●Wivu wa mapenzi wadaiwa kuwa chanzo cha tukio la kusikitisha

Na Regina Ndumbaro, Songea-Ruvuma.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikilia mwanamke mmoja, Wende Luchagula, kwa tuhuma za mauaji ya kikatili ya watoto watatu, akiwemo Lugola Lutelemula mwenye umri wa miaka 6 pamoja na mapacha wa miezi minane, Kulwa na Doto Lutelemula – wote wakazi wa kijiji cha Milonji, kata ya Lusewa, Wilaya ya Namtumbo.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea mnamo tarehe 12 Julai 2025, na linasemekana kuchochewa na wivu wa mapenzi kati ya wake wawili wa mume mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 25, 2025 katika Manispaa ya Songea, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Mkoa wa Ruvuma (SACP), Marco G. Chilya (Pichani) amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio hilo lilitekelezwa majira ya saa nane mchana na tayari mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.

“Tukio hili limehuzunisha na kushtua taifa zima, hasa ikizingatiwa kuwa waliouawa ni watoto wadogo wasio na hatia. Jeshi la Polisi limechukua hatua stahiki kuhakikisha mtuhumiwa anafikishwa kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo,” alisema Kamanda Chilya.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limetoa rai kwa wanandoa wanaoishi katika ndoa za wake wengi kuwa wavumilivu, kujiepusha na chuki au wivu wa kupindukia, na kutafuta suluhu kwa njia ya amani kupitia viongozi wa dini, wazee wa familia au viongozi wa kijamii.

Pia, jamii imetakiwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema pale panapojitokeza viashiria vya migogoro au uvunjifu wa amani, ili kuzuia madhara makubwa kama haya kutokea tena.

Jeshi hilo limeahidi kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha mazingira salama na yenye ustawi kwa wote, hasa watoto ambao ni kundi lenye uhitaji mkubwa wa ulinzi na upendo kutoka kwa jamii nzima.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: