Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikagua eneo la maafa ya ajali ya kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Novemba, 2024.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua eneo la maafa ya ajali ya kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Novemba, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwajulia hali na kuwapa pole majeruhi wa ajali ya kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo ambao wamelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Ilala Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Novemba, 2024.
Na Mwandishi Wetu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya ziara katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, leo Novemba 20, 2024, mara baada ya kurejea kutoka Brazil. Ziara hiyo ililenga kukagua shughuli za uokoaji kufuatia ajali ya kuporomoka kwa jengo lililosababisha maafa makubwa.
Akizungumza na wananchi baada ya ukaguzi, Rais Samia alithibitisha kuwa watu 20 wamepoteza maisha kutokana na ajali hiyo.
“Jitihada kubwa katika tukio hili zililenga kuwaokoa wenzetu waliokuwa wamekwama ndani ya jengo hilo wakiwa hai, lakini jitihada hizi haziondoshi kudra ya Mungu. Pamoja na juhudi zilizofanywa, tumepoteza wenzetu, na hadi sasa idadi yao ni 20,” alisema Rais Samia.
Aidha, alieleza kuwa miili ya marehemu hao tayari imeshazikwa kwa ushirikiano wa familia na serikali.
Rais Samia alibainisha kuwa ajali hiyo ni pigo kubwa kwa taifa, kwa kupoteza nguvu kazi muhimu, na kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.
Kwa lengo la kuzuia matukio kama haya siku zijazo, Rais Samia alisema akiwa nchini Brazil alimwagiza Waziri Mkuu kuunda tume ya watu 20 ili kufanya ukaguzi wa majengo yote katika eneo la Kariakoo.
“Naambiwa tume hiyo tayari imeundwa. Baada ya kukamilisha kazi yao, tutazingatia mapendekezo yao. Kama wataelekeza kwamba majengo yaliyo chini ya kiwango yabomolewe, hatutasita kuchukua hatua hiyo,” alisisitiza Rais Samia.
Mbali na vifo vilivyoripotiwa, idadi ya majeruhi wa tukio hilo bado inaendelea kufanyiwa tathmini. Timu za uokoaji, zikiwemo vikosi vya zimamoto, polisi, na wanajamii wa kujitolea, zimekuwa zikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha usalama wa manusura na kurejesha hali ya kawaida katika eneo hilo.
Wakazi wa Kariakoo na maeneo jirani wamehimizwa kushirikiana na serikali kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: