Dar es Salaam. Taasisi isiyo ya kiserikali ya RAOMA Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania Plc wamezindua mfumo mpya wa kidijitali wa elimu unaoitwa SOMO, chini ya kampeni ya Twende Zetu Darasani, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa elimu bora kupitia teknolojia.
Mfumo huo umeundwa mahususi kusaidia ufundishaji na ujifunzaji wa masomo yote kwa kuzingatia mtaala wa taifa, huku ukimwezesha mwalimu kufundisha wanafunzi waliopo maeneo mbalimbali nchini kwa wakati mmoja. Lengo ni kuunganisha shule, walimu na wanafunzi kwa kutumia zana za kidijitali ili kuongeza ubora wa elimu na kuifanya ipatikane kwa usawa.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri wa Elimu, Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Ladslaus Mnyone, alisema matumizi ya teknolojia katika elimu ni msingi muhimu wa kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
Alisema kuwa kupitia mifumo ya kidijitali, taifa linaongeza fursa za elimu, linaimarisha ubora wake na kuwaandaa wanafunzi kuwa na stadi zitakazochochea uchumi wa baadaye. Pia aliwapongeza wadau waliohusika katika ubunifu huo akisema ni hatua kubwa ya mapinduzi ya elimu nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa RAOMA Foundation, Rahma Abdallah, alisema ushirikiano wao na Vodacom unalenga kuhakikisha teknolojia inasaidia kutimiza ndoto za wanafunzi na kuboresha mazingira ya ujifunzaji.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi ili mfumo huo ufike katika shule nyingi zaidi na kuchochea elimu jumuishi.
Naye Mkuu wa Bidhaa za Biashara na Suluhisho kutoka Vodacom Tanzania, Ali Z. Ali, alisema ubunifu wa SOMO ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo kuiwezesha Tanzania kuingia kikamilifu katika ulimwengu wa kidijitali.
Alieleza kuwa mfumo huo utamwezesha mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wengi katika shule tofauti bila kulazimika kuwepo darasani, jambo litakalosaidia kupunguza changamoto za upungufu wa walimu na kuongeza ubora wa ufundishaji.
Uzinduzi wa mfumo wa SOMO unatazamwa kuwa hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea elimu ya kisasa, jumuishi na inayotumia teknolojia, huku ukilenga kuandaa kizazi chenye ujuzi wa kidijitali na uwezo wa kushindana kimataifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: