Katika maisha jifunza jambo kubwa:

Ukidhalilishwa, usighadhibike.

Ukitengenezewa fitna, usichukie.

Ukiwekewa ukuta, usijaribu kuubomoa kupita kwa nguvu.

Ukitengenezewa majungu, umia lakini jikaze.

Mungu ana njia zake za kukufariji, na pia ana namna zake za kuwaadhibu wale wanaokuumiza. Subira ni silaha kubwa.

Weka moyoni mwako kumbukumbu za watu hawa katika maisha yako:

Aliyekuinua wakati ulikuwa chini.

Aliyekuhifadhi wakati huna pa kujihifadhi.

Aliyekuacha ukiwa kwenye giza la matatizo.

Aliyekupa heshima wakati ukidharauliwa.

Aliyekupa thamani uliponyimwa thamani.

Aliyekusogelea wakati wengine walikukimbia.

Unapopitia maumivu, usijiumize zaidi kwa kumfikiria sana yule aliyekuletea machungu. Dawa ya maumivu ni kukubali hali, kusimama imara, na kusonga mbele. Usijiumize kwa sababu kufanya hivyo ni kutimiza malengo ya yule aliyekutesa.

Kauli ya, “Sikuamini kama fulani anaweza kunifanyia hivi,” imetoka kwa wengi walioumizwa na watu wao wa karibu. Ili ujilinde, nenda kwenye kioo na muamini unayemuona humo – huyo ndiye usalama wako wa kweli. Wengine wape furaha, lakini usiwape imani yako yote.

Kumbuka: Ukiishi kwa kuumiza wengine, Mungu hukuletea watu wa kukuumiza wewe na kizazi chako. Lakini ukiishi kwa kuwafariji na kuwapa furaha wengine, Mungu hukuletea watu wa kukuinua na kukufurahisha. Wema husafiri mbali, lakini uovu husafiri mbali zaidi.

Muda hauwezi kubadilisha mtu, bali hufichua sura yake halisi. Kadiri unavyosubiri, ndivyo muda utakavyokuletea majibu ya kweli kuhusu watu wanaokuzunguka. Kuwa mtulivu, muda ndio shahidi wa haki.

Maisha haya tumeazimwa kila kitu: uhai, afya, uzuri, ubaya, utajiri na hata umasikini. Siku Mungu akiamua, huchukua tu alichotuazima bila kutuomba ruhusa wala kutuandaa. Kwa sababu hiyo, tuishi maisha kwa nidhamu, kwa unyenyekevu na heshima – maana cha kuazimwa si cha kutamba nacho.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: