Articles by "MAISHA NA MAHUSIANO"
Showing posts with label MAISHA NA MAHUSIANO. Show all posts
Kulikuwa na kijiji kimoja kilichoishi watu wema na wabaya kwa pamoja. Kijiji kilibarikiwa na mto ulioleta uhai kwa kila kiumbe. Ng’ombe walikunywa maji yale na kutoa maziwa matamu, lakini vilevile, nyoka walikunywa maji hayo hayo na kutengeneza sumu kali.
(Maji yaleyale anayokunywa ng’ombe kutengeneza maziwa, ndiyo hayo hayo anayokunywa nyoka kutengenezea sumu yake.)

Katika kijiji hicho, aliishi mzee mmoja mwenye mbwa aliyekuwa mwaminifu. Lakini siku moja, mbwa yule akaanza kumbwekea bwana wake kila alipomkaribia. Mzee akagundua kuwa jirani yake alikuwa amemzoesha kumpa mifupa kwa siri.
(Mbwa wako akianza kukubwekea, tambua kuna mtu mwingine anamlisha.)

Siku moja, mzee huyo aliona panya akimcheka paka wake shupavu. Alishangaa, lakini hakujua kuwa panya alikuwa amejificha karibu na shimo lake la kutorokea.
(Ukiona panya anamcheka paka, ujue yupo karibu na shimo.)

Baadaye, mbweha alifika nyumbani kwake kuomba msamaha baada ya kuiba vifaranga wawili. Kwa moyo wa huruma, mzee akamsamehe. Lakini haikupita muda, mbweha huyo akarudi tena — safari hii akaiba mbuzi wake mzima.
(Ukimsamehe mbwea kwa kukuchukulia vifaranga wako, kuna siku atakuibia mbuzi wako.)

Mzee alijaribu kumshawishi nyani wake wa shambani kwamba asali ni tamu kuliko ndizi, lakini nyani akacheka tu na kusema, “Hata tamu ya dunia, siwezi kuiacha ndizi yangu.”
(Huwezi kumshawishi ngedere asali ni tamu kuliko ndizi.)

Siku moja mzee alipokuwa akipita shambani, alikuta mzoga wa mbuzi wake kati ya mimea ya viazi. Wengi walidhani labda alikufa kwa njaa, lakini macho ya mzee yaliona zaidi — alijua kuwa kilichomuua kilikuwa sumu kutoka kwa nyoka aliyekunywa maji yale yale ya mtoni.
(Ukikuta mzoga wa mbuzi kwenye shamba la viazi, unapaswa kujua kilichomuua si njaa.)

Baadaye, tumbili walianza kumpigia makofi kila alipopita, wakimsifia kwa maneno matamu. Lakini ndani ya usiku ule ule, walimuangushia ndizi zake zote ardhini.
(Tumbili akikupigia makofi, ujue anakaribia kukuangushia ndizi zako.)

Mwishowe, mzee akaenda kumshauri kijana wa kijiji aliyekuwa anajulikana kwa ukaidi. Alimwambia, “Usisubiri hadi uharibifu ukufike ndipo usikie.” Lakini kijana hakusikia. Ilibidi apitie mateso ndipo ajifunze.
(Kenge huwa hasikii mpaka atokwe na damu masikioni.)

Ndipo mzee akakaa chini ya mti wa mwembe, akatazama mto ule ule, akatabasamu kwa uchungu na kusema:

“Maisha ni kama maji yale ya mtoni — yanamlisha ng’ombe na nyoka kwa pamoja. Uamuzi ni wako kama utakua wa kutoa maziwa au sumu.”
Baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, taifa letu limepata majeraha kutokana na matendo ya baadhi ya vijana waliotumika vibaya kufanya fujo na vurugu. Wengi wamepoteza maisha, wengine wamejeruhiwa, na ndoto nyingi zimezimika — yote kwa sababu ya kuchochewa na watu wenye maslahi binafsi.

Kijana, usikubali kuwa chombo cha uharibifu.
Usikubali kutumiwa kuvunja amani kwa ahadi za muda mfupi au hisia za hasira.
Tafakari kabla ya kuchukua hatua — je, unachokifanya kinajenga au kinabomoa mustakabali wako?

Acha nia ovu, jenga nia njema.
Tumia nguvu zako kwa maendeleo, elimu, ubunifu, na kulinda amani ya nchi yako.
Kumbuka, taifa lenye amani linatoa nafasi kwa ndoto zako kukua.

🇹🇿 Tanzania inakuhitaji ukiwa imara, mwenye hekima, na mwenye upendo.
#KijanaWaAmani #UsikubaliKutumika #AmaniKwanza #TanzaniaYetu #FikraSahihi

Kuna maumivu ambayo hayawezi kuelezeka kwa maneno — maumivu ya kumpenda mtu kwa dhati, kumpigania, kumuinua, kumsamehe, kumsomesha, au hata kumuuguza… halafu siku moja unaamka na kugundua amekuacha kama hukuwahi kuwepo.
Huu ni uchungu wa kimya, ule unaolia ndani ya roho, si kwa hasira, bali kwa maswali yasiyo na majibu.

Lakini ukweli ni huu: maumivu haya hayajawekwa ili yakumalize, bali yakukamilishe.

JINSI YA KUPONA BAADA YA KUUMIZWA NA MTU ULIYEMPENDA KWA DHATI

Hapa chini ni hatua 10 za kupona kiakili, kihisia, na kiroho baada ya kuumizwa na mtu uliyetolewa roho yako kumpenda.

1. KUBALI KUUMIA — USIJIFICHE NYUMA YA NGUVU BANDIA

Usijifanye “nipo sawa” wakati moyo wako unavuja damu. Kubali kuwa umeumizwa, ukubali kwamba ulipenda kupita kiasi. Kukubali ndiyo hatua ya kwanza ya uponyaji.

Usione aibu kulia — machozi si udhaifu, ni njia ya roho kutoa sumu ya huzuni. Wacha moyo wako upate nafasi ya kuvujisha maumivu badala ya kuyabeba ndani na kuwa mzigo wa maisha.

2. USIJILAUMU KWA WEMA WAKO

Wema wako haukuwa kosa. Ulichofanya kilikuwa sahihi, ila kwa mtu asiye sahihi.

Kujitolea kwako, huruma yako, na moyo wako wa kutoa havipaswi kuwa sababu ya kujichukia. Dunia inahitaji watu kama wewe, ila safari ijayo lazima ujifunze kuweka mipaka.

Tambua: mtu aliyekuacha hakukataa wema wako, alishindwa kuuhimili.

3. TOA WAZI KWA HISIA ZAKO KWA NJIA ZENYE AFYA

Badala ya kujifungia chumbani na kulia kila siku, andika hisia zako.

Andika barua ambayo hautamtumia.

Enda baharini, mlimani, au sehemu tulivu—piga kelele, lia, toa yote.

Hiyo ni njia ya roho kujisafisha. Ukijinyima nafasi ya kutoa hisia, utajikuta unalipiza kisasi kimya, au unakuwa mtu mkavu kihisia kwa wote.

4. USIRUDISHE HESHIMA KWA MTU ALIYEITUPA

Baada ya kuumizwa, kuna jaribu la kutaka kuonyesha bado unamjali, bado uko pale. Hapana.

Ukirudisha heshima kwa mtu ambaye hakujali hisia zako, unazidisha kidonda.

Sio chuki — ni heshima binafsi. Acha roho yake iende. Usijaribu kumshawishi akuone tena. Wacha akumbuke mwenyewe alivyoondoka kwa mtu ambaye hakuwa na kosa ila moyo safi.

5. TENGA MUDA WA UKIMYA NA UPWEKE

Upweke ni tiba ya nafsi. Wengi wanakimbilia uhusiano mwingine au marafiki wapya haraka ili kusahau, lakini wanajikuta wanaumizwa tena.

Tulia. Tembea peke yako. Tafakari.

Sauti ya ndani yako haiwezi kuzungumza kwenye kelele.

Ukimya utakufundisha kitu ambacho mapenzi hayakuweza—kuwa rafiki wa nafsi yako.

6. JIFUNZE SOMO BADALA YA KUJENGA UKUTA

Kila maumivu yana fundisho. Usiyatumie kujenga chuki au ukuta wa kutomwamini mtu tena.

Jiulize: “Nilijifunza nini kuhusu moyo wa binadamu? Nilijifunza nini kuhusu mipaka? Nilijifunza nini kuhusu mimi?”

Maumivu yasipoleta hekima, yanakuwa mateso bure. Wacha yakukue.

7. JENGA UPYA UTAMANI WA MAISHA BILA YEYE

Wakati mtu anaondoka, si dunia yote imeondoka.

Rudisha furaha ndogo ulizokuwa nazo: soma kitabu, fanya mazoezi, soma neno la Mungu, tembelea watu wanaokujali kwa dhati.

Polepole utaona, maisha yana rangi nyingine hata bila mtu huyo.

Usiishi kwa kumbukumbu ya jana. Kila siku mpya ni nafasi ya kuandika ukurasa mpya wa furaha yako.

8. WACHA MUNGU AWE DAKTARI WA MOYO WAKO

Kuna maumivu ambayo hakuna maneno, hakuna marafiki, hata pesa haiwezi kutuliza—lakini Mungu anaweza.

Mpe nafasi aingie katika nafasi iliyoachwa wazi.

Omba si kwa hasira, bali kwa upole: “Bwana, nisaidie nione maana ya hili.”

Mara nyingi, Mungu anaondoa mtu fulani sio kwa sababu hakupendi, bali kwa sababu hawezi kuwa sehemu ya hatima yako.

9. JIFUNZE KUPENDA KWA HEKIMA, SIO HURUMA

Wakati mwingine, tuliumizwa si kwa sababu tulipenda vibaya, bali tulichanganya huruma na upendo.

Safari ijayo, usipende kwa sababu unahisi huruma au unataka kuokoa mtu. Penda kwa uwiano—kwa moyo na akili.

Weka mipaka ya hisia zako; upendo usio na mipaka huvuta watu wasio na mipaka.

10. TENGENEZA MAONO MPYA YA MAISHA YAKO

Ukipoteza mtu, usione ni mwisho. Ni nafasi ya kujenga toleo jipya la wewe.

Andika malengo mapya. Fufua ndoto ulizoacha kwa sababu yake.

Usiruhusu maumivu yakufanye ushindwe kuamini tena katika upendo.

Mtu sahihi hatatisha uhuru wako, hatakufanya ujisikie mdogo, wala hatakupenda kwa sababu ya msaada wako—atakupenda kwa sababu ya utu wako.

MANENO YA KUHITIMISHA

Usijilaumu kwa kuwa mtu mzuri.

Wema wako si upumbavu, ni zawadi ambayo dunia inahitaji.

Lakini sasa umejifunza kitu muhimu — kwamba upendo haumaanishi kujitolea hadi kujiua ndani.

Upendo wa kweli ni ule unaoweza kutoa na bado ukaendelea kujiheshimu.

Na siku moja, utamuangalia nyuma huyo aliyekuacha, moyo wako ukiwa umetulia, halafu utasema kwa utulivu:

“Asante kwa kuniumiza, maana maumivu yako yamenifundisha kujipenda.”

Katika maisha jifunza jambo kubwa:

Ukidhalilishwa, usighadhibike.

Ukitengenezewa fitna, usichukie.

Ukiwekewa ukuta, usijaribu kuubomoa kupita kwa nguvu.

Ukitengenezewa majungu, umia lakini jikaze.

Mungu ana njia zake za kukufariji, na pia ana namna zake za kuwaadhibu wale wanaokuumiza. Subira ni silaha kubwa.

Weka moyoni mwako kumbukumbu za watu hawa katika maisha yako:

Aliyekuinua wakati ulikuwa chini.

Aliyekuhifadhi wakati huna pa kujihifadhi.

Aliyekuacha ukiwa kwenye giza la matatizo.

Aliyekupa heshima wakati ukidharauliwa.

Aliyekupa thamani uliponyimwa thamani.

Aliyekusogelea wakati wengine walikukimbia.

Unapopitia maumivu, usijiumize zaidi kwa kumfikiria sana yule aliyekuletea machungu. Dawa ya maumivu ni kukubali hali, kusimama imara, na kusonga mbele. Usijiumize kwa sababu kufanya hivyo ni kutimiza malengo ya yule aliyekutesa.

Kauli ya, “Sikuamini kama fulani anaweza kunifanyia hivi,” imetoka kwa wengi walioumizwa na watu wao wa karibu. Ili ujilinde, nenda kwenye kioo na muamini unayemuona humo – huyo ndiye usalama wako wa kweli. Wengine wape furaha, lakini usiwape imani yako yote.

Kumbuka: Ukiishi kwa kuumiza wengine, Mungu hukuletea watu wa kukuumiza wewe na kizazi chako. Lakini ukiishi kwa kuwafariji na kuwapa furaha wengine, Mungu hukuletea watu wa kukuinua na kukufurahisha. Wema husafiri mbali, lakini uovu husafiri mbali zaidi.

Muda hauwezi kubadilisha mtu, bali hufichua sura yake halisi. Kadiri unavyosubiri, ndivyo muda utakavyokuletea majibu ya kweli kuhusu watu wanaokuzunguka. Kuwa mtulivu, muda ndio shahidi wa haki.

Maisha haya tumeazimwa kila kitu: uhai, afya, uzuri, ubaya, utajiri na hata umasikini. Siku Mungu akiamua, huchukua tu alichotuazima bila kutuomba ruhusa wala kutuandaa. Kwa sababu hiyo, tuishi maisha kwa nidhamu, kwa unyenyekevu na heshima – maana cha kuazimwa si cha kutamba nacho.

Dondoo 15 za matumizi sahihi ya muda ambazo zinaweza kukusaidia kazini na hata kwenye maisha ya kila siku:

1. Panga ratiba ya kila siku – andika majukumu yako kabla ya kuanza siku.

2. Weka vipaumbele – fanya mambo ya muhimu kwanza.

3. Tumia kalenda au daftari la kumbukumbu – kusaidia kukumbuka tarehe na mikutano.

4. Epuka kazi nyingi kwa wakati mmoja (multitasking) – maliza moja kabla ya kuanza nyingine.

5. Weka muda maalum wa mapumziko – kupunguza uchovu na kuongeza ufanisi.

6. Tumia teknolojia kwa busara – alarms, reminders, na apps za kupanga muda.

7. Punguza usumbufu – kama simu na mitandao ya kijamii unapofanya kazi.

8. Gawa majukumu (delegation) – usijaribu kufanya kila kitu mwenyewe.

9. Weka muda wa dharura (buffer time) – kati ya majukumu ili kuepuka msongo.

10. Anza mapema – kufanya kazi kubwa kabla ya muda haujaenda sana.

11. Jifunze kusema ‘hapana’ – kwa kazi au shughuli zisizo na umuhimu mkubwa.

12. Weka malengo ya muda mfupi na mrefu – ili kujua unakoelekea.

13. Kagua maendeleo yako – angalia kama unatumia muda vizuri.

14. Tambua saa zako za ufanisi zaidi – fanya kazi ngumu wakati akili ikiwa timamu.

15. Hifadhi muda kwa ajili ya familia na afya yako – usitumie muda wote kazini pekee.
●Wivu wa mapenzi wadaiwa kuwa chanzo cha tukio la kusikitisha

Na Regina Ndumbaro, Songea-Ruvuma.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikilia mwanamke mmoja, Wende Luchagula, kwa tuhuma za mauaji ya kikatili ya watoto watatu, akiwemo Lugola Lutelemula mwenye umri wa miaka 6 pamoja na mapacha wa miezi minane, Kulwa na Doto Lutelemula – wote wakazi wa kijiji cha Milonji, kata ya Lusewa, Wilaya ya Namtumbo.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea mnamo tarehe 12 Julai 2025, na linasemekana kuchochewa na wivu wa mapenzi kati ya wake wawili wa mume mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 25, 2025 katika Manispaa ya Songea, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Mkoa wa Ruvuma (SACP), Marco G. Chilya (Pichani) amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio hilo lilitekelezwa majira ya saa nane mchana na tayari mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.

“Tukio hili limehuzunisha na kushtua taifa zima, hasa ikizingatiwa kuwa waliouawa ni watoto wadogo wasio na hatia. Jeshi la Polisi limechukua hatua stahiki kuhakikisha mtuhumiwa anafikishwa kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo,” alisema Kamanda Chilya.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limetoa rai kwa wanandoa wanaoishi katika ndoa za wake wengi kuwa wavumilivu, kujiepusha na chuki au wivu wa kupindukia, na kutafuta suluhu kwa njia ya amani kupitia viongozi wa dini, wazee wa familia au viongozi wa kijamii.

Pia, jamii imetakiwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema pale panapojitokeza viashiria vya migogoro au uvunjifu wa amani, ili kuzuia madhara makubwa kama haya kutokea tena.

Jeshi hilo limeahidi kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha mazingira salama na yenye ustawi kwa wote, hasa watoto ambao ni kundi lenye uhitaji mkubwa wa ulinzi na upendo kutoka kwa jamii nzima.
Wanawake (kama ilivyo kwa wanaume pia) wanaweza kutumia mbinu mbalimbali kuficha usaliti wa kimapenzi. Hapa chini ni baadhi ya njia ambazo wanawake hutumia kuficha usaliti, kulingana na uzoefu wa wataalam wa mahusiano, saikolojia ya tabia na simulizi halisi za maisha:

●1. Kubadilisha Ratiba Ghafla lakini kwa “Sababu Zenye Mantiki”

Wanawake wengi huongeza muda kazini au huanza “mashughuli mapya” kama:

Kujitolea kusaidia kwenye taasisi zisizo za kiserikali

Kujiunga na vikundi vya mazoezi au ibada

Kufanya “shughuli za kikazi” weekend Sababu hizi zinaonekana halali, lakini huweza kutumika kuficha miadi ya faragha.

●2. Kuongeza Umakini Kwa Mpenzi Wake Halali (Ili Kuficha Hatia)

Baadhi ya wanawake wanaosaliti huanza kuonyesha:

Mapenzi ya ghafla yasiyo na sababu

Zawadi zisizotarajiwa

Kuwa wapole kuliko kawaida Hili hufanyika ili kumshawishi mwanaume kwamba hakuna tatizo lolote, huku wakificha hatia ya usaliti.

●3. Kulinda Simu Kupita Kiasi

Kuweka password ngumu

Kuondoka na simu hata chooni

Kupokea simu wakiwa na wasiwasi au kwenda mbali kupokea

Kubadilisha majina ya wapenzi wa pembeni kuwa majina ya jinsia moja au "Boss", "Client", "Auntie"

●4. Kuanzisha Migogoro Isiyo na Sababu

Anakuchokonoa bila sababu, au anakulaumu kwa kila kitu

Anaanzisha ugomvi ili awe na “sababu” ya kutokulala nyumbani au kutopatikana

Anaacha kuonyesha upendo na mguso wa kimapenzi kama njia ya “kukwepa lawama”

●5. Kujifanya Ameokoka au Amebadilika Dini Sana

Anaanza kujitenga kimapenzi akitumia kisingizio cha “safari ya kiroho”

Anatumia dini kuficha ukweli kwamba hayuko sawa kihisia, wakati sababu halisi ni usaliti

●6. Kulalamika Sana Kwamba “Anafuatiliwa”

Anakushambulia kuwa unamchunguza sana ilhali wewe hujauliza chochote

Anaanza kutumia maneno kama “huna imani na mimi”, “mbona unanipima?”, “mapenzi si kifungo” Hili ni janja ya kujikinga asije akaulizwa maswali kuhusu mienendo yake isiyoeleweka.

●7. Kudai Hana Hamu ya Tendo la Ndoa Kwa Muda Mrefu

Anaweza kudai yuko “stressed”, ana uchovu wa kazini, au ana matatizo ya kiafya

Lakini ukweli ni kwamba mahitaji yake ya kimapenzi yanatimizwa kwingine

●8. Kuweka Siri Za Safari au Mikutano

Hataki uende naye kazini au kwenye sherehe fulani

Anasema amesafiri kikazi lakini hawezi kupiga simu au kutuma picha

Safari nyingi za ghafla zisizopangwa

●9. Kudai Rafiki wa Kike (ambaye si halisi)

Hucheza karata ya rafiki wa kike aliyempenda sana: “Niko na Asha”, kumbe ni mwanaume

Anaweka picha feki au hutaja majina ya ndugu wa jinsia moja kama kisingizio

 ●10. Kuvuruga Mawasiliano na Familia Yako

Anaanza kutopenda marafiki na ndugu zako

Anakata mawasiliano na watu waliokuwa wa karibu Sababu: watu hao wanaweza kuona au kuhisi tabia yake isiyo ya kawaida

Hitimisho:

Sio wanawake wote hufanya haya. Hizi ni tabia za mtu binafsi, sio jinsia nzima. Pia, wanaume pia hutumia mbinu nyingi sana kuficha usaliti. Njia bora ya kushughulikia mashaka ya usaliti ni mawasiliano ya wazi, uchunguzi wa tabia (si tuhisia), na msaada wa kitaalamu wa mahusiano pale panapohitajika.
Kwanza kabisa ni muhimu kuelewa kwamba mahusiano ya kimapenzi ni safari ya pamoja ambayo inahitaji mawasiliano, uvumilivu na kujitolea.

Kumridhisha mke wako kimapenzi sio tu juu ya tendo la ndoa bali ni kuhusu kuunda uhusiano mzuri na wenye afya. Kuna hatua kadhaa za kuzingatia

1. #MAWASILIANO
Ongea na mke wako kuhusu hisia zake, anachopenda na kile ambacho hakipendi. Mawasiliano ya wazi na ya heshima ni msingi wa mahusiano mazuri.

2. #UELEWA WA MWILI
Jifunze kuhusu mwili wa mke wako na anavyopenda kuguswa. Hii inaweza kusaidia kugundua maeneo yanayompa raha zaidi.

3. #USIHARAKISHE
Chukua muda wako na usiharakishe tendo la ndoa. Fanya maandalizi ya kimapenzi kama vile mabusu, kukumbatiana na mambo mengine ya upendo. Zingatia pia mambo madogo madogo ambayo yanaweza kumfurahisha mke wako nje ya tendo la ndoa kama vile kumletea maua au zawadi yoyote, kumwandikia ujumbe wa mapenzi au hata kumwandalia mtoko wa jioni. Hayo yatamfanya ajione unampenda,unamjali na unamthamini.

4. #UVUMILIVU NA UPENDO
Uvumilivu ni muhimu. Kila mtu ana mapungufu yake,pata muda wa kumjua mke wako vizuri. Hakikisha unamwonyesha upendo na kujali.

5. #ELIMU NA ZIADA.
Usione aibu kutafuta elimu zaidi kuhusu mahusiano na mapenzi. Vitabu, makala na mazungumzo na wataalamu wa mahusiano vinaweza kukusaidia kuongeza uelewa wako.

KUMBUKA
Lengo ni kumfanya mke wako ajisikie salama, kuthaminiwa na kupendwa.

Hii ndiyo njia ya uhakika ya kujenga mahusiano ya kimapenzi yenye afya na furaha.

Ni mimi shangazi mtiifu.
Joyce wa Moro
Mwalimu wa MAHUSIANO, UCHUMBA NA NDOA.

0658474191