Articles by "WAZIRI MKUU"
Showing posts with label WAZIRI MKUU. Show all posts
Na Mwandishi Wetu.

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini nchini katika kulinda amani, kuimarisha maadili na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumapili (Machi 15, 2026) wakati akitoa salamu katika Ibada iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mpanda Mjini, Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, iliyoongozwa na Askofu Imani Ahobokile Chibona.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika kujenga Taifa lenye hofu ya Mungu, upendo, haki na uwajibikaji.

“Nimekuja pia na salamu za upendo kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye anatambua mchango mkubwa wa taasisi za dini katika kudumisha amani, maadili mema na mshikamano wa kitaifa,” amesema.





Waziri Mkuu amesema taasisi za dini zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi, hususan katika sekta za elimu, afya na malezi ya jamii.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Katavi ikiwemo miradi ya maji, barabara na nishati kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.

Akizungumzia sekta ya maji, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 ambapo jana aliweka jiwe la msingi la mradi wa kusambaza maji kutoka Bwawa la Milala unaotarajiwa kuzalisha lita milioni 12 za maji kwa siku na kuhudumia wakazi wa Manispaa ya Mpanda.

Katika sekta ya miundombinu, amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya Mpanda – Tabora yenye urefu wa kilometa 352 kwa kiwango cha lami ambayo imekuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huo.

Aidha, amesema ujenzi wa barabara ya Mpanda – Uvinza – Kanyani unaendelea ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 15.7, huku ujenzi wa barabara ya Kagwira – Karema nao ukiendelea kwa lengo la kufungua fursa za kiuchumi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Waziri Mkuu pia amesema Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme katika Mkoa wa Katavi ambapo vijiji vyote 172 tayari vimeunganishwa na umeme huku vitongoji 534 kati ya 912 vikifikishiwa huduma hiyo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa akisisitiza kuwa amani ya nchi ni matokeo ya jitihada za pamoja za Serikali, taasisi za dini na wananchi.

“Taifa letu limeendelea kuwa kisiwa cha amani kwa sababu ya mshikamano wa Watanzania. Tuendelee kuwa mabalozi wa amani katika familia, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla,” amesema.

Akizungumzia umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuwa mnufaika namba moja wa amani ni mwananchi mwenyewe na Taifa kwa ujumla.

“Tunapaswa kuepuka migogoro isiyo ya lazima hususan ya ardhi. Hata tukigombana au kupigana ardhi haiongezeki. Kilicho muhimu ni kukaa pamoja, kuzungumza na kushirikishana ili kutumia ardhi yetu kwa manufaa ya wote,” amesema.

Amesema kuendelea kwa migogoro ya ardhi kunaweza kuliweka Taifa katika mazingira yasiyo mazuri na kupelekea chuki pamoja na kuvunjika kwa umoja wa kitaifa. Ameongeza kuwa msingi wa maendeleo ya Taifa lolote ni amani, umoja na mshikamano, hivyo ni muhimu kuendelea kuliombea Taifa lisipoteze tunu hizo.

Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Dkt. Imani Ahobokile Chibona, amesema Kanisa linaendelea kuhimiza waumini kudumisha amani, mshikamano na maadili mema katika jamii kwani amani ya Taifa inaanza na mtu mmoja mmoja katika familia na jamii.

Askofu Chibona pia ameitaka jamii kuendelea kuwaombea viongozi wa kitaifa ili Mungu awape hekima, nguvu na afya njema katika kuliongoza Taifa, huku akisisitiza kuwa Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali.

Na Mwandishi Wetu, Babati - Manyara

WAZIRI MKUU, Dk. Mwigulu Nchemba, amewaagiza watendaji wote wa serikali nchini kuanza kuandaa jedwali maalum litakaloonesha namna walivyotatua kero za wananchi katika kila wiki ya mwisho wa mwezi, akisisitiza uwajibikaji na ufuatiliaji wa karibu wa huduma za umma.

Ametoa agizo hilo leo Machi 1, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi ya Zamani, Babati, mkoani Manyara.

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumilia hali ya kulimbikizwa kwa matatizo ya wananchi bila kuyapatiwa ufumbuzi kwa wakati, akibainisha kuwa uwepo wa viongozi na watendaji katika kila eneo unalenga kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa urahisi.

Amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali si kugawana vyeo bali kuwahudumia wananchi kwa vitendo, na kwamba ufuatiliaji mkali utaanza kufanyika ili kubaini watendaji wanaotekeleza majukumu yao ipasavyo na wale wanaoshindwa.

“Hatukutengeneza ofisi hizi za serikali ili kugawana vyeo. Tukianza kufuatilia kwa karibu, tutajua nani anaweza kazi na anastahili kubaki ofisini,” amesisitiza.

Kauli hiyo imekuja wakati Serikali ikiendelea kusisitiza uwajibikaji wa watendaji wa umma na kuimarisha mifumo ya kushughulikia malalamiko ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Na Mwandishi Wetu, Manyara.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, ametoa maagizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Manyara kufuatilia matumizi ya fedha zilizotumika katika ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto pamoja na ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo.

Ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo, akieleza kuwa amepokea taarifa za kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha katika utekelezaji wa mradi huo. Waziri Mkuu alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, kwa kufuatilia suala hilo na kufanikisha kurejeshwa kwa fedha zilizobainika kupotea, huku akisisitiza kuwa wahusika wote wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Akizungumza katika ziara hiyo, Sendiga alisema kuwa tangu kuanza kwa Awamu ya Sita, mkoa wa Manyara umepokea zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, akimshukuru Waziri Mkuu kwa kuanza ziara yake mkoani humo na kuendelea kusikiliza changamoto za wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Faraja Ngerageza, alisema mradi huo ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kuanza kutumika mwezi Machi mwaka huu.

Baadhi ya wananchi wa Kiteto walimshukuru Waziri Mkuu kwa kutembelea eneo hilo, kusikiliza kero zao na kuahidi kuzitatua, wakieleza kuwa ziara hiyo imeongeza matumaini ya kuboreshwa kwa huduma za maendeleo katika wilaya hiyo.

Ziara ya Waziri Mkuu inaendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara, ambapo kwa sasa yupo wilayani Simanjiro akizindua miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi.

Na Mwandishi Wetu, Arusha.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameibuka kinara wa Tuzo za Kitaifa za Uhifadhi na Utalii (Serengeti Awards) baada ya kutunukiwa Tuzo Maalum ya Kiongozi Mwenye Maono (Visionary Leadership Award) kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya Maliasili na Utalii nchini.

Tuzo hiyo ilitolewa katika hafla ya kitaifa iliyofanyika leo Januari 31, 2026, katika Ukumbi wa Mount Meru Hotel jijini Arusha, ikitambua uongozi wa kimkakati wa Rais Samia katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu maarufu za Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania, pamoja na juhudi zake za kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utalii na kuimarisha uhifadhi wa maliasili.

Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyesema jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita zimeendelea kuleta matokeo chanya katika sekta ya utalii. Alieleza kuwa kuanzia Januari hadi Novemba 2025, Tanzania ilipokea watalii wa kimataifa 2,097,823, ikiwa ni ongezeko la takribani asilimia 9.02 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa sekta ya Maliasili na Utalii inachangia takribani asilimia 21 ya Pato la Taifa, ambapo asilimia 17 inatokana na utalii na asilimia 4 kutoka sekta ya misitu na nyuki, huku sekta hiyo ikitoa ajira kwa takribani Watanzania milioni tatu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, alimpongeza Rais Samia kwa uongozi wake thabiti uliowezesha kuimarika kwa uhifadhi wa maliasili pamoja na ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo barabara na viwanja vya ndege katika maeneo ya hifadhi, hatua zilizorahisisha shughuli za utalii na kuongeza mvuto wa Tanzania katika soko la kimataifa.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na shabiki wa klabu ya Manchester City ya Uingereza, Braydon Bent, ambaye alieleza kuvutiwa na uzuri wa vivutio vya utalii vya Tanzania, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Ngorongoro, pamoja na ukarimu wa Watanzania, akisema safari yake nchini itaendelea kuwa kumbukumbu isiyosahaulika katika maisha yake.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza utalii, kulinda mazingira, na kuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka hifadhi wananufaika kiuchumi. Aidha, alihimiza matumizi ya teknolojia na ubunifu ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa la utalii.

Alimalizia kwa kuwakumbusha Watanzania kuwa amani ni tunu kuu ya Taifa, na kuwasisitiza kushirikiana kulinda rasilimali zilizopo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza katika Ibada ya Jumpili aliyoshiriki katika Usharika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Kisasa jijini Dodoma, Novemba 16, 2025.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwasisitiza Watanzania kuyaombea taifa ili amani, upendo na mshikamano viendelee kudumu nchini, akisema maombi ni nguzo muhimu ya utulivu wa taifa.

Wito huo umetolewa leo Jumapili, Novemba 16, 2025 na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, alipowasilisha salamu za Rais Samia kwa waumini na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kisasa mkoani Dodoma.

“Mheshimiwa Rais anawasalimu sana. Rai yake kwa Watanzania wote ni kuendelea kuiombea nchi yetu, tuwe watulivu na tuendelee kudumisha amani,” alisema Waziri Mkuu wakati akisoma salamu hizo.

Dkt. Mwigulu alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani ya nchi kwa sababu bila amani hakuna shughuli yoyote muhimu inayoweza kufanyika, ikiwemo ibada, maendeleo ya kijamii na utekelezaji wa mipango ya serikali.

“Pasipo amani hatuwezi kutekeleza majukumu yetu mengine. Pasipo amani hatuwezi hata kufanya ibada. Ndiyo maana tunapaswa kuiombea nchi yetu kila mara. Tukidumisha amani, tunaweza kukabiliana hata na mambo magumu,” alisema.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma, Dkt. Christian Ndossa, ambaye aliwahimiza waumini na Watanzania kwa ujumla kumtanguliza Mungu katika maisha yao, kuwa na matumaini na kujiepusha na matendo maovu.

Katika ibada hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na mke wake, Mama Neema Mwigulu Nchemba, sambamba na viongozi mbalimbali wa serikali na Bunge akiwemo Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo; Mbunge wa Kilolo, Ritha Kabati; Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya; Mbunge wa Viti Maalumu, Balozi Dkt. Pindi Chana; Mbunge wa Itigi, Yohana Msita na Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga.

Ibada hiyo imeendelea kuwa sehemu ya mwamko wa viongozi kuitaka jamii kuenzi amani kama msingi wa maendeleo ya taifa.

Na Mwandishi Wetu.

Alizaliwa mwaka 1960 katika kijiji kidogo cha Namoto, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi. Leo hii, jina la Kassim Majaliwa Majaliwa linaandikwa kwa heshima kubwa katika historia ya Tanzania. Safari yake ni ya kuvutia kutoka maisha ya kawaida kabisa hadi kuwa mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa taifa.
‎Kiu yake kubwa ilikuwa ni kufundisha, hivyo hakuchelewa alisomea ualimu katika Chuo cha Ualimu Mtwara na baadaye Chuo cha Ualimu Kitangali kilichopo Mtwara.
‎Alianza kuwa mwalimu, akilea vijana kwa bidii na maadili, Akawa mkufunzi katika Chuo cha Ualimu mtwara huku akijijengea misingi imara kwa huduma ya jamii,
‎Hakika alijitengeneza kama kiongozi mwenye maarifa, nidhamu, na mwelekeo wa maendeleo kwa taifa.
Kiu yake ya kujifunza iliendelea hadi alipopata shahada kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Open University of Tanzania).
‎Majaliwa aliyeanzia ualimu, ukufunzi wa chuo cha ualimu, ukatibu wa chama cha walimu, Ukuu wa wilaya ya Rufiji, Unaibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu tawala za mikoa na Serikali za motaa TAMISEMI yana hatimaye Waziri Mkuu wa –
‎ leo ameandika historia isiyo futika katika taifa letu.
‎CHAMA CHA WALIMU MKOA WA SINGIDA CWT wanamkumbuka zaidi hasa kipindi ambacho alianzisha, kusimamia na kukamilisha ujenzi wa jengo la ghorofa la ofisi za chama cha walimu mkoani Singida alipokuwa akihudumu kama Katibu wa CWT mkoani Singida.
‎Majaliwa amechagua historia imjadili katika maisha yake yote.
Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliiona nyota ya Majaliwa kutokea Singida, akamteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo alipowekwa kiti moto na wabunge wawili wababe wa wilaya hiyo – marehemu Samuel Sitta na Juma Kapuya waliokuwa wabunge wa Jimbo la Urambo na Kaliua.
‎Hamad, Majaliwa akahamishiwa wilaya ya Rufiji alipohudumu hadi mwaka 2010 ndipo alipoamua kujitosa jimboni Ruangwa kugombea ubunge wa jimbo hilo.
‎Hakika nyota njema iliyoanzia ualimu haikazimika baada ya uchaguzi huo ambapo siku anawaaga watumishi wa wilaya ya Rufiji alikohudumu kama mkuu wa wilaya baada ya kushinda ubunge.
‎Katikati ya maandalizi ya kuelekea jimboni, analisikia jina lake akiwa miongoni mwa manaibu mawaziri wa serikali ya Jakaya Mrisho Kikwete.
‎Mwaka 2010, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Ruangwa, kutokana ile kasi yake ya utendaji, jicho la hayati John Pombe Joseph Magufuli lilimuona Novemba 2015 na kumteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.
‎Mtu mwema aliyewahi kutokea katika ardhi ya nchi yetu.
Leo hii tunamzungumzia Kasim Majaliwa
‎Kiongozi imara ambaye ameziishi Enzi na kuziheshimu nyakati zake
‎Kwa ridhaa yake mwenyewe Ameamua kuuwaga Waziri Mkuu baada ya kutangaza kutogombea ubunge wa Ruangwa.
‎Vyovyote iwavyo, vyovyote itakavyotafsiriwa, na vyovyote itakavyoonekana – lakini ukweli usemwe, Majaliwa ameandika historia yake. Sio rahisi kwa kiongozi wa ngazi yake kuamua kung’atuka na kuachia madaraka makubwa kama Uwaziri Mkuu.
‎Watangulizi wake kadhaa iliwabidi wastaafu siasa baada ya kushindwa kupata uteuzi wa nafasi ya juu baada ya kuhudumu kama Waziri Mkuu. Naam, tulimuona hayati Msuya akishindwa urais na hayati Mkapa ndipo akastaafu rasmi siasa mwaka 1995. Ilimchukua hadi kushindwa urais na Jakaya Kikwete mwaka 2005 ndipo akaamua kuistaafu rasmi siasa na kuitwa Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye. Sio hao tu, hata Mizengo Pinda ilimbidi ashindwe kwanza kura za maoni za urais mwaka 2015 na kuteuliwa Magufuli ndipo akatangaza kustaafu siasa.
‎Tofauti kabisa na Majaliwa Kassim Majaliwa aliyetangaza kutogombea tena ubunge wa Ruangwa. Ifahamike kuwa kutokugombea ubunge ni sawa na kusema ameamua kustaafu Uwaziri Mkuu, kwa sababu hauwezi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kama hautokani na ubunge wa kuchaguliwa jimboni. Hii ndiyo kusema kuwa Majaliwa amestaafu rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.

Amestaafu akiwa bado ana nguvu, ana nishati na uwezo wa kuendelea kuwa mtumishi mwandamizi wa serikali. Waziri Mkuu mwenye historia ya utumishi uliojaa uadilifu na kujitolea. Ni kiongozi wa kipekee anayestaafu mapema kuliko waliomtangulia, lakini akiacha alama ya kudumu. Kassim Majaliwa ni kielelezo cha uongozi wa kweli – unaotanguliza maadili, unyenyekevu, na maslahi ya taifa kuliko jina binafsi.
‎Tanzania itamkumbuka daima kama mtumishi mwadilifu, ambaye alitumikia taifa kwa moyo wote – kwa utulivu, busara, na heshima ya juu. Hongera sana Majaliwa, tumeuona na kuuonja utamu wa utumishi wako kama Waziri Mkuu wa nchi hii.
Hakika wewe ni shujaa unayestahili kukumbukwa, ni mwamba unayehitaji kuegemewa.
‎Unaanza maisha mapya ya ustaafu ukiwa na nguvu na maarifa mapana kiasi cha kuwa mshauri bora kwa wa watakaoendelea madarakani.
‎Itoshe kusema umafanya kila ulichotakiwa kufanya katika nchi, Taifa limafaidika katika kila idara ulipokwepo
‎Sasa ni muda wa wajukuu kufurahia wema wa Babu Kasim Majaliwa
‎Kila la heri, Fahari ya Kusini.
‎Kila la heri, Mpiganaji.

Na. Mwandishi wetu - Kilimanjaro


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa siku 100 kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Wafanyakazi wa Umma (PSSSF) Ndg. Abdul-Razaq Badru kuhakikisha Awamu ya Pili ujenzi wa kiwanda cha kuchakata Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro unakamilika na kuanza kufanya kazi ifikapo Julai 2024.
Agizo hilo amelitoa leo Februari 22, 2024 alipo fanya ziara ya kukagua ujenzi katika kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro International Leather Industries Ltd (KLICL) ikiwa ni sehemu ya kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na serikali kupitia Ofisi hiyo.
Mhandisi Luhemeja amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutaongeza thamani ya zao la ngozi ghafi, kufungua fursa za soko la uhakika la Ngozi kutoka kwa wafugaji, kuongeza ajira kwa vijana na mapato ya fedha za ndani na za kigeni.


Aidha, amefurahishwa na ubora wa bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo na kutoa wito kwa watanzania kuwa na tamaduni za kuthamini bidhaa zinazo zalishwa nchini.


Awali akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Ndg. Abdul-Razaq Badru amesema amepokea maagizo hayo ya Katibu Mkuu Mhandisi Luhemeja na kuahidi kuwa PSSSF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi kama ilivyo elekezwa ili watanzania waanze kunufaika na mradi huo.


Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Mhandisi Saiba Edward amesema mradi huo pamoja na mambo mengine, utaongeza kipato kwa wakazi wa Kilimanjaro na Mikoa jirani kupitia fursa za uzabuni, uwakala na usambazaji wa bidhaa.


Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Magereza Frank Mwakijungu amebainisha kuwa Magereza ni mbia wa utekelezaji wa Mradi huo hivyo watasimamia ujenzi wa kiwanda hicho ili kikamilike kwa wakati kwa manufaa ya watanzania.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemaja (kushoto) akikagua bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro International Leather Industries Ltd (KLICL) leo Februari 22, 2024 ikiwa ni mwendelezo wa kukagua miradi inayotekelezwa na serikali kupitia Ofisi hiyo.




















Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) ya Dodoma katika eneo la Mkonze jijini Dodoma
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) ya Dodoma katika eneo la Mkonze jijini Dodoma,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) iliyopo eneo la Mkonze jijini Dodoma,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC, Profesa John Kondoro (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika eneo la Mkonze jijini Dodoma
Baadhi ya mafundi waoshiriki katika ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika eneo la Mkonzi jijini Dodoma wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao baada ya kukagua ujenzi huo,
Muonekano wa Jengo la Makao Mkuu ya Shirika la Reli Tanzania TRC jijini Dodoma ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake, Novemba 24, 2022. Mheshimiwa Majaliwa pia alikagua ujenzi wa Setesheni Kuu ya Reli ya Kisasa SGR katika eneo hilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 06 Septemba, 2022.

PICHA NA IKULU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akifuatilia Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) unaoendelea katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres mjini Tunis,Tunisia, Agosti 27, 2022. Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Tunisia Kais Saied alipowasili katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres kuhudhuria Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8), mjini Tunis,Tunisia, Agosti 27, 2022. Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na Rais wa Tunisia Kais Saied alipowasili katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres kuhudhuria Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8), mjini Tunis,Tunisia, Agosti 27, 2022. Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
---
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemshukuru Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida kwa misaada ambayo nchi yake inaipatia Tanzania ili kuleta unafuu kwenye maisha ya wananchi wake.

“Tanzania tunaishukuru sana Serikali ya Japan kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwakwamua wananchi wake kiuchumi na kuwezesha ujenzi wa miundombinu hadi vijijini,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Agosti 27, 2022) wakati akizungumza naye kwa njia ya mitandao kwenye ukumbi wa Palais des Congres, jijini Tunis, Tunisia. Mheshimiwa Kishida ameshindwa kuhudhuria mkutano kwa sababu ya maambukizi ya UVIKO 19.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye anamwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa TICAD ulioanza leo, alimweleza Waziri Mkuu huyo kwamba Tanzania bado inaomboleza na wananchi wa Japan kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Shinzo Abe na akatumia fursa hiyo kuwapa pole.

Akigusia miradi ambayo Serikali imeisaidia Tanzania, Waziri Mkuu amesema: “Iko miradi mingi ambayo imetekelezwa na Japan kupitia taasisi ya JICA, wako wawekezaji wanafanya biashara nasi na pia yako makampuni ambayo yamejitoa kusaidia sekta muhimu.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuiomba Japan ikamilishe ahadi yake ya kutekelza miradi waliyoiahidi kwenye mkutano wa TICAD 7 ambayo inahusu ujenzi wa barabara ya Arusha mpaka Holili mkoani Kilimanjaro, mradi wa maji wa Zanzibar, ujenzi wa bandari ya Kigoma na bandari ya uvuvi Zanzibar.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan, amemtumia salamu Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote na akataka uhusiano wa nchi hizo mbili kupitia taasisi yao ya JICA.

Mapema, akitoa tamko kwa niaba ya Rais Samia kwenye mkutano huo wa wakuu wa nchi na Serikali, Waziri Mkuu alisema bara la Afrika linakabiliwa na matatizo ya kiuchumi ambayo kwa kiasi kikubwa chimbuk lake ni UVIKO 19.

“Nimewaeleza madhara ya UVIKO 19 ambayo yanaikumba Afrika Tanzania ikiwemo, matatizo ya vita ya Ukraine na Urusi ambavyo vimesaabisha bei za bidhaa nyingi kupanda. Nimewaambia ujko umuhimu wa mataifa makubwa ya G20 kuungana na Japan ambayo ni ya tatu kwa ukubwa kiuchumi ili kuzisaidia nchi za Afrika.”

Amesema iko haja ya kuziwezesha nchi za Afrika kujitegemea ili ziweze kuwasaidia wananchi wake kupata fursa za elimu, kujenga uweza wa shughuli za kilimo, utalii ili waweze kukuza uchumi wao.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Rais Tunisia, Mhe. Kais Saied ambapo Rais wa Senegal, Mhe. Macky Sall alitoa hotuba ya ufunguzi na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Kishida Fumio akahutubia kwa njia ya mitandao kutokea Japan.

Pamoja na masuala mengine, mkutano huo wa siku unatarajiwa kukubaliana kuhusu namna ya kuiwezesha Afrika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dunia ili kuiwezesha kufikia Agenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (Agenda 2063).

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na janga la UVIKO 19, amani na usalama, mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji mgumu wa malighafi na mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazotegemewa na nchi za Afrika kama vile gesi, mafuta na pembejeo za kilimo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Bara la Afrika.