KAMA mtu ataandaa Tuzo kwa ajili ya taasisi yenye bahati mbaya zaidi hapa nchini kwa sasa, sina shaka taasisi hiyo itakuwa ni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Na kama tuzo hiyo inatakiwa kushindaniwa na watu; basi mshindi atakuwa kati ya Rais wa TFF, Wallace Karia au Katibu Mkuu, Wilfred Kidao.

Kama kama viatu ambavyo nisingependa kuvivaa kwa sasa, basi vitakuwa ni viatu vya wawili hawa au taasisi hii.

Wao ndiyo viongozi wa kwanza katika muda wa miongo minne hapa Tanzania kufanikisha nchi yetu kushiriki katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2019) yaliyofanyika nchini Misri. Kwa kutumia Kiswahili kinachoeleweka, hawa ndiyo viongozi wa TFF ambao wamefanikisha hili baada ya miaka takribani 40 ya kutafuta fursa hii.

Kwa mtu ambaye hajui nini maana ya miaka 40, anatakiwa kujifunza kuhusu safari ya Waisraeli kutoka utumwani Misri (sadfa nyingine hii) kwenda Kanani.

Baada ya mafanikio hayo ya kujivunia, kuna watu leo wanapendekeza eti uongozi mzima wa TFF ujiuzulu kwa Stars kufanya vibaya kwenye mashindano hayo. Mojawapo
ya mambo yaliyonishangaza zaidi wiki hii ni hili. Tangu lini Watanzania wakaadhibiana kwa kufanya vizuri?

Na mfano unaotumika ni wa Misri. Eti tuige mfano wa Misri ambako kocha na Rais wa ‘TFF’ yao wamejiuzulu baada ya kutolewa na Afrika Kusini. Misri ni mabingwa wa kihistoria wa kombe hili na kwa sababu walikuwa wenyeji, kila mmoja alitaraji wangefanya vema. Hatua waliyochukua huko Misri ilitarajiwa.

Kuna mtu aliamini Tanzania ingetwaa ubingwa wa AFCON? Kuna mtu aliamini tungepenya katika kundi ambalo lilikuwa na timu za Senegal na Algeria? Senegal ilikuwa inapewa nafasi ya kutwaa kombe lakini kocha wao, Aliou Cisse, aliwaambia wanahabari katika mkutano wake wa kwanza walipofika Misri kwamba yeye alidhani Algeria wana nafasi kuliko wao.

Mpira huwa una matokeo ya ajabu na tungeweza kupenya lakini asilimia zaidi ya 80 tulijua kwamba tungeishia raundi ya kwanza tu. Tukaishia raundi ya kwanza hiyohiyo lakini ajabu ni kwamba watu wanadai tatizo ni TFF.

TFF ambayo imeita wachezaji wote waliotakiwa na mwalimu. TFF ambayo ilipeleka kambi ya timu katika nchi ambayo ilipendekezwa na mwalimu wa timu. TFF ambayo imepandisha hadhi ya Taifa kwa kuwaweka wachezaji katika hoteli za hadhi ya juu na hata kuwaongezea posho wachezaji wa timu hiyo?

TFF hii hii ambayo imetoka kufanikisha kufanyika kwa AFCON ya Vijana kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu? TFF hiihii ambayo imerejesha mashindano ya vijana ambayo yalitelekezwa katika miaka ya karibuni?

Ukimuuliza kila mpenda soka, atakwambia msingi wa maendeleo ya mchezo huu upo katika sehemu mbili; kukuza vijana na kufundisha walimu wa kutosha.

Nimemsikiliza Kidao mara nyingi katika mahojiano na waandishi wa habari na amekuwa akisisitiza kwamba sasa wanaelekeza nguvu zao katika maeneo hayo. Sasa hapo kosa la TFF, Karia, Kidao au Kamati ya Utendaji ya TFF ni ipi?

Mojawapo ya tatizo letu kama nchi ni kwamba mara nyingi tumekuwa hatujui tunachotaka. Tukipewa hiki, tunataka kile, tukipewa kile tunataka hiki. Mwaka mmoja uliopita, ungewauliza Watanzania wanataka nini, wangesema angalau tu watoe nuksi ya kwenda kushiriki Misri.

Wallace Karia na TFF yake leo walitakiwa wapongezwe kwa mafanikio yao. Kwenye uchaguzi ujao wa TFF, Karia angeweza kabisa kujitambulisha kama ‘RAIS WA AFCON’ na wenzake kumpa kura za kutosha. Hii ni kwa sababu amefanikisha mfupa uliowashinda wengi.

Wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, TFF ilipewa kila aina ya msaada ikiwamo kulipiwa kocha wa timu ya taifa lakini bado Taifa Stars haikufuzu. Leo hii, TFF inalipa gharama zote yenyewe na bado imefanikisha jambo ambalo hakuna aliyetalitarajia mwaka mmoja tu uliopita.

Mimi ningedhani Watanzania sasa wangejikita kwenye kuishauri TFF kuhusu mapungufu yaliyopo na lipi la kufanya ili sasa tuanze kuwaza kucheza Kombe la Dunia huko mbeleni.

Tushauri, tukosoe lakini tuwape nafasi watu ambao tayari wameweka rekodi na kuonyesha kwamba wanaweza kufanya makubwa zaidi endapo watapewa muda na nafasi ya kufanya waliyoyapanga.

Tuwape nafasi TFF wafanye kazi.

Ezekiel Kamwaga
Dar es Salaam
10 Juni 2019
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: