
Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Madini imezidi kuonesha dhamira yake ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji wa kimkakati barani Afrika, baada ya kukaribisha rasmi kampuni kutoka Korea Kusini kuja kuwekeza katika sekta ya madini nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amesema uwekezaji huo unahitajika zaidi katika maeneo ya utafiti wa madini, uongezaji thamani, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchimbaji na uchakataji wa madini, hususan madini muhimu na ya kimkakati.
Mbibo ametoa kauli hiyo Januari 28, 2026 jijini Dodoma, wakati wa kikao kati ya Wizara ya Madini na ujumbe kutoka Korea Kusini uliowakilisha Shirika la Kukuza Biashara na Uwekezaji la Korea (KOTRA) pamoja na Kampuni ya HD Construction Equipment, inayojihusisha na utengenezaji wa mitambo na teknolojia za uchimbaji madini.
Amesema maboresho ya sera na sheria yaliyofanywa na Serikali yamelenga kuvutia wawekezaji wenye mtaji, teknolojia na nia ya kuwekeza kwa muda mrefu, hasa katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata madini ndani ya nchi na uhamishaji wa teknolojia kwa Watanzania.
“Tanzania iko tayari kwa ubia wa kimkakati unaoongeza ajira, mapato ya ndani na ushindani wa kimataifa. Tunakaribisha wawekezaji wanaoleta suluhisho za kisasa kwenye mnyororo mzima wa thamani wa madini, kuanzia utafiti hadi uongezaji thamani ndani ya nchi,” amesema Mbibo.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi na Kamishna wa Biashara wa KOTRA Ofisi ya Dar es Salaam, Kim Sangwoo, amesema Korea Kusini ina dhamira ya kuongeza uwekezaji wake katika Ukanda wa Afrika Mashariki kupitia miradi yenye tija na uwajibikaji, huku Tanzania ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye mazingira rafiki ya uwekezaji.
Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya HD Construction Equipment, Soohong Min, amesema kampuni za Korea zina uzoefu mkubwa katika teknolojia za kisasa za uchimbaji, mitambo mizito, pamoja na mifumo bora ya uzalishaji, ambayo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ajenda ya Tanzania ya uongezaji thamani wa madini.
● Majadiliano kati ya pande hizo mbili yalihusisha maeneo muhimu kama:
● Utafiti wa kina wa madini kwa kutumia teknolojia za kisasa
● Uchakataji na uongezaji thamani wa madini
● Ujenzi wa viwanda na miundombinu ya uzalishaji
● Uhamishaji wa teknolojia kwa wataalamu wa ndani
Kwa pamoja, pande zote zimeonesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiteknolojia, huku Serikali ikisisitiza kuwa mlango uko wazi kwa wawekezaji wanaoendana na dira ya maendeleo jumuishi na endelevu ya Taifa.
KOTRA ni taasisi ya Serikali ya Korea Kusini iliyoanzishwa mwaka 1962 kwa lengo la kukuza biashara ya kimataifa na uwekezaji wa kigeni, na ina ofisi katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania kupitia ofisi yake ya Dar es Salaam.









Toa Maoni Yako:
0 comments: