Articles by "AJ"
Showing posts with label AJ. Show all posts

Mkuu wa Idara ya Wateja wakubwa wa Vodacom Tanzania PLC Rahma Dachi (wa pili kulia) akimkabidhi zawadi ya shukrani kwa wasaidizi wa wachezaji wakiwakilishwa na afisa utawala wa Lugalo Golf Club Major Chadiel Msechu (wa kwanza kushoto). Tukio hilo limefanyika jana wakati wa ugawaji wa tuzo na zawadi kwa washindi wa mchezo wa golf jijini Dar es salaam.
Vodacom Tanzania, kupitia kitengo cha Vodacom Business kinachoshughulika na wafanyabiashara wakubwa pamoja na wadau mbalimbali wa michezo, wamekabidhi tuzo na zawadi kwa washindi tofauti wa mashindano ya golf yaliyofanyika katika uwanja wa TPDF Lugalo jijini Dar es Salaam, tarehe 2 Agosti mwaka huu. Hafla hiyo ilikuwa sehemu ya mashindano ya Vodacom Corporate Masters, yaliyolenga kuhamasisha ushiriki wa wadau kutoka sekta mbalimbali kupitia michezo ya kijamii kama golf. Tuzo hizo zilitolewa kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na watoto wa kike na wa kiume, wanawake, wanaume pamoja na wachezaji wa golf waliobobea kutoka mashirika tofauti. Kupitia tukio hili, Vodacom iliendeleza dhamira yake ya kuunga mkono michezo, kukuza vipaji na kudumisha uhusiano wa kijamii na wadau wake wa karibu.

Dodoma. Tarehe 10 Aprili 2025: Baada ya ufanisi mkubwa kwenye mauzo ya Samia Infrastructure Bond yaliyohitimishwa mapema Januari, Serikali imewataka makandarasi kote nchini kuchangamkia mikopo iliyoanza kutolewa na Benki ya CRDB.

Utoaji wa mikopo hiyo uliozinduliwa na Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa jijini hapa itatolewa kupitia mfumo maalumu ujulikanao kama Samia Financing Portal, utawaunganisha wadau wote watatu yaani Benki ya CRDB, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na mkandarasi hivyo kupunguza muda wa kushughulikia maombi ya mhusika.
“Ni fahari kubwa kuona mafanikio ya juhudi za pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi kupitia TARURA na Benki ya CRDB ambao kwa pamoja tulizindua Samia Infrastructure Bond mwishoni mwa mwaka jana. Fedha zilizopatikana kutokana namauzo ya hatifungani hiyo sasa zipo tayari kwa ajili ya kutekeleza malengo yaliyokusudiwa. Niwaombe makandarasi kuitumia vyema fursa hii wanapotekeleza miradi waliyoshinda,” amesema Waziri Mchengerwa.


Waziri amesema ushirikiano baina ya TARURA na Benki ya CRDB unakusudi akuondoa changamoto ya upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi kwa wakati ya barabara mijini na vijijini jambo litakalochangia kuharakisha maendeleo ya wananchi.
“Fedha zote kiasi cha shilingi bilioni 323 ziizotokana na mauzo ya Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond zitatumika kutekeleza miradi ya barabara inayosimamiwa na TAMISEMI.

Mfumo wa Samia Infrustructure Portal utarahisisha uchakataji wa maombi ya makandarasi ukitumia muda mfupi sana tofauti na ilivyo kwa mikopo mingine. Ni imani yangu na serikali kwa ujumla kuwa hali ya utekelezaji wa miradi itabadilika baada ya kuzinduliwa kwa mikopo hii itakayotolewa na Benki ya CRDB,” amesisitiza Waziri Mchengerwa.

Mpaka tarehe 09 Aprili 2025, waziri amesema tayari imeshalipa madeni ya makandarasi zaidi ya 457 na malipo ya makandarasi wengine 322 yanakamilishwa na watalipwa na TARURA hadi kesho, Ijumaa ya tahere 11 ikiwa ni maelekezo ya Serikali kuhakikisha makandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali nchini wamelipwa fedha zao na hawakwamishwi.
Kabla ya kumkaribisha waziri, Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya CRDB, Vaxery Makwi amesema benki imekamilisha utaratibu wa ndani na sasa ipo tayari kuanza kuwawezesha makandarasi kutekeleza majukumu yao bila kikwazo cha kifedha.

Makwi amesema makandarasi watawawezesha kupata dhamana za utekelezaji wa miradi wa kama dhamana ya utekelezaji wa mradi wakati wa utekelezaji wa zabuni (Bid Bond), Dhamana ya Utekelezaji wa Mradi (Performance Guarantee), na Dhamana ya Malipo ya Awali (Advance Payment Guarantee) na hati ya uthibitisho wa malipo (Letter of Credit).
Vilevile, watanufaika na mkopo wa kuanzisha mradi (bridge financing) mkopo wa bidhaa zinakazoagizwa kutoka nje (Post Import Loan), na uwezeshaji kupitia cheti cha malipo (Certificate Discounting).

“Ili kuhakikisha walengwa wanapata fedha kwa wakati, tumeandaa mfumo unaoitwa Samia Infrastructure Finance Portal unaopatikana kwenye tovuti ya Benki yetu ya CRDB pamoja na ile ya TARURA ambako makandarasi watatakiwa kujisajili ili kunufaika na uwezeshaji unaotolewa. Baada ya kujisajili, mkandarasi ataweka taarifa zake zote ambazo zitaenda TARURA kwa ajili ya uthibitisho, kisha taarifa hizo zitatumwa benki,” amesema Makwi.

Mfumo huo, Makwi amesema unamruhusu mwombaji kujisajili na kuomba mkopo autakao akiwa mahali popote pale bila kulazimika kwenda tawini hivyo kuokoa muda ambao anaweza kuutumia kufanya mambo mengine. Awali, amesema ilikuwa inamchukua mkandarasi mpaka mwezi mmoja kupata uthibitisho wa mradi anaouombea mkopo sasa hali imebadilishwa kupitia mfumo huo.
Ili kunufaika na mkopo wa makandarasi, mwombaji anatakiwa kuwa amesajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi Tanzania (CRB) katika daraja lolote, awe na mkataba halali wa mradi unaoendana na ukomo wa daraja lake kulingana na viwango vya CRB, awe na uzoefu wa kazi unaothibitishwa na angalau mradi mmoja aliowahi kuutekeleza kwa mafanikio, na awe na historia nzuri ya kukopa inayoweza kuthibitishwa.

“Napenda kuwajulisha makandarasi kuwa Benki yetu ya CRDB imejipanga viliyo kutoa mikopo hii kupitia matawi yetu yaliyopo kote nchini. Wafanyakazi wetu wameandaliwa ipasavyo na wana ujuzi wa kutosha kuhakikisha huduma hii inatolewa kwa ufanisi na kwa haraka. Katika kila tawi, kuna timu maalum kwa ajili ya kutoa ushauri wa kitaalamu. Nawawakaribisha makandarasi kote nchini kutumia fursa hii ili kukamilisha miradi wanayoitekeleza,” amesema Makwi.









Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Chai Tanzania (TBT) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB pia, Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto) akipokea vitendea kazi vya majukumu yake kutoka kwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (wa kwanza kushoto) katika mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wa sekta ya chai nchini uliofanyika jijini Dodoma leo. Wengine katika picha ni wajumbe wa bodi hiyo ya wakurugenzi ambao ni Imani Kajula (wa pili kulia) na Nashon Kamnyungu (wa kwanza kulia).
Dodoma. Tarehe 8 Aprili 2025: Katika mkakati wa kuongeza mchango wa sekta ya chai nchini, serikali imemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania (TBT) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB pia, Abdulmajid Nsekela kuhakikisha anatumia uzoefu wake katika sekta ya fedha pamoja na uzoefu walionao wajumbe wake kushughukia changamoto zinazorudisha nyuma maendeleo ya chai nchini.

Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe alipozindua bodi mpya ya wakurugenzi ya TBT kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wa tasnia ya chainchini uliofanyika jijini hapa.
Bashe amesema tangu awe waziri wa kilimo haridhishwi na maendeleo yaliyopo kwenye zao la chai kutokana na mambo mengi yanayoendelea ikiwamo kushuka kwa mapato yatokanayo na mauzo yake nje ya nchi, wasafirishaji kutoelewa kwa uwazi kiasi wanachokipeleka nje ya nchi na kushuka kwa kiasi kinachozalishwa nchini kilamwaka.


“Tulipokuwa tunatafuta mwenyekiti mpya wa Bodi ya Chai Tanzania tulisema tumpate mtu anayetoka sekta ya fedha atakayeijua sekta ya chai ambayo changamoto yake kubwa ni upatikanaji wa mikopo ili ashiriki kuitatua changamoto hiyo na kuifanya sekta hii ikue na kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye kipato cha wakulima na wadau wa sekta ya chai pamoja na kuchangia zaidi kwenye pato la taifa,” amesema Mheshimiwa Bashe.


Baada ya kumpata mwenyekiti, amesema waliwatafuta wajumbe wenye ujuzi na uzoefu katika sekta tofauti ikiwamo masoko ili wasaidie kuweka mkakati wa kuitengenezea nembo imara chai ya Tanzania itakayoiwezesha kushindana kimataifa.
Kwenye maelekezo yake kwa bodi hiyo ya wakurugenzi pamoja na menejimenti ya TBT, Waziri Bashe amesema changamoto zote zilizopo kwenye sekta ya chai ni mfumo wake hivyo ameitaka bodi ya wakurugenzi kuupitia mpango mkakati waTBT pamoja na sera ya chai na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuziondoa kero zilizopo.


“Hakikisheni kunakuwa na uwazi wa taarifa kwa sababu wapo baadhi ya wasafirishaji ambao hawaisajili mikataba yao yote hivyo kuinyima serikali taarifa sahihi. Kwa msafirishaji atakayebainika kutotoa taarifa za mzigo anaosafirisha afutiwe leseni. Sekta ya chai inao wadau wasiopenda kukutana, kila mmoja anataka afanye mambo yake kivyake. Undeni kamati itakayowahusisha wadau wengine kuangali namna ya kuyashughulikia matatizo tuliyonayo ili tuwe na chai bora zaidi,” amesisitiza Waziri Bashe.


Akionyesha utayari wa kuyatekeleza maelekezo hayo, Nsekela aliyeteuliwa Februari 2025 kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TBT amesema anayo imani watazishughulikia kero zilizopo na kuifanya sekta ya chai kuwa na mchango mkubwa zaidi kuanzia kwa wakulima mpaka viwanda vinavyolichakata zao hilo.


“Tunahitajia maridhiano kwa kuwajumuisha wadau wote katika sekta ya chai. Asiwepo anayefaidi zaidi ya mwenzake. Ni lazima tufanye mabadiliko ya uwazi. Kila mdau awe na atoe taarifasahihi. Katika hatua hizo zote, tutahitaji ustahimilivu wa kuleta maboresho tunayoyakusudia. Tutafanya marekebisho muhimu katika mnyororo mzima wa zao la chai na tukisikilizana, tutafanikiwa kujenga pamoja,” amesema Nsekela akizinukuu 4R za Rais Samia Suluhu Hassan na kusisitiza kwamba zikitumika katika maeneo tofauti zinaweza kubadili hali iliyopo na kuleta maisha bora kwa Watanzania.
Licha ya uzoefu wake mkubwa katika sekta ya fedha nchini, Nsekela pia anaifahamu sekta ya kilimo kwani alikuwamwenyekiti wa Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (TSHTDA) kabla haujaunganishwa na TBT hivi karibuni na ni mwenyekiti wa Kamisheni ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania.


Tanzania kuna zaidi ya wakulima wadogo 32,000 wa chai huku wananchi wengine zaidi ya milioni 2 wakipata ajira zisizo za moja kwa moja katika sekta hii.
Kuanzia Disemba 2024 hadi Machi 2025, Tanzania imeingiza zaidi ya Shilingi bilioni 50.25kutokana na vibali vya kusafirisha chai nje ya nchi vinavyotolewa na TBT.


Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali imewavutia wawekezaji waliowekeza katika maeneo ya Kilolo, Njombe na Mbeya.Aidha, wawekezaji na wanunuzi kutoka maeneo mbalimbali duniani wameendelea kujitokeza ili kuwekeza na kununua chai ya Tanzania.
Akizungumzia baadhi ya kero zilizopo, Mwenyekiti wa Wakuu wa Wilaya kutoka halmashauri zinazolima chai nchini, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Mheshimiwa Jaffer Haniu ameitaja bei ndogo ya majani mabichi ya chai na kuchelewa kwa malipo ya wakulima pamoja na kufungwa kwa viwanda vya chai kuwa kunawakatisha tamaa wakulima.







Na Veronica Mwafisi-Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepitisha Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zake kwa Mwaka wa fedha 2025/26 baada ya kupitia mafungu yote yaliyo chini ya ofisi hiyo na kujiridhisha.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Kyombo amezungumza hayo tarehe 27 Machi, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Bunge jijini Dodoma alipokuwa akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo mara baada ya Wajumbe wa Kamati kujadili na kuridhia taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora.

“Kamati imejadili na kuridhia kupitisha Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zake kwa Mwaka wa fedha 2025/26, niwapongeze kwa maandalizi mazuri yenye uwazi, Kamati inawaasa kuwa na matumizi mazuri ya fedha pale zitakapopitishwa katika vikao vya Bunge la Bajeti ambapo tunaamini mtafikia malengo ya kuwatumikia watanzania kwa maendeleo ya nchi. Mhe. Kyombo amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kwa kuwa na majadiliano mazuri na ofisi anayoiongoza ambayo wanaamini yatawasaidia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa majukumu yao kupitia bajeti hiyo.

Mhe. Mwenyekiti, nitoe shukrani za dhati kwa niaba ya ofisi ninayoiongoza mara zote tumepokea maoni, ushauri na michango mbalimbali kutoka katika Kamati yako inayolenga kuboresha Utumishi wa Umma nchini kwa lengo la kutimiza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Utumishi wa Umma uliotukuka.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya ofisi hiyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amesema Kamati hiyo imekuwa msaada mkubwa wa kuiongoza Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora kwa kuwapatia maarifa mengi kutoka kwa Wajumbe wote wa Kamati hiyo yenye kuboresha utendajikazi.

Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na taasisi zake kwa Mwaka wa fedha 2025/26 umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Maelekezo ya Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26).



Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu) Dkt. Rose Likangaga akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mjumbe wa Tume, Dkt. Zakia Mohamed Abubakar.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu) Dkt. Rose Likangaga akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mjumbe wa Tume, Dkt. Zakia Mohamed Abubakar.
Mwenyekiti wa Mafunzo, Bw. Khalid Khalif akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Na Mwandishi wetu, Songea
Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura mkoani Ruvuma wametakiwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao baadae mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Zakia Mohamed Abubakar kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu) Dkt. Rose Likangaga wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa watendaji hao mkoani Ruvuma.

“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao,” ilisema sehemu ya hotuba hiyo.

Dkt Likangaga akisoma hotuba hiyo alisema ni matarajio ya Tume kuwa, mara baada ya zoezi hili lililopo mbele yao kukamilika watu watakaokuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni Wapiga Kura Halali.

Aidha alisema, jukumu la uhamasishaji linawahusu moja kwa moja wao watendaji kwa kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yao kupitia nyenzo walizonazo.

“Ninasisitiza kwamba, mabango na vipeperushi mtakavyopewa na Tume mvisambaze mapema katika kata zote zilizopo katika halmashauri zenu. Kazi yenu kubwa ni kusimamia na kuendesha shughuli zote za uboreshaji katika halmashauri zenu,”ilisisitiza hotuba hiyo.

Watendaji hao wameatakiwa kuisoma kwa umakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sheria za Uchaguzi, Kanuni za Uboreshaji, Maelekezo na Miongozo yote inayotolewa na Tume ili kazi yao ifanyike kwa uadilifu na haki.

Pia wametakiwa kuwasiliana na Tume kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala yote yanayohusiana na utekelezaji wa majukumu yao pindi wanapokutana na changamoto zozote.

“Tume imetekeleza jukumu lake katika hatua ya mafunzo na hivyo nanyi mna wajibu wa kuhakikisha kuwa mnatekeleza kikamilifu majukumu yote mliyokasimiwa,” ilisema sehemu ya hotuba hiyo.

Pia Tume imewataka watendaji hao kuwa makini katika kila eneo la usambazaji na utunzaji wa vifaa na muda sahihi wa ufunguaji na ufungaji wa vituo vya kuandikishia wapiga kura.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unataraji kuanza Januari 12 hadi 18, 2025 katika mikoa ya Songwe, Njombe, Rukwa na Ruvuma kwenye Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Mbinga, Mbinga Mji, Wilaya ya Songea na Manispaa ya Songea ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

Mafunzo hayo yaliwahusisha Maafisa Waandikishaji,Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi, Maafisa TEHAMA wa Halmashauri.


Washiriki wakisikiliza hotuba ya kufunga mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea

mmoja wa wakufunzi akitoa maelekezo wakati wa mafunzo kwa vitendo.

Washiriki wakifanya mafunzo kwa vitendo.