Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza rasmi kuwa Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utafanyika Jumatano ya tarehe 29 Oktoba 2025, ambapo wananchi watachagua viongozi katika ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani.
Akizungumza leo Julai 26, 2025 katika hafla ya uzinduzi wa ratiba ya uchaguzi iliyofanyika jijini Dodoma, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Jacobs Mwambegele, amesema maandalizi ya uchaguzi huo yameanza rasmi huku akizihimiza taasisi, vyama vya siasa na wananchi kuzingatia taratibu zilizowekwa.
“Tume imeweka ratiba ya uchaguzi kwa uwazi na kwa kuzingatia Katiba na Sheria ya Taifa. Tunawahimiza Watanzania wote kushiriki kikamilifu huku tukidumisha amani,” alisema Jaji Mwambegele.
RATIBA MUHIMU YA UCHAGUZI:
-
Utoaji wa Fomu za Uteuzi kwa Wagombea Urais na Makamu wa Rais: Agosti 9 hadi 27, 2025
-
Siku ya Uteuzi wa Wagombea (Rais, Makamu wa Rais, Wabunge na Madiwani): Agosti 27, 2025
-
Kampeni Tanzania Bara: Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025
-
Kampeni Zanzibar: Agosti 28 hadi Oktoba 27, 2025
-
Siku ya Upigaji Kura Kitaifa: Oktoba 29, 2025
.jpg)
Jaji Mwambegele ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Katiba, kila mpiga kura atakuwa na haki ya kupiga kura moja kwa kila nafasi—yaani Rais, Mbunge na Diwani—na kuwa Tume itahakikisha mazingira ya uchaguzi yanazingatia uhuru, haki, usawa na uwazi.
VYAMA 18 VYATHIBITISHA KUSHIRIKI
Katika uchaguzi huo, vyama 18 kati ya 19 vyenye usajili kamili vimethibitisha ushiriki wao baada ya kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi mnamo Aprili 12, 2025. Vyama hivyo ni pamoja na CCM, ACT-Wazalendo, CUF, ADC, CHAUMMA, TLP, NCCR-Mageuzi, CCK, DP, MAKINI, SAU, UMD, AAFP, ADA-TADEA, NLD, UPDP, UDP na NRA.
CHADEMA YAJIONDOA
Hata hivyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimejitangaza kutoshiriki uchaguzi huo, kikieleza kuwa mazingira yaliyopo hayatoi nafasi kwa uchaguzi huru na wa haki. Hali hiyo imeibua maoni mseto kutoka kwa wachambuzi wa siasa na wanaharakati wa demokrasia.
INEC YAHAKIKISHA USHIRIKI WA WOTE
INEC imewataka wadau wote wa uchaguzi wakiwemo wapiga kura, vyombo vya habari, vyama vya siasa na mashirika ya kiraia kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi ili uchaguzi huo uwe wa amani na mafanikio kwa taifa zima.
“Uchaguzi ni mchakato wa kidemokrasia wa kujenga taifa. Ushiriki wa kila raia ni muhimu. Tutahakikisha kila hatua inaendeshwa kwa uwazi,” alisisitiza Jaji Mwambegele.
Uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kuwa wa kwanza kufanyika chini ya usimamizi wa INEC tangu kuanzishwa kwake kama Tume Huru, na unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kati ya vyama vya siasa mbalimbali.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments: