi na punguzo maalum katika maduka ya Shoppers na Village Supermarket, pamoja na ofa maalum kwenye migahawa na maeneo ya burudani, ikiwemo Karambezi Café na CIP Lounge katika uwanja wa ndege.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Stanley Kafu, alisema kampeni hii imeundwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wateja katika msimu wa sikukuu.

“Iwe ni maandalizi ya sherehe, safari, kununua mahitaji ya familia au kulipia ada za shule, malipo kwa kutumia kadi ya Exim yanampa mteja urahisi, usalama na nafasi zaidi ya kushinda,” alisema.

Aliongeza kuwa kampeni hii ni sehemu ya mkakati wa Exim katika kuharakisha mabadiliko ya kidijitali nchini.

Mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania aliipongeza Benki ya Exim kwa kuendesha kampeni inayoakisi uwazi, ukweli na maslahi ya wateja. Aliahidi kuwa droo zote za washindi zitasimamiwa kwa uadilifu na bila upendeleo.

Kwa mujibu wa Exim, ongezeko la matumizi ya kadi litasaidia kupunguza hatari za kubeba fedha taslimu na kuimarisha mfumo wa kifedha wenye ufanisi zaidi. Benki hiyo imewataka wateja wote kushiriki na kufurahia msimu wa sikukuu kupitia kampeni hii.

Kampeni ya “Chanja Kijanja, Dili Ndio Hili” inatarajiwa kuvutia maelfu ya washiriki huku ikibadilisha namna Watanzania wanavyofanya malipo katika msimu wa sikukuu na hata baada ya msimu huo.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: