Dar es Salaam, Oktoba 2, 2025: Baada ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi kuhusu huduma duni za usafiri wa Mwendokasi, hususan katika njia ya Kimara, Serikali hatimaye imeongeza idadi ya mabasi mapya ili kurahisisha huduma kwa abiria.

Abiria katika kituo cha Kivukoni na maeneo mengine ya Kimara wameeleza kufurahishwa kwao na uamuzi huo, wakisema umeonesha Serikali imesikia kilio cha wananchi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya ucheleweshaji na msongamano wa abiria.

Maoni ya Abiria

Alex Michael, ambaye amekuwa mtumiaji wa muda mrefu wa mabasi ya Mwendokasi, alisema kabla ya mabasi mapya kuletwa walilazimika kukaa muda mrefu vituoni bila uhakika wa usafiri, jambo lililowalazimu kutumia usafiri mbadala wa bodaboda kwa gharama kubwa.

“Baada ya kuanza kwa mradi huu karibu miaka 10, mwanzo huduma ilikuwa nzuri na inavutia sana, lakini kadri siku zilivyopita mabasi mengi yakawa yanaharibika na huduma ikawa mbovu. Tunaishukuru Serikali kwa hatua hii ya kuleta mabasi mapya,” alisema Michael.

Kwa upande wake, Amina Ramadhani, mkazi wa Kimara Baruti, alihimiza Serikali kuhakikisha mabasi hayo mapya yanabaki kudumu kwenye njia ya Kimara na sio ya muda mfupi pekee.

“Tunataka mabasi haya yaendelee kutoa huduma hapa Kimara kwa muda mrefu, si kama inavyodaiwa kuwa yameletwa kwa muda tu kabla ya kupelekwa njia ya Mbagala–Gerezani,” alisema Amina.

Historia ya Malalamiko
Wananchi wa Kimara wamekuwa wakilalamikia upungufu wa mabasi ya Mwendokasi, hali iliyosababisha foleni kubwa vituoni na abiria kulazimika kutafuta usafiri mbadala.

Ujio wa mabasi mapya unatarajiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa adha hiyo na kuongeza ufanisi wa huduma katika mradi wa usafiri wa Mwendokasi jijini Dar es Salaam.



Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: