Articles by "KILIMO"
Showing posts with label KILIMO. Show all posts
Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha SAGCOT, kinachoratibu maendeleo ya kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Ukuaji wa Kilimo Tanzania (SAGCOT),Geoffrey Kirenga amesema watamkumbuka Rais wa awamu ya Pili, Ali Hassan mwinyi kwa kuleta ushawishi mkubwa katika maendeleo ya kilimo nchini.

Kauli hiyo ameitoa katika taarifa yake ya buriani kwa Rais huyo aliyezikwa kijini kwao Mangapwani kisiwani Unguja Machi 2 mwaka huu.

Alisema kifo Rais Mwinyi, aliyeliongoza taifa la Tanzania kuanzia mwaka 1985 hadi 1995 ni pigo kubwa kwa wakulima na wadau wa maendekeo kwa ujumla.

"Kipindi cha Rais Mwinyi kilikuwa alama ya sera za mageuzi zilizoboresha kilimo, nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania na ustawi wa wananchi wake," Kirenga alisema.

Alisema chini ya uongozi wa Mwinyi, nchi ilianza Mpango wa Urekebishaji wa Uchumi mnamo mwaka 1986, hatua muhimu iliyolenga utulivu wa uchumi na marekebisho ya kimiundombinu yaliyohamasisha biashara binafsi na kurahisisha vizuizi vya uagizaji.

"Juhudi zake zilikuwa muhimu katika kujihusisha tena na taasisi za fedha za kimataifa kama Benki ya Dunia na IMF, hivyo kuiwezesha Tanzania kutoka katika matatizo ya kiuchumi na kuelekea kwenye njia ya ustawi," Kirenga alifafanua zaidi.

Utawala wa Mwinyi pia unakumbukwa kwa kuanzisha mfumo wa vyama vingi, ukianzisha enzi mpya wa kiuchumi na mageuzi ya kisiasa. Licha ya kukabiliwa na changamoto kama vile migogoro ya kifedha, ukame, na athari za mshtuko wa bei ya mafuta duniani, sera za Mwinyi ziliielekeza Tanzania kuelekea uchumi unaotegemea soko, zikibadilisha mwelekeo wa baadaye wa nchi.

"Katika miaka yake ya mwisho, Rais Mwinyi alijishughulisha kwa dhati na kilimo, akihamasisha faida za kilimo kwa vijana wa Tanzania. Shamba lake la papai huko Msalato, Dodoma, linasimama kama ushuhuda wa imani yake katika kilimo kama chachu ya maendeleo," alisema Kirenga.

Utetezi huu unaendana na juhudi za Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan, hususan Agenda 10/30 na Mipango Mkuu wa Mabadiliko ya Kilimo, yenye lengo la kuiinua sekta ya kilimo ya Tanzania hadi mafanikio mapya ifikapo mwaka 2030.

Kupitia urithi wake, Ali Hassan Mwinyi , Kirenga anasema anaendelea kuhamasisha vizazi vijavyo na mipango yenye lengo la kubadilisha sekta ya kilimo ya Tanzania, kuhakikisha mustakabali wenye ustawi na endelevu kwa taifa na wananchi wake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban akionesha maharage Lishe yanayouzwa na kampuni hiyo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

KAMPUNI ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha imewaomba wakulima Mkoa wa Singida kuchangamkia fursa ya kuanzisha kilimo cha maharage lishe na kuwa itawasaidia kuwatafutia soko.

Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo , Beatrice Alban hivi karibuni mjini Singida wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kilimo cha maharage hayo ambayo ni muhimu kwa masuala ya lishe.

Alban alisema wamefika Mkoa wa Singida kupeleka fursa yenye faida zaidi ya tatu ya kwanza ikiwa inahusu masuala ya lishe ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kuanzia ngazi ya familia hadi jamii ambapo Seikali imeiona na ya pili ni uchumi hasa kwa mkulima ambaye kila siku amekuwa hapigi hatua na badala yake amekuwa akirudi nyuma.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwa kuiona changamoto hiyo kampuni hiyo inatamani kuona mkulima akipiga hatua kubwa katika masuala ya kilimo na sio kurudi nyuma.

Alban alizungumzia fursa nyingine kuwa ni ile inayohusu afya ya watoto ambayo inakwenda na usemi usemao ‘afya ya mtoto ni furaha ya mzazi’ kwani mtoto akiwa na afya bora mzazi atafanya kazi vizuri na kutunza kila kitu anachokipata na kujumuika na jamii katika shughuli mbalimbali.

Alisema katika nchi yetu kumekuwa na changamoto ya lishe hasa kwenye mikoa mingi hasa ile inayofanya vizuri kwenye masuala ya kilimo,

Alisema Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Siliani Arusha waligundua maharage yenye virutubisho vingi ambayo yanaweza kuufanya mwili kukua na kupokea matokeo kwa haraka na kuwa maharahe hayo yanaitwa maharage lishe.

Alisema maharage hayo ni ya kawaida na yanapikwa kama yanavyopikwa mengine lakini hayo yamerubishwa kwa kutumia teknolojia ya udongo na kuongezwa madini ya zinki na chuma ambayo ni muhimu na kuwa kama mwili wa binadamu utakosa madini hayo utakuwa ukinyemelewa na magonjwa mengi na mgonjwa akipelekwa hospitali kutokana na mwili wake kukosa madini hayo hata dawa atakayopewa haitaweza kufanya kazi.

“Mwili wetu unahitaji kuwa na madini ya zinki na chuma kwa wingi ili tuweze kuwa na afya bora,” alisema Alban.

Mkurugenzi huyo alitoa maelezo hayo ili kuonesha umuhimu wa maharage hayo ambapo alisema kampuni hiyo ipo tayari kutoa ushauri na maafisa ugani kwa ajili ya kilimo cha maharage hayo ikiwa ni pamoja na kuwatafutia soko.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban akionesha maharage Lishe yanayouzwa na kampuni hiyo.


Muonekano wa maharage lishe yakiwa sokoni
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban (kushoto) akiwa katika moja ya maonesho ya vyakula.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban akiwa Uwanja wa Ndege wa Songwe jijini Mbeya wakati wa safari za kuhamasisha kilimo cha maharage hayo.

WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe kulia akimgaia mche wa Mbegu ya Mchikichi zinazozalishwa na Shamba la Wakala wa Mbegu Asa Mkinga Mkulima wakati wa halfa ya ugawaji miche hiyo shamba la Mwele lililopo wilaya ya MkingaWAZIRI wa Kilimo Husein Bashe katika akionyeshwa maeneo mbalimbali yeye miche ya Michikichi kwenye Shamba la Wakala wa Mbegu Asa lililopo wilayani Mkinga wakati wa ziara yake kulia ni Mtendaji Mkuu wa Asa Sophia Kashenge na kushoto ni mkulima aliyepewa miche shamba la Mwele lililopo wilaya ya Mkinga
Waziri wa Kilimo Husein Bashe katikati akitembelea Shamba la Wakala wa Mbegu ASA wilaya ya Mkinga wakati wa ziara yake shamba la Mwele lililopo wilaya ya Mkinga kulia ni Mtendaji Mkuu wa ASA Sophia Kashenge akisisitiza jambo
Mtendaji mkuu wa wakala wa Mbegu (ASA) Sophia Kashenge kushoto akimueleza jambo Waziri wa Kilimo Husein Bashe wakati alipotembelea wakala huo kwa ajili kugawa miche kwa wakulima
Mtendaji mkuu wa wakala wa Mbegu (ASA) Sophia Kashenge wa pili kutoka kulia akimuonyesha kitu Waziri wa Kilimo Husein Bashe wakati wa ziara yake kwenye Shamba hilo
Waziri wa Kilimo Husein Bashe akizungumza na wakulima wa wilaya ya Mkinga wakati wa ziara yake ya kutembelea Shamba la Mwele lililopo wilayani Mkinga
Mkurugenzi wa Bodi Mkonge Tanzania (TSB) Saady Kambona akiwa na viongozi wengine wakifuatilia kwa umakini maelekezo ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe
Watumishi wa Wakala wa mbegu za kilimo nchini (ASA) katika shamba la Mwele lililopo wilaya ya Mkinga wakiwa na viongozi wengine wakimsikiliza kwa umakini Waziri wa Kilimo Husein Bashe

Na Oscar Assenga,MKINGA

WAKALA wa mbegu za kilimo nchini (ASA) katika shamba la Mwele lililopo wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wamezindua zoezi la ugawaji wa mbegu za michikichi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu la kutaka zao hilo litumike ipasavyo kuongeza uzalishaji wa mafuta hapa nchini.

Hatua ya utekelezaji huo imekuwa na mafanikio makubwa naa kwa sasa wana michikichi elfu 88 na lengo ni kutoa michikichi laki mbili kwa wakulima ambao wataipanda katika maeneo mbalimbali na hivyo kuwezesha kilimo cha zao kuwa na tija

Akizungumza wakati akikabidhi Miche ya Michikichi kwa Wakulima wwa zao hilo lengo likiwa ni kukabidhi michikichi laki mbili katika wilaya ya Mkinga mkoani Tanga,Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema wananchi wanaopewa miche hiyo lazima wajaze fomu na kusaini ikiwemo kubaki na kumbukumbu ambazo zitapelekewa Halmashauri.

Alisema zitapelekwa huko ili maafisa kilimo wapewe taarifa kwenye vijiji vyao ambavyo wananchi wamepewa miche ili wawafuatilie kwa ukaribu wanapopata matatizo waone namna ya kuyapatia ufumbuzi huko huko vijijini.

Waziri Bashe alisema kwa sababu wamekuwa bahati mbaya wakigawa miche lakini mingi inaishia njiani haikui na wananchi wanapoteza muda na kuweka nguvu zao hivyo ni muhimu uwepo wa ufuatiliaji huo

“Leo tunagawa miche ya Michikichi wilaya ya Mkinga na wananchi ambao wamepewa watajaza fomu kusaini na kubaki na kumbukumbu ambazo baadae zitapelekwa Halmashauri pia maafisa Kilimo wapewa Taarufa kwenye Vijiji vyao kwa lengo la kuwa na ufuatiliaji wa karibu watakakukumbana na matatizo waweze kuyapatia ufumbuzi”Alisema

Hata hivyo Waziri huyo alisema wataanzisha mashamba makubwa ya pamoja ambao amesema miongoni mwa wafaidika watakuwa wananchi wa maeneo husika huku akisisitiza umuhimu wa maafisa kilimo wakae vijijini.

“Kama walimu wanakaa vijijini na maafisa kilimo nao wakate vijiji lakini pia mikutano ya Serikali za vijiji ifanye kazi ya kujadili maafisa Kilimo maeneo hayo kama hawatimizi wajibu wao kama hawafanyi hivyo serikali za vijiji ziandike taarifa kwenye mustasari zipelekewe kwenye WDC halafu ziende Halmshauri”Alisema

Waziri huyo alisema kwamba katikaa taarifa hiyo waeleze Afisa kilimo walionae hajawahi kuwatembelea wakulima hata siku moja kwani Serikali imegawa pikipiki na sasa wanawapa vishkambie na wamepekea vipima afya vya udongo ili wanapopima shamba wawaambie kama shamba linafaa kulima mashina au na huduma hiyo ni bure.

Katika hatua nyengine Waziri Bashe amemuagiza Mkurugenzi wa Asa Sophia Kashenge waanze shughuli za kuzalisha miche ya minazi kwenye kituo hichgo kama wanavyozalisha mice ya mazao mengine ili wananchi waweze kupata m iche ya minazi kutoka kwenye kituo hicho,

Awali akizungumza katika Mtendaji mkuu wa wakala wa Mbegu (ASA) Sophia Kashenge alisema kwa sasa wana michikichi elfu 88 na lengo ni kutoa michikichi laki mbili kwa wakulima.

Sophia alisema kwamba wamefarijika sana kuona Waziri kufika katika shamba hilo ambalo kipindi cha nyuma lilikuwa limetekelezwa lakini nguvu ya Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu imeonekana na wameweza kulifufua.

Alisema kwamba huwezi kufanya uzalishaji bila kuwa na miuondombinu ya umwagiliaji na hivyo lengo lao wataendelea kuongeza uzalishaji wa mbegu jambo ambalo ni kipaumbele cha nchi.

“Suala la Uzalishaji wa Mbegu za Michikichi ni Agizo la Waziri Mkuu tokea 2018 na sisi tumeitika vizuri tuna mashamba matatu ya ASA na la Mkinga ni la pili kwa uzalishaji wa michikichi na tunaamini kazi tunayoifanya ni kumuongezea mwananchi kipato”Alisema

Naye kwa upande wake Mkulima wa zao la Michikichi Mtarajiwa wilayani Mkinga Maaono Mkangwa alisema serikasli imechukua uamuzi mzuri kuwaletea kilimo hicho ambacho wanaamani kitawainua kiuchumi.

Mpango wa serikali ni kupunguza kiwango kikubwa cha kuingiza mafuta kutoka nje ya nchi wakati mafuta hayo yanaweza kuzalishwa na wakulima hapa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Ranchi ya Mbogo Bw. Naweed Mullah (kulia) akimuongoza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Daniel Mushi (kushoto) na timu ya washiriki wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) waliofika shambani kwake Chalinze, Septemba 03,2023 kwa ajili ya kuona namna anavyofanya shughuli zake.
Meneja Uendelezaji biashara kutoka kiwanda cha kusindika nyama cha "TANCHOICE" Bw. Luwungo Hassan (aliyesimama mbele) akielezea kwa ufupi historia ya kiwanda hicho kwa washiriki wa Mkutano wa Jukwa la mifumo ya Chakula (AGRF) waliofika kiwandani hapo Septemba 03, 2023.
Sehemu ya aina ya Ng'ombe waliopo kwenye ranchi ya Mbogo iliyopo Chalinze mkoani Pwani.

Nchi za China na Kenya zimeonekana kuvutiwa na fursa za uwekezaji zilizopo kwenye sekta ya Mifugo mara baada ya kuwatembelea wawekezaji wa ndani ambao ni Ranchi ya Mbogo na Kiwanda cha kuchakata nyama cha “Tanchoice” vilivyopo mkoani Pwani Septemba 03, 2023.

Ziara hiyo ambayo ni miongoni mwa shughuli za utangulizi zinazofanyika kabla ya kufanyika kwa mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya chakula barani Afrika (AGRF) iliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya Mifugo Dkt. Daniel Mushi ambapo alibainisha kuwa Wizara yake imejiandaa kikamilifu kutumia fursa zitakazojitokeza katika pindi chote cha mkutano huo kuiimarisha sekta ya Mifugo nchini.

“Sisi kwa sasa kama nchi tunasema “flagship” ya wizara yetu ni nyama na samaki ambazo tunazipeleka nje ya nchi na kwa mwaka jana tulifanikiwa kusafirisha tani elfu 14 na malengo yetu ni kuvuka tani elfu 16 kwa mwaka huu wa fedha na hilo tunaweza kufanikiwa kwa kuleta wadau wengi zaidi kama mbogo ranchi” Amesema Dkt. Mushi.

Aidha Dkt. Mushi ameongeza kuwa lengo la mkutano huo ni kupata wawekezaji na masoko mapya ili nyama inayozalishwa nchini iweze kuuzwa kwa wingi nje ya nchi hatua ambayo anaamini itachangia ongezeko la fedha za kigeni kwa kiwango kikubwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ranchi ya Mbogo Bw. Naweed Mullah amesema kuwa anatarajia kutumia mkutano huo wa kimataifa wa jukwaa la Mifumo ya chakula kuhakikisha anatoa elimu ya kutosha kwa washiriki wa ndani na nje ya nchi kuhusu njia bora za uongezaji thamani wa ng;ombe wa asili waliopo hapa nchini na barani Afrika kwa ujumla.

“Tunajua ulimwengu mzima unakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula hasa nyama na hali ya upatikanaji wa zao hilo imeendelea kushuka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi hivyo tunaamini jukwaa hili limelenga kujadili namna bora ya kukabiliana na changamoto hiyo” Ameongeza Bw. Mulllah.

Naye mmoja wa washiriki wa ziara hiyo Bi. Wangari Kurya kutoka nchini Kenya mbali na kukoshwa na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya Mifugo nchini amevutiwa zaidi na namna Serikali inavyohamasisha aina zote za kilimo ikiwa ni tofauti na kwao ambako kilimo mazao ndio kimekuwa kikisisitizwa zaidi.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya “FAMSUN” kutoka nchini China Bw. Joy Lee amevutiwa na namna Tanzania ilivyobarikiwa kuwa na ardhi kubwa na nzuri kwa ajili ya kufanya shughuli za ufugaji tofauti na hali ilivyo nchini kwao ambako wanalazimika kutumia kiwango kikubwa cha teknolojia ili kutekeleza shughuli hizo kwenye maeneo madogo waliyonayo.

“Ninatoa wito kwa wawekezaji wote kuja Tanzania kuna fursa nyingi sana za uwekezaji kwa upande wa sekta ya Mifugo” Amehitimisha Bw. 

Mkutano wa Jukwaa la kujadili Mifumo ya chakula barani Afrika unatarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia Septemba 05-08, 2023 ambapo takribani 6000 wa ndani na nje ya nchi wanatarajia kushiriki kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa mbolea kwa Pamoja wa TFRA, Josephy Charos akifafanua jambo wakati wa kikao baina ya wajumbe wa Bodi, Menejimenti na Wakulima wa AMCOSS ya Kaloleni tarehe 19 Julai, 2023 kulia kwake ni Mwenyekiti wa AMCOSS hiyo Mohamed Nditi
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Lilian Gabriel akizungumza jambo na wakulima wa AMCOSS ya Kaloleni (hawapo pichani) wakati wa kikao baina ya bodi, menejimenti ya TFRA na wakulima hao tarehe 19 Julai, 2023
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Shimo Peter Shimo akizungumza na wakulima wa AMCOSS ya Kaloleni Mkoani Kilimanjaro walipotembelea ili kujua changamoto wanazokutana nazo katika shughuli za kilimo hususani katika tasnia ya mbolea tarehe 19 Julai, 2023
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa , Thobias Mwesigwa akizungumza na wakulima wa Amcoss ya Kaloleli ya mkoani Kilimanjaro walipowatembelea kusikia changamoto zao pamoja na kuwashauri namna bora ya kuendeleza kilimo ili kupata tija zaidi

Na Mwandishi wetu -Kilimanjaro

Bodi ya Wakurugenzi na menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesema haitavumilia udanganyifu wa aina yeyote kwenye tasnia hiyo iwe unafanywa na watumishi, wafanyabiashara au wakulima.

"Hatutakubali kuvumilia udanganyifu wa aina yeyote iwe ni kwenye vipimo, bei ya mbolea au viwango vya ubora".

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Bodi ya TFRA, Thobias Mwesigwa wakati wa kikao baina ya wajumbe, menejimenti na wanachama wa AMCOSS ya Kaloleni iliyopo katika halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Mwesigwa ameeleza hayo baada ya mkulima Ramadhani Abdalla Mariki kuwasilisha ombi la kuwaagiza mawakala wa pembejeo za mbolea kuwa na mizani kwa ajili ya kupima mbolea ili kujiridhisha na uzito kama ulivyoandikwa kwenye vifungashio.

Aidha, mkulima Reward Shelukindo ameeleza uwepo wa baadhi ya wananchi wasiokuwa waaminifu wanaouza mbolea kinyume na bei elekezi iliyotolewa na serikali ikiuzwa kwa kiasi cha shilingi 75,000 hadi 100,000 jambo ambalo bodi hiyo imeeleza kutokuvumilia jambo hilo na kueleza hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watu hao wenye nia ovu.

"Wale waliobainika wamefanya udanganyifu msimu uliopita tunawafuta kwenye biashara ya mbolea lakini pia hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao na wale waliosafi tutaendelea nao.

Mwesigwa amewataka wakulima na watanzania kwa ujumla kutoa taarifa pindi wanapobaini uwepo wa udanganyifu kwenye kilimo hususan kucheza na ruzuku ya mbolea iliyotolewa na serikali kwa lengo la kuwakwamua wakulima na kuongeza uzalishaji.

"Mzee ukipata taarifa yoyote tupe tutaifanyia kazi. Naomba niwahakikishie wananchi kuwa changamoto hizo zitatatuliwa ili muweze kupata mbolea yenye viwango na kwa bei iliyotolewa na serikali" Mwesigwa alikazia.

Amewaomba wakulima kutoe ushirikiano kwa serikali, na kueleza kuwa, Bodi kwa kushirikiana na TFRA watajitahidi kutatua changamoto za wakulima hususan za kufikisha mbolea kwa wakulima kwa wakati.

Akieleza lengo la ziara hiyo, Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Josephy Charos amesema imelenga kuwatembelea wazalishaji, wanufaika ambao ni wakulima pamoja na wafanyabiashara ya mbolea ili kusikia changamoto wanazokutana nazo na kuzitafutia ufumbuzi.

Aidha, ameeleza kuwa, kufuatia Bodi kuwa na muda mfupi tangu iteuliwe imeona vyema kujifunza kwa vitendo na kupata uelewa wa kile wanachokisimamia kutokea chini kabisa.

Kwa upande wake Hadija Jabir Mjumbe wa bodi aliwashauri wakulima kuhakikisha wanapima afya ya udongo katika mashamba yao ili kuweza kutumia virutubisho sahihi kutokana na uhitaji uliojidhihirisha baada ya kupima.

Pamoja na hayo alitoa ushauri ka wakulima kutumia visaidizi vya udongo kama vile chokaa ili kuimarisha afya ya udongo na kuongeza mazao na tija kwenye kilimo.

Na Mwandishi wetu

Mpango mkakati wa AGRA wenye kaulimbiu ya kuchochea masoko jumuishi na yenye ushindani katika kilimo ili kuleta mabadiliko kwenye mifumo ya chakula nchini Tanzania umezinduliwa mjini Dodoma leo Jumatano.

Uzinduzi huo umefanywa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Hamis Ulega ambaye alkipongeza AGRA kwa kuja na mkakati huo wenye kugusa maeneo man manne muhimu.

Katika uzinduzi huo alikuwepo pia Waziri Mkuu Mstaafu na Mwenyekiti wa Baraza la Rais la chakula na kilimo, Mizengo Pinda.

Katika salmu zake kwenye uzinduzi huo Waziri wa Kilimo, Hussein Mohamed Bashe, akiwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Geofrey Mweli alisema serikali imeweka kipaumbele katika sekta ya kilimo ili kutengeneza maisha zaidi huku ikihakikisha kuwa vijana na wanawake wanajumuishwa.

“Tanzania inalenga kuwa ghala la chakula kwa Afrika na dunia nzima. Tumejitolea kufungua uwezo wa sekta ya kilimo, ambayo kwa sasa inachangia asilimia 25 ya Pato la Taifa na ni chanzo kikuu cha fedha za kigeni na chanzo cha ajira na utajiri.”

Alisema pamoja na mabadiliko ya teknolojia pia rais sanmia suluhu Hassan ametoa kibali cha kuajiri maofsia ugani wa kutosha na vifaa kusaidia kuleta mapinduzi

Pinda akizungumza alisema pamoja na kutambua mafanikio makubwa ambayo Tanzania imefikia bado kuna kazi kubwa ya kukabili umaskini mkubwa uliopo vijijini.

Ametaka sekta zote na wizara husika kuendeleza juhudi za kupambana na umaskini wa kipato na kuipa mifumo ya chakula

"Tuna ardhi, tuna kila kitu kinachohitajika. Tunachohitaji kufanya ni kuweka kipaumbele katika maendeleo na uboreshaji wa mifumo ya chakula ili kujenga maisha endelevu na kuinua jamii za vijijini."

Pinda :.. Tumefanya vizuri katika maeneo mengi na kubwa ni utulivu wa nchi yetu...mfumo wetu wa chakula haujapewa nafasi ya kutosha..kufungua uelewa zaidi juu ya hali ya nchi na umuhimu wa kuongeza kasi ya kutumia ardhi yetu ipasavyo na ndani ya rdhi yetu ipasavyo na ndani ya kipindi kifupi." alisema Pinda.

Alisema kuna umuhimu wa Nidhamu ya kazi na kujikita katika teknolojia za kileo kama walivyo Israel ambao hawana mito lakini wana kilimo cha umwagiliaji chenye tija.

Mkakati huo umelenga kuwajengea uwezo vijana na wanawake wa Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa kilimo na hivyo kukuza ajira ukuaji wa ustawi wa jamii na uchumi.

Mkakati huo unajumuisha uboreshaji wa upatikanaji wa fedha na masoko, na kukuza utumiaji wa teknolojia mahiri za hali ya hewa na matumizi ya pembejeo, kama vile mbegu na mbolea.

Mkakati huo umelenga kuwa na jukwaa thabiti la kushirikisha maarifa na ubunifu na kukuza mijadala yenye maarifa kuhusu changamoto katika kilimo na biashara na kuboresha ufikiaji wa afua muhimu za kifedha kwa lengo la kuwezesha matumizi makubwa ya teknolojia na sayansi katika kilimo.

Mkakati huo unatarajiwa kunufaisha wakulima milioni tatu nchini kwa kuwapatia masoko ya mazao yao.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katikauzinduzi huo Mkakati huo umeganyiwanyika katika maeneo tofauti Kijiografia ikiwamo Nyanda za Juu Magharibi, Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini, Nyanda za Juu Kaskazini na Zanzibar.

Aidha imeelezwa kuwa mazao yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na mahindi, mtama, maharagwe, mihogo, alizeti, soya, ngano, viazi na mazao ya bustani.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua mkakati huo, Mkuu wa Kikanda wa AGRA, Afrika Mashariki, Profesa Jean Jacques M. Muhinda alisema taasisi yake katika miaka hiyo mitano imelenga kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania kuwa na uzalishaji mkubwa wa chakula.

“Tanzania imeonyesha umahiri katika kubadilisha mifumo yake ya kilimo cha chakula. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, tunanuia kusaidia kufungua fursa zaidi za kilimo na masoko wakati nchi inapoendelea kufanya mabadiliko chanya kwenye kilimo. Tumejitolea kuunga mkono vipaumbele vya serikali kwa sekta ya kilimo ambayo imekuwa ikijijenga kwa miaka mingi.”

AGRA ambayo iliingia Tanzania mwaka 2006 imekuwa ikifanya kazi na serikali na mashirika binafsi na yale ambayo si ya kiserikali katika kuvutia uwekezaji, kusaidia mageuzi ya sera na kutoa zana za kilimo, maarifa na msaada kwa wakulima.

Aidha AGRA imeshirikiana na sekta binafsi kupitia Tanzania Agro-Industrialization Development Flagship,TAIDF, katika kuhakikisha kilimo kinakua na kinachangia katika pato la Taifa.

TAIDF ni mradi mkubwa wa kuwezesha maendeleo ya viwanda vya kilimo kwa kuhamasisha na kuratibu ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi; katika mradi huu ufadhili wa Dola za Marekani milioni 300 zilipatikana na kunufaisha wakulima zaidi ya milioni moja.

Serikali pia ilitoa vivutio mbalimbali vya kodi ili kuvutia uwekezaji kutoka sekta binafsi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Geofrey Mweli alisema Tanzania imelenga kuwa ghala la chakula kwa nchi za Afrika na duniani kote na hivyo haina budi kufungua uwezo wa sekta ya kilimo.

“Tanzania inalenga kuwa ghala la chakula kwa Afrika na dunia nzima. Tumejitolea kufungua uwezo wa sekta ya kilimo, ambayo kwa sasa inachangia asilimia 25 ya Pato la Taifa na ni chanzo kikubwa cha fedha za kigeni na chanzo cha ajira na utajiri." alisema Mweli.

Mwei alisema kwamba serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele sekta ya kilimo ili kukiwezesha kupaa huku ikisaidia kupata ajira wanawake na vijana.

Uzinduzi wa mkakati huo mpya wa AGRA unafanyika wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) litakaloanza Septemba 4 na kumalizika Septemba 8 mkoani Dar es salaam.

AGRF ni jukwaa kuu la Afrika lenye lengo la kuendeleza ajenda ya kilimo na mifumo ya chakula.

Mkutano huo utaleta pamoja makundi mbalimbali ikiwamo viongozi, watunga sera, wanasayansi, wakuu wa serikali, taasisi za kibinafsi, wakulima na vijana: ambao watakubaliana juu ya hatua za kivitendo ili kupata suluhisho kwa mifumo ya chakula barani Afrika.

"Jukwaa la mwaka huu lina umuhimu wa kipekee katika safari ya bara la Afrika kuelekea usalama wa chakula na ustawi wa pamoja." alisema

Mada ya mkutano wa 2023,itakuwa Regenerate, Recover, Act: Africa’s solutions to Food Systems Transformation, inalenga kuhakikisha bara la Afrika linaonesha umadhubuti wake katika kubadilisha mifumo ya chakula ili kuzalisha chakula cha kutosha na chenye lishe ndani yake na kuboresha jinsi kinavyozalishwa hasa ukizingatia mabadiliko ya hali ya hewa.

Afrika kwa sasa ni muagizaji mkuu wa chakula kutoka nje, na inaonekana uagizaji wa chakula utaendelea kupanda kutoka dola bilioni 43 mwaka 2019 hadi dola bilioni 110 mwaka 2025 kama hatua za makusudi zisipochukuliwa kukabili hali hiyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya AGRA, shirika hilo linafanya kazi zake kuwiana na Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini (ASDP II), unaolenga kubadilisha mifumo ya kilimo nchini Tanzania sambamba na kuongeza tija na kipato kwa wakulima wadogo.

AGRA pia inachochea ushirikishwaji wa sekta binafsi na uwekezaji katika kilimo kwa kushirikiana na serikali na washirika wa kimkakati.

Baada ya kujenga msingi thabiti wa teknolojia, ubia na miundo, AGRA iko tayari kuongeza kilimo chenye jumuishi na chenye ushindani nchini Tanzania.

Mkakati wake wa 2017-2021 uliunganisha ulilenga kuchochea na kudumisha Mabadiliko ya Kilimo Jumuishi. Mabadiliko hayo yalilenga kuongeza mapato na kuboresha usalama wa chakula kwa kaya za wakulima wadogo milioni 1.5 kwa kuwekeza dola za Marekani milioni 28.

kiasi hicho cha fedha kimewekezwa ambapo dola milioni 11.3 zilisambazwa kupitia ruzuku 31 tofauti ambapo wakulima 742,865 walinufaika.

Aidha, Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili umenufaika na ruzuku kubwa ya dola milioni 1.672. Zaidi ya wakulima 42,000 wamefaidika moja kwa moja na mpango huo, wakiongezewa na wakulima 34,000 walioathiriwa kupitia mipango mingine mbalimbali.

Kutokana na juhudi hizo Mauzo ya mazao chini ya mipango ya AGRA yalivutia $1.6 milioni.

Wakati AGRA ikizindua mpango mkakati wake mpya, shirika limedhamiria kuendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mabadiliko na ukuaji wa sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Mhandisi Erick Isack aliyesimama, akizingumzia namna ambavyo programu ya kuendeleza Kilimo na uvuvi, itakavyoboresha sekta ya uvuvi mkoani Lindi.
Wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu na Wizara ya Fedha, wakiangalia dagaa walioanikwa katika kichanja cha kienyeji, katika kata ya KILWA Kivinje,wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea maeneo yatakayoteleza programu ya KILIMO na UVUVI (AFDP) mkoani Lindi Leo.
Picha ikionesha washiriki wa Kikao cha ugeni kutoka programu ya kuendeleza Kilimo na uvuvi (AFDP) wataalam na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya KILWA,wakati Ujumbe huo ulipotembelea maeneo yatakayoteleza programu hiyo mkoani Lindi
Mtaalamu wa masuala ya Lishe na Jinsia Bi. Irene Mbando, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu akizingumzia namna ambavyo Programu Hiyo itakavyohusisha masuala ya Lishe na jinsia. Picha ikionesha Dagaa walioanikwa chini, katika kata ya KILWA Kivinje mkoani Lindi.
Kulia Bw. Robert Lee mtaalam wa Uvuvi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa maendeleo ya Kilimo Duniani (IFAD) akijadili jambo na Bw. Richard Abila mtaalamu wa Ufugaji wa viumbemaji kutoka IFAD.
Mfanya biashara wa dagaa,katika kata ya KILWA kivinje Wilayani KILWA, Mkoani Lindi akianika dagaa katika chanja ya kienyeji, ambapo programu ya kuendeleza Kilimo na uvuvi (AFDP) Itaenda kuwajengea chanja za kisasa.

Na Mwandishi Wetu - KILWA

IMEELEZWA kuwa, Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi AFDP inategemea kwenda KUBORESHA MAZINGIRA na maisha ya wavuvi wilayani Kilwa Mkoani Lindi.

Hayo yamesemwa mapema Leo tahehe 15 Mei 2023, Mkoani Lindi na Mtaalamu wa masuala ya mazingira wa mradi huo, Mhandisi Erick Isack kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu wakati Ujumbe wa Programu hiyo ulipokuwa katika Ziara ya kikazi Mkoani hapo.

Mhandisi Isack amesema programu hiyo itasaidia kujenga kiwanda Cha kuchakata samaki katika maeneo ya bandari ya uvuvi KILWA Masoko na ghala la kutunzia samaki. Sambamba na hilo programu hiyo pia itaenda kujenga vichanja vya kisasa vya kukaushia dagaa katika kata ya KILWA Kivinje.

Kwa Upande wake mtaalam wa masuala ya Lishe na jinsia Bi. Irene Mmbando alisema, programu itazingatia ushiriki wa jinsia zote ikiwa wanawake watashiriki Kwa asilimia sitini (60%) na Asilimia arobaini (40%) vijana.

Aliongeza Kwa kusema kuwa Mradi huo unalenga kufika kaya laki mbili na sitini ambazo zitahusika katika kilimo, uvuvi na ufugaji wa viumbemaji.

Akizingumzia masuala ya Lishe, mtaalamu huyo Alisema programu hiyo inakwenda kuzingatia maswala ya Lishe katika kaya husika.

Awali akiongea katika mazungumzo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya KILWA Bw. Eston Mngilangwa alisema, programu hii imezingatia mazingira halisi ya maeneo husika "Kwa upande wangu naona kama Lindi tumependelewa, tumeletewa miradi sita, programu hii tunaipokea Kwa mikono miwili, Tunashukuru sana, tunawahakikishia kuwa Mradi huu utaenda kuleta matokeo chanya, tumeshafanya maandalizi kwenye kila eneo,kama itatokea Kuna mahala tumekosea itakuwa ni suala la uelewa tuu." Alibainisha Mkurugenzi Huyo.

Ujumbe huo kutoka Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi, inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, uliohusisha wataalam kutoka IFAD, Wizara MIFUGO NA UVUVI, FEDHA na Wizara ya Kilimo itaendelea na ziara yake ya kikazi kisiwani Zanzibar wiki hii.
Na Waandishi wetu

IKIWA na lengo la kuwa kitovu cha uhakika wa chakula kimataifa, Tanzania inayosifika kwa uzalishaji wa chakula katika eneo la Afrika Mashariki imeanza kujiandaa kwa nguvu na kasi kubwa Mkutano wa AGRF-2023 (Jukwaa la Mifumo ya Chakula ya Afrika 2023) unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.

Katika maandalizi ya Mkutano wa AGRF-2023, utakaofanyika Dar es Salaam kuanzia Septemba 4 hadi 8, 2023 Tanzania wiki iliyopita iliratibu matukio matatu muhimu kuelekea mkutano huo.

Matukio hayo ni pamoja na uzinduzi wa Tanzania Agribusiness Deal Room, ambayo husaidia ushirikiano na uwekezaji katika mlolongo wa thamani ya mifumo ya chakula, Mkutano wa Value4Her Women in Agribusiness, unaowawezesha wanawake wajasiriamali na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu na kuanzisha mchakato wa usajili kwa ajili ya Mkutano wa AGRF-2023.

Matukio yote hayo yamefanyika kama sehemu ya kuonesha fursa na yameelezwa na wataalamu na wadau mbalimbali wa kilimo kuwa ni kuonesha dhamira ya Tanzania ya kuwavutia wawekezaji na kuendesha mabadiliko ya kimkakati katika sekta ya kilimo.

Mkutano huo mtarajiwa ambao umendaliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Kundi la Wadau wa AGRF umelenga kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo. Tanzania katika mkutano huo umelenga kuonesha mafanikio yake, kuonyesha uwezo wake mkubwa, na kuwavutia wawekezaji wa ndani na kimataifa wanaotafuta miradi ya kilimo yenye matumaini.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, anasema Mkutano huo unatarajiwa kuwaleta pamoja viongozi zaidi ya 3,000 kutoka bara la Afrika kujadili mabadiliko ya mifumo ya chakula na kuhakikisha uhakika wa chakula kwa wote.

Anasema chini ya uongozi wa maono wa Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania inajipanga kuwa kitovu cha uwekezaji cha kipekee barani Afrika.

Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimeelezea kuwa uhakika wa chakula ni kipaumbele kikubwa kwa Serikali ya Awamu ya Sita ya nchi hiyo, wakisisitiza dhamira yao ya kuhakikisha usambazaji na biashara endelevu na salama ya chakula.

Zikiwa na ushiriki wa kikamilifu katika maandalizi ya matukio hayo, wizara hizo mbili zinalenga kutumia uwezo mkubwa na uwezo kamili wa sekta ya kilimo, kuendesha ukuaji endelevu wa uchumi kwa kiwango kisichowahi kutokea, na kuzingatia hasa uwekezaji katika kilimo na ufugaji wa mifugo.

Mnamo Mei 12, 2023, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alizindua mchakato wa usajili kwa Mkutano wa AGRF-2023 huko Dodoma na akawaalika wadau wa kilimo duniani kujisajili na kushiriki katika tukio hilo muhimu.

Katika kufanikisha maandalizi hayo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alikutana na Bwana Amath Pathé Sene, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula ya Afrika (AGRF), kujadili jinsi mkutano wa kilimo wa AGRF unavyoweza kuhamasisha fursa za uwekezaji katika sekta ya mifugo na uvuvi nchini Tanzania.

"Katika mkutano wa AGRF, washiriki watakuwa na fursa muhimu ya kuona mafanikio na shughuli za wakulima wa Tanzania, wakipata ufahamu muhimu juu ya mazoea mazuri ndani ya sekta ya kilimo," alibainisha Bwana Sene. Aliweka mkazo kwenye jukumu muhimu la uvumbuzi, sera nzuri, na uwekezaji mkakati katika ujenzi wa mifumo thabiti ya chakula.

Aidha, mnamo Mei 11, 2023, Profesa Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, alizindua rasmi Tanzania Agribusiness Deal Room huko Dar es Salaam. Hatua hii inachangia ajenda ya mifumo ya chakula ya AGRF kwa kukuza ujasiriamali wa kilimo na kutoa mazingira rafiki kwa wakulima na wajasiriamali wa kilimo vijana kupata rasilimali, mafunzo, na fursa za mtandao.

"Agribusiness Deal Room ni nafasi yenye mwingiliano mkubwa kwa wahusika mbalimbali kushiriki na kuendeleza majadiliano katika ushirikiano wa pande mbili na pande nyingi. Hii, kwa upande wake, inasaidia kuongeza uwekezaji katika mlolongo wa thamani wa mifumo ya chakula," alisema Profesa Shemdoe.

Bwana Vianey Rweyendela, Meneja wa Nchi nchini Tanzania, alisisitiza umuhimu wa kitovu cha uwekezaji katika sekta ya biashara ya kilimo nchini Tanzania. Kwa mazingira yenye SME imara na fursa nyingi, nchi hiyo imekuwa kitovu kizuri cha uwekezaji kwa wawekezaji wanaotafuta fursa za kipekee na za kusisimua katika mifumo ya chakula.

Pia Mei 12, Profesa Riziki Silas Shemdoe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, alizindua rasmi Mkutano wa Value4Her Women in Agribusiness ambapo alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika sehemu ya biashara na kuvutia wawekezaji.

"Wakati tunazindua rasmi mpango wa Value for Her, nawahimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika sehemu hiyo ya biashara, kuonyesha uwezo wetu na kuunda fursa za uwekezaji za mabadiliko," alisema Profesa Shemdoe

Mkutano huo ulifanyika Dar es Salaam na ni hatua muhimu kuelekea Mkutano wa AGRF-2023 na lengo lake ni kuwawezesha wanawake wajasiriamali katika sekta ya kilimo. Value4Her Women in Agribusiness nchini Tanzania ina jumla ya wajasiriamali wa kilimo 152, ikivutia kampuni zinazoongozwa na wanawake na wadau katika mazingira ya kilimo.

Sabdiyo Dido Bashuna, Mkuu wa Idara ya Jinsia na Ujumuishaji katika AGRA, alihimiza mpango wa Value4Her nchini Tanzania kutumia fursa kubwa zinazotolewa na Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA).

"AfCFTA inafungua fursa kubwa kwa wajasiriamali wanawake Afrika. Kwa vyeti sahihi vya bidhaa na vyeti vya asili, wanawake wanaweza kufanya biashara kwa urahisi katika bara zima, wakifungua masoko mapyana kukuza ukuaji wa kiuchumi. Hebu wanawake wa Value4Her wawe wa kwanza kuchangamkia nguvu ya AfCFTA katika biashara na kujenga mustakabali wenye mafanikio!" alisisitiza Bashuna.
Kulia Mratibu wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bw. Salim Mwinjaka, akizungumza wakati wa ujumbe huo ulipotembelea Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, ujumbe huo upo katika ziara maalum ya ukaguzi wa maeneo yanayotekeleza program hiyo ya AFDP.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Profesa Godius Kahyarara akizungumza na ujumbe na wataalam kutoka Program ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) haupo katika picha ulipotembelea ofisini kwake jana jioni. ujumbe huo upo katika ziara maalum ya ukaguzi wa maeneo yanayotekeleza program hiyo ya AFDP.
Kushoto Bi Jackline Motcho, Afisa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi nchini (AFDP) akizungumza na baadhi ya wajumbe waliokuwepo katika ziara ya ukaguzi wa maeneo yanayotekeleza mradi huo katika kijiji cha Rubambagwe Wilayani Chato, Mkoani Geita.
Bi. SIFA Bujune, ni mfugaji wa viumbemaji katika kijiji cha Rubambagwe kilichopo Wilayani Chato, Mkoani Geita, akizungumzia baadhi ya changamoto wanazokutana nazo katika majukumu yao.
Picha ikionesha moja ya jengo lililojengwa katika kijiji cha Rubambagwe na Mradi wa kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) litakalo tumika wakati wa kutoa mafunzo kwa wafugaji wa viumbemaji

Na Mwandishi wetu - CHATO

Imeelezwa kuwa Mradi wa kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) unakwenda kutatua changamoto wanazokumbana nazo wafugaji VIUMBEMAJI katika kituo Cha Rubambagwe kilichopo Wilayani Chato,mkoani Geita.

Hayo yameelezwa Leo na Dkt. Nazaeli Madala, Mkurugenzi wa ukuzaji viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Dkt. amesema kituo Cha Rubambagwe kipo katika UJENZI ambapo, Nia na madhuni ya kituo hiki ni kuhamasisha, kuendeleza na kusimamia ukuzaji viumbe Maji,Kwa maana Ufugaji wa samaki kwa mabwawa na vizimba katika ukanda wa ziwa Victoria.

Alisema kuwa, kituo kitakwenda kutoa mafunzo ya utengenezaji wa chakula cha samaki,Ufugaji na ulishaji sahihi wa samaki, wafugaji watafundishwa pia namna ya kutengeneza chakula Cha samaki Kwa kutumia malighafi za asili, kutakuwa na majengo ambayo yatawezesha wafugaji wanaotoka mbali kukaa hapo wakati wa mafunzo, sambamba na hilo, kutakuwa na kiwanda kidogo Cha kutengeneza chakula cha samaki.

Aliongeza kusema kuwa kituo pia kitazalisha vifaranga vya samaki ili kuweza kutatua changamoto ambazo wafugaji wanakutana nazo "kutakuwa na kitotoleshi ambacho kitakuwa na uwezo mkubwa sana wa kuzalisha vifaranga ambavyo vitakwenda kuwezesha vitotoleshi vya sekta binafsi kupata wazazi "Alifafanua

Akiongea na ujumbe huo, Bi. Sifa Buguni mmoja wa wafugaji wa samaki Rubambagwe Chato alibainisha changamoto kubwa mbili walizokumbana nazo kabla ya mradi huu kukamilika kuwa ni pamoja na uhaba wa upatikanaji wa mbegu na chakula cha kulisha samaki.

Awali, ujumbe huu wa IFAD ulifika ofisini Kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Prof. Godius Kahyarara ambapo alisema ni wakati sasa kwa wakazi wa Mkoa wa Geita kujikita katika katika shughuli za kilimo na ufugaji wa viumbemaji na kwa uwekezaji wa uhakika kuweza kuwekeza katika sekta hizo kama wanavyowekeza katika sekta ya madini.

Ujumbe kutoka IFAD, wataalam na Mratibu wa Programu hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bw. Salim Mwinjaka wapo katika ziara ya ukaguzi wa maeneo yanayotekelezwa mradi huo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi akizungumza, katika ufunguzi wa warsha ya Siku mbili ya utambulisho na uelewa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa watendaji wa Mikoa na Halmashauri. Dodoma Leo
Picha ikionesha baadhi ya watendaji wa Mikoa na Halmashauri, wakifuatilia wasilisho waliposhiriki katika, warsha ya Siku mbili ya utambulisho na uelewa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa watendaji wa Mikoa na Halmashauri. Dodoma Leo
Sehemu ya washiriki wa warsha ya Siku mbili ya utambulisho na uelewa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa watendaji wa Mikoa na Halmashauri. Dodoma Leo

Na Mwandishi Wetu – Dodoma

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewataka watendaji wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kusimamia vizuri utekelezaji wa Programu ya Kilimo na Uvuvi katika maeneo yao kwani ni sekta muhimu katika uchangiaji wa uchumi na usalama wa chakula nchini.

Ameyasema hayo mapema leo Jijini Dodoma, katika warsha ya utambulisho na uelewa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa watendaji wa Mikoa na Halmashauri.

Dkt. Yonazi amesema kuwa Serikali imeona kuna ulazima wa kuwepo kwa usalama wa mbegu katika kilimo hivyo kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo nchini ASA imeweza kuwekeza mbegu kwa wingi ili kuyafikia maono ya serikali.

“Serikali imeendelea kusimamia uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora ambapo hadi kufikia Aprili 2023, jumla ya tani 49,962.35 za mbegu bora zimepatikana sawa na asilimia 26.68 ya mahitaji ya tani 187,197 kwa mwaka,”Alisema Dkt. Yonazi.

Aliongezea kuwa, serikali imejitahidi kuweka nguvu katika upatikanaji wa mbegu hizo ili kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula nchini, na kwa upande wa sekta ya uvuvi imehakikisha kunakuwa na manufaa ya rasilimali zilizopo katika sekta hiyo kwani bado hazijatumika vizuri.

Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali ina mpango wa kununua meli zitakazotumika katika uvuvi wa kina kirefu cha bahari na hivyo kuweza kuongeza lishe na hatimaye nchi kunufaiika na rasilimali za uvuvi.

Aliendelea kufafanua kuwa, Programu hii pia, itahusisha ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu mingine ikiwa ni pamoja na upanuzi wa vituo vya uzalishaji wa vifaranga vya samaki cha Kingolwira Morogoro.

“Lazima tushirikishe wadau ili tupeleke elimu ya kuweza kuzalisha vifaranga na kujenga mabwawa, natoa msisitizo kwa viongozi wa mkoa kuwa kuna jukumu la usimamizi, tuhakikishe tunasimamia vizuri mradi huu, kushauri na kuutekeleza kwa wakati.” Alisisitiza Dkt. Yonazi

Awali, akiongea wakati wa Ufunguzi wa Warsha hiyo Bw. Paul Sangawe Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, alisema lengo la programu hii kwa upande wa sekta ya uvuvi, ni kuendeleza ufugaji wa viumbe maji pamoja na kuanza uvuvi wa bahari kuu.

“Tunatazamia katika program hii meli zitanunuliwa kwa matumizi ya pande zote mbili za Muungano na kuwezesha nchi yetu kwa mara ya kwanza kufanya uvuvi katika bahari kuu ili kuweza kutumia rasilimali tulizonazo kwa ufanisi, lakini vile vile uzalishaji wa mbegu pamoja na usambazaji, na kuhakikisha fedha ambazo za mkopo ambazo tumepewa kutoka shirika la IFAD takribani dola 58.8 milioni,zinatumika kwa ufanisi na kuleta tija katika utelezaji wa program hii.” Alisisitiza

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchumi na Uzalishaji toka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Afisa Kilimo Mkuu Dkt. Rehema Mdendemi amesema programu hii ya maendeleo ya kilimo na uvuvi itaenda kuboresha maisha ya wakulima na wavuvi , na kujitosheleza kwa usalama wa chakula na kuleta ajira hivyo program hii ni ya muhimu kwa serikali na wanachi kwa ujumla.
Kaimu Rasi wa Ndaki ya Uchumi Kilimo na stadi za Biashara Dkt. Zena Mpenda akifungua warsha ya Wadau wa Mradi wa TRADE HUB kujadili matokeo ya utafiti.

Na Amina Hezron, Morogoro

WADAU wa zao la Soya kahawa miwa na nyama pori wametakiwa kushiriki kikamilifu kwenye kutoa mapendekezo na maoni yao kwenye Mradi wa Utafiti wa Biashara,Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub) ili matokeo yatakayopatikana yaweze kuinua tija ya mazao hayo nchini.

Hayo yameelezwa na Kaimu Rasi wa Ndaki ya Uchumi Kilimo na stadi za Biashara Dkt. Zena Mpendu aliyemuwakilisha Rasi wa Ndaki hiyo Dkt Damas Philip katika warsha iliyoandaliwa na mradi huo ili kuwasilisha matokeo ya awali ya utafiti wao kwa wadau ili kupata maoni yao juu ya namna bora ya kufanya biashara ya haki na endelevu.

Amewataka wadau hao kuzingatia kuwa tasnia hizo zinagusa kwa namna moja ama nyingine maisha na maendeleo ya wadau mbalimbali pamoja na uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla hivyo watumie fursa hiyo kwa makini kutoa maoni yao ya namna bora ya kuboresha biashara katika tasnia hizo zote za Nyama pori na Mazao ya kilimo.

“Ni vizuri tunaposikiliza hizi mada zinazotolewa tuangalie inaelezea kweli ile hali halisi kwenye maeneo yetu ili tuweze kuboresha yale ambayo tumeyaona lakini pia tuweze sasa kuangalia mapendekezo yanayotoka tuone hayo mapendekezo yatafanyika yanawezekana ili tukitoka hapa tuwe na mapendekezo ambayo ni bora zaidi”, alisema Dkt. Zena.

Dkt. Zena ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikiboresha mara kwa mara Sheria, taratibu na Kanuni kuhakikisha kwamba biashara hizo hazisababishi ongezeko la uharibifu wa mazingira na upotevu wa baionuai hivyo ni muhimu kama wadau wa biashara kuhakikisha wanaingia kwenye mikataba ya kijani kwenye biashaa zao ili kuwe na biashara endelevu kwaajili ya watu na ulimwengu pia.

Akieleza malengo ya warsha hiyo Mratibu wa Utafiti na Machapisho SUA Prof. Japhet Kashaigili amesema kuwa ni kuwasilisha kwa wadau matokeo ya tafiti kadhaa ambazo mradi huo umeyapata ili wapate nafasi ya kuyajua, kuyajadili na kutoa mapendekezo ili kuona ni namna gani yanaweza kuchangia kwenye maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

“Lengo lingine la pili la warsha yetu hii na mradi ni kutengeneza mpango au njia itakayotupeleka nchi mahali fulani kuptia ufanyaji wa biashara yenye haki na endelevu nchini Tanzania lakini pia bidhaa zetu ziweze kuhimili ushindani kwenye masoko ya kimataifa na kukuza uchumi”, alifafanua Prof. Kashaigili.

Aidha amesema dhumuni kubwa linalobeba mradi huo ni kuhakikisha biashara ya mazao na nyama pori inakuwa ni injini ya ukuaji wa uchumi jumuishi,Kuondoa umasikini na kama mbinu ya kutekeeleza maendeleo endelevu kama ilivyosisitizwa kwenye Mpango wa maendeleo endelevu bila kuchangia uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Mkuu wa mradi huo Prof. Reuben Kadigi amesema warsha hiyo ya wadau ni muhimu sana katika kupata maoni na mapendekezo ambayo yatawasaidia watafiti kuweza kutengeneza andiko la sera ambalo litawasilishwa Serikalini ili kusaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Kila mchango wa mdau unaotolewa andika mahali kila ushauri andika ili mwisho wa siku tupate kitu kizuri kifupi cha kuwasilisha serikalini baada ya kufanya uchambuzi wa kina kulingana na matokeo tuliyoyapata maana mwisho wa siku hatuwezi kupeleka kwa watunga sera kitu kinacholeweka nawaweze kukifanyia kazi kwa ustawi wa biashara nchini”, alieleza Prof. Kadigi.

Kwa upande wake Dkt. Charles Malaki aliyemuwakilisha Kaimu Rasi wa Ndaki hiyo amewashukuru wadau waliojitokeza katika warsha hiyo na amewataka kutoa maoni na mapendekezo ya kuboresha matokeo ya tafiti hizo ili kuisaidia Serikali baadae kupata sera bora zitakazosaidia kuwa na uendelevu katika biashara ambayo inajali Mazingira,Nyama pori pamoja na watu.

Mradi wa Utafiti wa Biashara,Maendelo na Mazingira (TRADE Hub)ni mradi wa miaka mitano unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na washirika wengine kutoka katika nchi kumi na tano za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil kuanzia Februari 2019 hadi Machi 2024.


Mratibu wa Utafiti na Machapisho (SUA) ambaye pia ni mtafiti kwenye mradi huo Prof. Japhet Kashaigili akieleza malengo ya Warsha hiyo na kazi ambazo mradi huo umefanya hadi sasa.
Mkuu wa mradi wa TRADE HUB, Prof. Reuben Kadigi akitoa neno la ukaribisho kwa Wadau hao kutoka nchi nzima kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo.
Dkt. Charles Malaki akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi na wadau.
Picha ya pamoja ya washiriki wa warsha hiyo kutoka SUA na Mikoa mbalimbali ambao ni wadau wa Mazao ya Soya, Kahawa, Mpunga, Parachichi na wawakilishi wa Halmashauri na Makampuni yaliyo kwenye mnyororo wa thamani ya mazao hayo.
Wadau wa Mradi wa TRADE HUB wakifuatilia mawasilisho ya matokeo ya tafiti mbali mbali zilizofanywa kwenye mzao ya Soya, Kahawa,Parachichi,Miwa na Nyama Pori.
Mkutano ukiendelea.
Wadau wakiwa kwenye mkutano huo.
Wadau wa Mradi wa TRADE HUB wakifuatilia mawasilisho ya matokeo ya tafiti mbali mbali zilizofanywa kwenye mzao ya Soya, Kahawa,Parachichi,Miwa na Nyama Pori.
Wadau wa Mradi wa TRADE HUB wakifuatilia mawasilisho ya matokeo ya tafiti mbali mbali zilizofanywa kwenye mzao ya Soya, Kahawa, Parachichi, Miwa na Nyama Pori.
Mkutano ukiendelea.