Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam Desemba 18, 2025: Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kuanza kwa mchakato mpana wa mapitio ya kanuni, sheria na ada za leseni zinazosimamia vyombo vya habari vya mtandaoni, kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wadau wa sekta hiyo wakidai mfumo wa sasa unakandamiza ubunifu na kuua ajira kwa vijana.

Hatua hiyo imetangazwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Kuwe Bakari, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa Serikali, mabloga na waandishi wa habari za mtandaoni jijini Dar es Salaam. Dkt. Bakari alisema Serikali imeamua kusikiliza kilio cha wadau hao na kutafuta suluhu ya kudumu.

Alibainisha kuwa gharama kubwa za leseni pamoja na urasimu wa kikanuni vimekuwa vikwazo vikubwa vinavyowafanya waandishi wengi wa mtandaoni kushindwa kurasimisha shughuli zao. Ili kupata mapendekezo yenye tija, alisema TCRA imeelekeza Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA) kuteua wajumbe wanne watakaoungana na jopo la wataalamu wa TCRA kufanya mapitio ya ada na sheria husika.

“Tunahitaji mfumo unaolinda maslahi ya taifa lakini pia unaowezesha vijana wetu kunufaika na ubunifu wao. Ndiyo maana tumeamua kufanya kazi hii kwa pamoja,” alisema Dkt. Bakari.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, aliwasilisha uchambuzi unaoonesha kuwa Tanzania ina vizingiti vikubwa ikilinganishwa na nchi jirani za Afrika Mashariki. Alieleza kuwa wakati mwanablogu wa Tanzania analazimika kulipia kati ya Shilingi 500,000 hadi zaidi ya Shilingi milioni moja kwa ada za maombi na leseni, nchini Kenya hakuna hitaji la leseni ya gharama hiyo, huku Uganda ada ikiwa kati ya Shilingi 60,000 hadi 100,000.
Msimbe alisema hali hiyo inawafanya mabloga wengi kutumia mtaji wao kulipia gharama za kiserikali badala ya kuwekeza katika vitendea kazi muhimu kama kamera, kompyuta na vifaa vya kurekodia, jambo linalopunguza ushindani wao katika soko la kikanda na kimataifa.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuachana na mtazamo wa adhabu dhidi ya waandishi wa habari za mtandaoni na badala yake kuanza kuwalea kupitia uwezeshaji wa kiuchumi.

Bw. Msigwa alitangaza kuwa Serikali iko katika mchakato wa kuanzisha mfuko maalum utakaolenga kuwawezesha mabloga na waandishi wa mtandaoni kumiliki vitendea kazi vya kisasa na kukuza taaluma zao.

Alifafanua kuwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha waandishi wa habari za mitandaoni na mabloga—ambao wengi wao ni vijana wa kizazi cha Gen Z—wanatambuliwa kama washirika muhimu wa maendeleo ya taifa na si watu wa kuandamwa na faini na vikwazo pekee.

Kuhusu changamoto za kodi, Msigwa alisema Serikali itakaa meza moja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutafuta suluhu ya kodi kubwa ambazo hazilingani na kipato cha waandishi wa mtandaoni. Alisisitiza kuwa blogu zinapaswa kutambuliwa kama biashara ndogo na za kati (SMEs) zinazochangia pato la taifa kupitia utalii, uwekezaji na mawasiliano ya kimkakati.

Lengo la mchakato huo, kwa mujibu wa Serikali, ni kujenga mazingira rafiki yatakayochochea ubunifu wa vijana, kuongeza ajira na kuhakikisha sekta ya habari za mtandaoni inakuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: