Na Mwandishi Wetu, Manyara.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, ametoa maagizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Manyara kufuatilia matumizi ya fedha zilizotumika katika ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto pamoja na ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo.

Ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo, akieleza kuwa amepokea taarifa za kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha katika utekelezaji wa mradi huo. Waziri Mkuu alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, kwa kufuatilia suala hilo na kufanikisha kurejeshwa kwa fedha zilizobainika kupotea, huku akisisitiza kuwa wahusika wote wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Akizungumza katika ziara hiyo, Sendiga alisema kuwa tangu kuanza kwa Awamu ya Sita, mkoa wa Manyara umepokea zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, akimshukuru Waziri Mkuu kwa kuanza ziara yake mkoani humo na kuendelea kusikiliza changamoto za wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Faraja Ngerageza, alisema mradi huo ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kuanza kutumika mwezi Machi mwaka huu.

Baadhi ya wananchi wa Kiteto walimshukuru Waziri Mkuu kwa kutembelea eneo hilo, kusikiliza kero zao na kuahidi kuzitatua, wakieleza kuwa ziara hiyo imeongeza matumaini ya kuboreshwa kwa huduma za maendeleo katika wilaya hiyo.

Ziara ya Waziri Mkuu inaendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara, ambapo kwa sasa yupo wilayani Simanjiro akizindua miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: