Na Mwandishi Wetu, Arusha.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameibuka kinara wa Tuzo za Kitaifa za Uhifadhi na Utalii (Serengeti Awards) baada ya kutunukiwa Tuzo Maalum ya Kiongozi Mwenye Maono (Visionary Leadership Award) kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya Maliasili na Utalii nchini.
Tuzo hiyo ilitolewa katika hafla ya kitaifa iliyofanyika leo Januari 31, 2026, katika Ukumbi wa Mount Meru Hotel jijini Arusha, ikitambua uongozi wa kimkakati wa Rais Samia katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu maarufu za Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania, pamoja na juhudi zake za kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utalii na kuimarisha uhifadhi wa maliasili.
Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyesema jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita zimeendelea kuleta matokeo chanya katika sekta ya utalii. Alieleza kuwa kuanzia Januari hadi Novemba 2025, Tanzania ilipokea watalii wa kimataifa 2,097,823, ikiwa ni ongezeko la takribani asilimia 9.02 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa sekta ya Maliasili na Utalii inachangia takribani asilimia 21 ya Pato la Taifa, ambapo asilimia 17 inatokana na utalii na asilimia 4 kutoka sekta ya misitu na nyuki, huku sekta hiyo ikitoa ajira kwa takribani Watanzania milioni tatu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, alimpongeza Rais Samia kwa uongozi wake thabiti uliowezesha kuimarika kwa uhifadhi wa maliasili pamoja na ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo barabara na viwanja vya ndege katika maeneo ya hifadhi, hatua zilizorahisisha shughuli za utalii na kuongeza mvuto wa Tanzania katika soko la kimataifa.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na shabiki wa klabu ya Manchester City ya Uingereza, Braydon Bent, ambaye alieleza kuvutiwa na uzuri wa vivutio vya utalii vya Tanzania, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Ngorongoro, pamoja na ukarimu wa Watanzania, akisema safari yake nchini itaendelea kuwa kumbukumbu isiyosahaulika katika maisha yake.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza utalii, kulinda mazingira, na kuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka hifadhi wananufaika kiuchumi. Aidha, alihimiza matumizi ya teknolojia na ubunifu ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa la utalii.
Alimalizia kwa kuwakumbusha Watanzania kuwa amani ni tunu kuu ya Taifa, na kuwasisitiza kushirikiana kulinda rasilimali zilizopo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.







Toa Maoni Yako:
0 comments: