Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limewaasa wananchi wa wilaya ya Kigoma kuzingatia usalama na utunzaji wa mazingira wanapofanya shughuli za usafiri majini ikiwa ni pamoja na kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) nchini.
Hayo yamesemwa na Afisa Mfawidhi Mkoa wa Kigoma Nahodha. Adam Mamilo wakati wa kutoa elimu ya Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira majini iliyofanyika katika Ukumbi wa Kigoma Social mkoani Kigoma.
Nah. Mamilo amewaasa wananchi kuzingatia kanuni za usalama, ulinzi na utunzaji mazingira kama zinavyodhibitiwa na TASAC ili kuokoa maisha, pamoja na kuzingatia taarifa za TMA ili kujiepusha na athari zinazoweza kutokea wanapofanya shughuli zao kwa majini.
“Nawasihi wananchi wanaojishughulisha na shughuli yoyote majini, kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya usafiri majinoi ili kujiepusha na madhara yanayoweza kutokea ikiwemo ajali majini. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha tuna vifaa vya kujiokolea katika vyombo vyetu vya usafiri na hii ni pamoja na jaketi okozi na vifaa vya kuzimia moto. Lakini pia tuzingatie taarifa zinazotolewa na TMA,” amesema Naho. Mamilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mabaharia (TASU), Kanda ya Magharibi inayohusisha Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa, Bw. Issa Mussa amesema kuwa wananchi hasa wamiliki na waendesha vyombo pamoja na wavuvi wanapaswa kuzingatia kanuni na taratibu ili kujiepusha na madhara yanayoweza kutokea kwa kutozingatia miongozo hiyo ya usafiri majini.
“Kwa kweli tuna changamoto ya kuzingatia kanuni na sheria za usafiri majini na kusababisha watu kupoteza maisha majini. Hivyo tutaendelea kuhamasisha kufuata sheria na kanuni hizo kwa usalama wetu” amesema Bw. Mussa.
Zoezi la utoaji elimu ni zoezi endelevu linalozingatia mpango wa elimu kwa umma kutoka TASAC katika kutekeleza majukumu yake.

Toa Maoni Yako:
0 comments: