
Huu ni ujumbe wa onyo la wazi na la dhati—afya si jambo la kubahatisha wala la kusukuma mbele kwa sababu yoyote ile. Kwa muda mrefu tumekuwa na mazoea ya kupuuza dalili ndogo ndogo, tukijipa faraja kwamba ni uchovu wa kazi, msongo wa mawazo, au athari za starehe za muda mfupi. Ukweli mchungu ni kwamba magonjwa mengi hayaanzi kwa kelele; huanza taratibu, kimya kimya, hadi pale yanapofikia hatua mbaya ambapo gharama yake huwa kubwa—kimwili, kifedha, na hata kisaikolojia.
Ni muhimu kuelewa kwamba mwili wako huwa unatoa ishara mapema kabisa. Maumivu ya mara kwa mara, uchovu usioelezeka, kizunguzungu, au hata mabadiliko madogo ya kawaida ya mwili—hivi vyote vinaweza kuwa ni tahadhari. Lakini wengi wetu huchagua kuvipuuzia, aidha kwa sababu ya shughuli nyingi, hofu ya kugundua tatizo, au imani kwamba “bado niko sawa.” Hapo ndipo tunapokosea.
Ukweli ni huu: kuchelewa kuchukua hatua kunaweza kugharimu maisha. Ugonjwa unapokuwa umechelewa kugundulika, matibabu yake huwa magumu zaidi, gharama zake huongezeka, na wakati mwingine hata uwezekano wa kupona hupungua. Wakati mwingine tunajikuta tukitumia nguvu nyingi kupambana na kitu ambacho kingeweza kuzuilika au kudhibitiwa mapema kabisa.
Kwa vijana hasa, kuna changamoto ya maisha ya kasi—kazi, starehe, mitandao, na pilika pilika zisizoisha. Katika harakati hizi, afya huwekwa pembeni. Wengine huona kwenda hospitali kama kupoteza muda, au huogopa majibu watakayopata. Lakini ukweli ni kwamba, kujua hali yako ya afya mapema ni nguvu, si udhaifu. Ni hatua ya ujasiri na kujipenda.
Ni wakati sasa wa kubadili mtazamo:
Afya iwe kipaumbele, si chaguo la ziada.
Kufanya uchunguzi wa afya iwe sehemu ya ratiba yako ya kawaida, si jambo la dharura tu.
Kusikiliza mwili wako iwe kawaida, si mpaka uumie sana ndipo uchukue hatua.
Jamii yenye watu wenye afya bora ni jamii yenye nguvu, maendeleo, na ustawi. Lakini jamii inayopuuzia afya yake hujikuta ikikumbwa na mzigo mkubwa wa magonjwa, vifo vya mapema, na hasara zisizo za lazima.
Hivyo basi, huu ni wito wa tahadhari kwa kila mmoja:
Usisubiri hadi hali iwe mbaya.
Usidharau dalili yoyote.
Usikimbie ukweli wa afya yako.
Chukua hatua sasa. Jilinde. Jipende. Afya yako ni jukumu lako.
Je, una watu? Kama huna, jitahidi kutengeneza watu.
1. Siku ukikumbwa na kesi au kupelekwa mahabusu, una watu wa kukusaidia au ni mwisho wa safari? Kama huna, tengeneza watu.
2. Siku ukilazwa hospitali, una watu wa kukuletea msaada wa chakula na bili? Kama huna, tengeneza watu.
3. Siku unapokwama hata nauli ya chakula, una mtu wa kukukopesha hata kidogo? Kama huna, tafuta watu.
4. Siku unapofukuzwa kwenye nyumba, una watu wa kunusuru mali zako? Kama huna, tengeneza watu.
5. Siku unapokamatwa kwa kosa barabarani, una mtu wa kukushauri au kukusaidia kisheria? Kama huna, tengeneza watu.
6. Nafasi za ajira zinapotangazwa (polisi, jeshi, ualimu n.k.), una watu wa kukupa taarifa sahihi na kukushauri? Kama huna, tengeneza watu.
7. Unapodhulumiwa mali zako, una watu wa kukulinda na kukusimamia? Kama huna, tafuta watu.
8. Una sifa zote za kupandishwa cheo au kuteuliwa, lakini una watu wa kukusemea? Kama huna, tengeneza watu.
9. Unapobambikiziwa kesi nzito, una watu wa kukusaidia kutafuta haki? Kama huna, tengeneza watu.
10. Unapoanzisha au kupanua biashara, una watu wa kukufungulia milango na kupunguza vikwazo? Kama huna, tafuta watu.
Ukweli ni kwamba dunia hii inaendeshwa kwa watu.
Elimu bila mtandao wa watu mara nyingi haina matokeo makubwa. Biashara bila watu haisongi. Siasa bila watu hukwama. Kipaji bila watu hufifia. Mafanikio bila watu ni ndoto ngumu kufikia.
Watu ni maisha. Watu ni mtaji. Watu ni fursa.
Hakikisha una watu serikalini, mtaani, hospitalini, mahakamani, kazini, kwenye biashara, na hata nje ya nchi.
Huo ndio mtandao wa mahusiano — kwa Kiingereza huitwa connection.
Jenga mahusiano, linda watu wako, heshimu watu — utapunguza kwa kiasi kikubwa ugumu wa maisha.
Ndoa ni taasisi nyeti inayohitaji busara, uvumilivu, mawasiliano na heshima kutoka kwa pande zote mbili. Changamoto nyingi zinazojitokeza katika ndoa za kisasa hazitokani na jinsia, bali na mitazamo, malezi na tabia binafsi. Zifuatazo ni baadhi ya mienendo inayoweza kuathiri uimara wa ndoa endapo haitasimamiwa kwa hekima.
Kwanza, kujikita zaidi kwenye sura au mvuto wa nje kuliko tabia na maadili kunaweza kuleta changamoto. Uzuri ni neema, lakini unapokuwa msingi pekee wa mahusiano bila kujengwa na maadili, unyenyekevu na mawasiliano, ndoa inaweza kuyumba. Urembo bila busara unaweza kusababisha matarajio yasiyo halisi na kukosa uthabiti wa kihisia.
Pili, changamoto zinazoweza kuja pamoja na elimu bila unyenyekevu. Elimu ni baraka kubwa, lakini pale ambapo mmoja wa wanandoa anatumia elimu kama chanzo cha majivuno, dharau au kutotaka kushirikiana, inaweza kuathiri mahusiano. Ndoa bora hujengwa juu ya ushirikiano, si mashindano ya nani anajua zaidi.
Tatu, malezi na mazingira ya maisha ya utotoni yanaweza kuathiri namna mtu anavyoingia na kuendesha ndoa. Wale waliokulia katika mazingira ya maisha ya juu wanaweza kupata ugumu wa kuzoea maisha tofauti baada ya ndoa ikiwa hawajajifunza kubadilika na kushirikiana. Hili si kosa, bali ni eneo linalohitaji mazungumzo na kuelewana.
Nne, kutokuwepo kwa uwiano kati ya majukumu ya kiroho, kazi na familia pia kunaweza kuleta changamoto. Iwe mtu ni kiongozi wa dini, msanii, mfanyabiashara au mtumishi wa kawaida, familia inahitaji muda, upendo na uwepo wa kihisia. Maisha ya kiroho ni muhimu, lakini hayapaswi kuwa sababu ya kupuuzia wajibu wa kifamilia.
Kwa ujumla, ndoa haidumu kwa sababu ya uzuri, elimu, fedha wala hadhi ya mtu, bali hudumu kwa sababu ya unyenyekevu, heshima, uaminifu, mawasiliano mazuri na moyo wa kujifunza. Mwanamume na mwanamke wanapojenga mahusiano kwa misingi hiyo, ndoa nyingi zinaweza kudumu na kuwa chanzo cha furaha badala ya maumivu.
Katika maisha jifunza jambo kubwa:
Ukidhalilishwa, usighadhibike.
Ukitengenezewa fitna, usichukie.
Ukiwekewa ukuta, usijaribu kuubomoa kupita kwa nguvu.
Ukitengenezewa majungu, umia lakini jikaze.
Mungu ana njia zake za kukufariji, na pia ana namna zake za kuwaadhibu wale wanaokuumiza. Subira ni silaha kubwa.
Weka moyoni mwako kumbukumbu za watu hawa katika maisha yako:
Aliyekuinua wakati ulikuwa chini.
Aliyekuhifadhi wakati huna pa kujihifadhi.
Aliyekuacha ukiwa kwenye giza la matatizo.
Aliyekupa heshima wakati ukidharauliwa.
Aliyekupa thamani uliponyimwa thamani.
Aliyekusogelea wakati wengine walikukimbia.
Unapopitia maumivu, usijiumize zaidi kwa kumfikiria sana yule aliyekuletea machungu. Dawa ya maumivu ni kukubali hali, kusimama imara, na kusonga mbele. Usijiumize kwa sababu kufanya hivyo ni kutimiza malengo ya yule aliyekutesa.
Kauli ya, “Sikuamini kama fulani anaweza kunifanyia hivi,” imetoka kwa wengi walioumizwa na watu wao wa karibu. Ili ujilinde, nenda kwenye kioo na muamini unayemuona humo – huyo ndiye usalama wako wa kweli. Wengine wape furaha, lakini usiwape imani yako yote.
Kumbuka: Ukiishi kwa kuumiza wengine, Mungu hukuletea watu wa kukuumiza wewe na kizazi chako. Lakini ukiishi kwa kuwafariji na kuwapa furaha wengine, Mungu hukuletea watu wa kukuinua na kukufurahisha. Wema husafiri mbali, lakini uovu husafiri mbali zaidi.
Muda hauwezi kubadilisha mtu, bali hufichua sura yake halisi. Kadiri unavyosubiri, ndivyo muda utakavyokuletea majibu ya kweli kuhusu watu wanaokuzunguka. Kuwa mtulivu, muda ndio shahidi wa haki.
Maisha haya tumeazimwa kila kitu: uhai, afya, uzuri, ubaya, utajiri na hata umasikini. Siku Mungu akiamua, huchukua tu alichotuazima bila kutuomba ruhusa wala kutuandaa. Kwa sababu hiyo, tuishi maisha kwa nidhamu, kwa unyenyekevu na heshima – maana cha kuazimwa si cha kutamba nacho.














.jpeg)

