TRENDING NOW






Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya siku moja kuhusu sharia za uchaguzi kwa Maafisa Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya nchini. Mafunzo hayo yamefanyika leo Oktoba 17, 2024 jijini Dodoma. Pamoja nae ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Ramadhani Kingai.
***********
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Maafisa wa Polisi nchini wametakiwa kujenga tabia ya kujikumbusha sheria mbalimbali ikiwemo zinazohusu masuala ya uchaguzi ili kuepuka kuyumbishwa na wanasiasa wanaoamua kupotosha yaliyomo katika sheria hizo kwa maslahi yao binafsi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani wakati akifungua mafunzo ya Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya nchini yaliyofanyika leo Oktoba 17, 2024 mkoani Dodoma.

Kailima amesema, mafunzo ya aina hii ni muhimu kwa kipindi hiki ambacho kuna Sheria Mpya mbili zinazosimamia masuala ya Uchaguzi. Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024.

“Katika sheria zote mbili yapo mabadiliko makubwa katika maeneo mbalimbali ambayo ni muhimu sana kwenu kuyafahamu kipindi hiki ambacho uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga unaendelea na mwakani itakuwa ni uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani,” alisema Kailima.

Aliongeza, mafunzo hayo kuhusu sheria za uchaguzi yana umuhimu na maana kubwa katika maandalizi ya zoezi zima na mchakato wa kuelekea chaguzi zilizopo mbele yetu kama Taifa.

“Uelewa wenu kuhusu sheria hizi, utasaidia sana usimamiaji wa sheria na kuchukua hatua za udhibiti wa uvunjifu wa sheria hizo pamoja na sheria zingine ili watakaokiuka sheria hizo waweze kufunguliwa mashtaka ipasavyo na kuwatendea haki kwa kitakachoamuliwa na Mahakama,” alisisitiza Kailima.

Aliendelea kwa kusema kuwa, anaamini kuwa baada ya mada inayohusu sheria za uchaguzi kuwasilishwa wakuu hao wa upepelezi watakuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kwenda kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pindi zoezi linapofanyika katika maeneo yao.

Lengo la mafunzo kwa maafisa hayo ni kuwajengea uelewa kuhusu haki za vyama, wananchi na makundi mengine katika vipindi vyote vya uchaguzi, kwa maana kabla ya uchaguzi Mkuu, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Pamoja na masuala ya Sheria za uchaguzi, washiriki hao ambao ni Wakuu wa Upelelezi walipata kujua wajibu wa Jeshi la Polisi wakati wa uchaguzi, Bank Note Security features, utambuzi wa bidhaa bandia na hatimiliki, upelelezi sambamba na utafiti katika mapungufu ya kisheria.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Ramadhani Kingai (kulia) akifafanua jambo akati wa mafunzo ya siku moja kuhusu sharia za uchaguzi kwa Maafisa Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya nchini. Mafunzo hayo yamefanyika leo Oktoba 17, 2024 jijini Dodoma. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Bw. Selemani Mtibora akiwapitisha katika maeneo muhimu yaliyomo kwenye Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024.


Mkurugenzi wa Daftari na Tehama wa INEC, Stanslaus Mwita akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani (kushoto) akizungumza jambo na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Ramadhani Kingai wakati wa mafunzo ya siku moja kuhusu sheria za uchaguzi kwa Maafisa Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya nchini. Mafunzo hayo yamefanyika leo Oktoba 17, 2024 jijini Dodoma.

Washiriki wakifuatilia mada


Washiriki mbalimbali ambao ni Wakuu wa Upelelezi Wilaya na Maofisa wengine mbalimbali wakishiriki katika mijadala kuhusu sheria za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.






●Itafanyika ndani ya nchi na nje ya nchi

●Itaendeshwa na Tume ya Madini kushirikiana na Soko la Bidhaa Tanzania

●Marekebisho ya Sheria na Kanuni yakamilika

⚫️ Ni utekelezaji wa Rais Samia kukuza biashara ya Tanzanite


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Madini inarudisha minada ya ndani ya madini ya vito itakayofanyika katika maeneo ya uzalishaji hususan Mirerani, Mahenge, Tunduru, Dar es salaam, Arusha na Tanga na kimataifa itafanyika mji wa Bangkok na Jaipur nchini Thailand.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 16, 2024 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini jijini Dodoma.

Waziri Mavunde amesema kuwa baada ya taratibu za marekebisho ya kisheria kukamilika juu ya uendeshaji wa minada hiyo wanatarajia ndani ya muda mfupi ujao kuanza taraibu za kuweka miundombinu ya kuanza minada ya ndani.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa, uendeshaji wa maonesho na minada ya kimataifa nchini ni fursa muhimu ya kutangaza madini ya vito yanayozalishwa hususan kwenye masoko ya kimataifa ambayo ni njia mojawapo ya kuwafikisha watanzania katika masoko ya uhakika na upatikanaji wa bei nzuri na stahiki.

Waziri Mavunde ameieleza Kamati ya Nishati na Madini kuwa, Mpango wa kurejesha minada ya madini ya vito ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha jijini Mwanza tarehe 13 Juni, 2024.
Kwa upande wake , Naibu Waziri wa madini Dkt.Steven Kiruswa amesema, kwa sasa wataalam wa Wizara ya Madini wamepata uzoefu mkubwa katika minada na maonesho ya kimataifa baada ya kujifunza namna biashara za kimataifa zinavyofanyika pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye mnyororo mzima wa thamani madini katika nchi mbalimbali ikiwemo Marekani , India , Afrika Kusini na Thailand.
Awali, akiwasilisha taarifa kuhusu uboreshaji na utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Masoko na vituo, minada ya ndani na kimataifa ya madini ya vito kwa Kamati hiyo, Kaimu Mtendaji Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema kuwa, minada hiyo itaendeshwa na Tume ya Madini kwa kushirikiana na Soko la Bidhaa la Tanzania (TMX) kupitia mfumo wa mauzo wa kielektroniki ambapo usimamizi utahusisha shughuli za uthaminishaji na upangaji wa madini ili kuweza kupata bei nzuri kulingana na madini husika,akisisitiza kwamba lengo kuu ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito na usonara barani Afrika.

Mhandisi Lwamo ameongeza kuwa, minada ya vito itaifungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo Utalii na biashara katika kipindi husika ikiwa ni pamoja na kuliingizia taifa fedha za kigeni.
Pamoja na mambo mengine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. David Mathayo ameendelea kumpongeza Waziri wa Madini na wasaidizi wake kwa kazi nzuri ya kuisongesha Sekta ya Madini katika ngazi ya kimataifa inayoleta tija katika uchumi wa nchi na hasa katika mkakati wa kurudisha hadhi na thamani ya madini ya vito yakiwemo madini ya Tanzanite ambayo ni madini yanayopatikana Tanzania peke yake.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Kassim akizindua Wiki ya Vijana kitaifa uliofanyika Jijini Mwanza.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Kassim   amewataka vijana wa Kitanzania kutumia fursa za maendeleo ya kidigitali kama njia ya kujitengenezea fursa za ajira na kuacha kutumia mitandao ya kijamii kwa mambo yasiyofaa.

Mhe. Majaliwa amewataka vijana kufichua na kuziainisha taasisi zenye nia ovu ya kuharibu na kuvunja mila na desturi za Kitanzania, pamoja na taasisi hizo binafsi kujitambulisha na kutoa malengo ya Taasisi.

Katika kuadhimisha siku ya Vijana Kitaifa, Shirika lisilo la kiserikali la BRAC Maendeleo Tanzania,limeadhimia kuendelea na kuwekeza kwenye kutoa elimu zaidi kuhusiana na maendeleo ya vijana

Akizungumzia maadhimisho hayo, Meneja wa Mkoa Mwanza Novatus Tarimo amesema elimu wanayotoa kwa vijanai ni  kuwawezesha vijana kupaza sauti kwa Serikali na  jamii ili waweze kujiinua kiuchumi kupitia fursa mbalimbali zilizopo.

Amesema, Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania limekuwa na miradi ya uwezeshaji kiuchumi kwa vijana na ikiwa ni katika  kuunga mkono Serikali ya awamu ya sita kwa kuwainua kiuchumi na kuwapa fursa za kujiajiri.

Tarimo amesema,  wao ni Wadau namba moja wa maendeleo na wamekuwa wakifanya kazi na Serikali kwa ngazi ya kitaifa na  kuwekeza kwenye kutoa hamasa kutokana na matakwa muhimu kwa wakati huo.

 "Vijana ndio taifa la kesho, kuna kila sababu ya kuwasaidia vijana hawa kwa kupaza sauti zao na kuwapatia elimu ya zaidi ili waweza kujiendeleza na kujiinua kiuchumi na kujiajiri,"amesema Tarimo.

"Mradi wa AIM, unaojihusisha na utoaji wa elimu na uwezeshaji wa kiuchumi na katika kipindi chote umekuwa na mafanikio makubwa sana,"

BRAC Maendeleo ni shirika lililojikita katika kuwezesha kiuchumi vijana kwa elimu ya ujasiriamali, na kwa kutoa mikopo ya vikundi kwa wakina.mama kupitia BRAC Finance Limited.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Kassim aizungumza na Vijana waliojitokeza katika viwanja hivyo  amewataka vijana wa Kitanzania kutumia fursa za maendeleo ya kidigitali kama njia ya kujitengenezea fursa za ajira na kuacha kutumia mitandao ya kijamii kwa mambo yasiyofaa.Maandamano ya wafanyakazi na vijana wa BRAC Maendeleo Tanzania wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yaliyofanyika Jijini Mwanza.
Wananchi wakipita na kupata maelezo kutoka wafanyakazi wa BRAC Maendeleo Tanzania kuhusiana na uwezeshaji wa Vijana nchini
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatarajia kuanza rasmi usimamizi wa shughuli zote za kibandari katika mwalo wa Kirumba ulipo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza kufuatia tangazo lililotolewa kwenye gazeti la Serikali.

Akitoa taarifa kwa umma Ijumaa Oktoba 11, 2024 kupitia waandishi wa habari, Meneja Bandari Kanda ya Ziwa Victoria, Erasto Lugenge alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa tangazo la Serikali namba 855 la tarehe 24/12/2023 ambalo linaipa TPA mamlaka ya kusimamia mialo yote iliyo rasmi.

Lugenge aliongeza kuwa shughuli za usimamizi wa mwalo huo zitaanza kesho rasmi Jumamosi Oktoba 12, 2024 zikihusisha usimamizi wa usalama wa vyombo vya majini.

Awali mwalo huo ulikuwa ukisimamiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ukiwa ni miongoni mwa mialo 10 katika Ziwa Victoria iliyotangazwa kusimamiwa na TPA.
Na George Binagi- GB Pazzo, Mwanza.
Meneja Bandari Kanda ya Ziwa Victoria, Erasto Lugenge akitoa taarifa kwa umma kuhusu TPA kuanza kuusimamia mwalo wa Kirumba wilayani Ilemela.

Meneja Bandari Kanda ya Ziwa Victoria, Erasto Lugenge akizungumza na wanahabari jijini Mwanza.
Tazama Video hapa chini
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeanza uchimbaji wa kisima eneo la Kisasa-Mwangaza Jiji Dodoma baada ya maagizo ya Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb.) kwa DUWASA kutafuta suluhisho la changamoto ya maji katika maeneo ya Kisasa Bwawani, Kisasa East, Nyumba 300 na Mwangaza.

Zoezi la uchimbaji wa kisima hicho umeanza Oktoba 11 na utakamilika Oktoba 12, 2024 huku hatua inayofuata ni upimaji wa wingi wa maji na ubora wa maji kabla ya kuanza uendelezaji wa kisima hicho.

Uchimbaji kisima eneo la Kisasa - Mwangaza ni hatua ya utatuzi wa changamoto ya ukosefu wahuduma ya maji kwa wananchi wa maeneo ya Kisasa Bwawani, Kisasa East, Nyumba 300 na Mwangaza.

Baadhi ya Wananchi na Viongozi wa Serikali ya Mtaa Nyumba 300 na Mwangaza wameishukuru serikali kwa kusikia kilio chao katika kuwapatia huduma ya maji.

Viongozi na wananchi waliotembelea uchimbaji wa kisima hicho leo ni Donatha Zitatu - Mwenyekiti wa Mtaa Nyumba 300, Vicent Malisa Balozi Mwangaza, Pendo Masigati- Mwananchi wa Nyumba 300 na Mathew Laurent- Balozi Nyumba 300.

Katika jitihada zake za kuendelea kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekutana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi kuzungumzia masuala ya usalama wa usafiri wa majini kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kanali Mtambi ameipongeza TASAC kwa hatua mbalimbali wanazochukua kuimarisha masuala ya usafiri wa majini na ushirikiano wanaoutoa katika Mkoa wa Mara na hususan usalama wa wasafiri katika katika Ziwa Victoria.

Kanali Mtambi ameiomba TASAC kuendelea kutoa elimu kuhusu sheria na kanuni zinazohusiana na usafiri wa majini kwa wananchi na taasisi za Serikali na binafsi ili kupunguza ajali na athari za ajali za vyombo vya usafiri wa majini.
“Sisi kama Serikali tunatakiwa kuendelea kuwahakikishia usalama watumiaji wa Ziwa Victoria ikiwemo wasafiri wanaotumia vyombo vya usafiri vya majini kuhusiana na usalama wao wanapotumia usafiri wa majini,” amesema Mhe. Kanali Mtambi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira na Usafiri wa Majini, Bi. Leticia Mutaki amesema TASAC inaendelea na jukumu lake la utoaji wa elimu ya usalama wa usafiri majini kwa wadau wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo taasisi na Halmashauri kuhusiana na usimamizi wa usafiri wa majini.
“Tuna mpango wa kuingia katika makubaliano ya ushirikiano na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Halmashauri zote zinazopakana na ziwa ili Halmashauri zisaidie kusimamia usafiri wa majini kwa niaba ya TASAC,” amesema Bi. Mutaki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TASAC, Bi. Judith Kakongwe amesema Sheria na kanuni za sasa zinawabana zaidi wenye vyombo vya usafiri kuweka jaketi okozi lakini haziwabani abiria kuzivaa jambo ambalo linaleta changamoto kwa sababu wamiliki wakiweka bila kuvaliwa hazisaidii kama inatokea ajali.

“Tupo kwenye mchakato wa kubadili vipengele vya sheria na kanuni ili abiria nao wabanwe kuvaa jaketi okozi na sio tu wamiliki wa chombo kama ilivyo sasa ili kusaidia kupunguza madhara ajali zinapotokea” amesema Bi. Kakongwe.