Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe limekanusha vikali taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa askari wa polisi mkoani humo alichomwa moto na kuporwa silaha, likizitaja taarifa hizo kuwa za uongo, za kupotosha na zisizo na ukweli wowote.
Akizungumza na vyombo vya habari Januari 28, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mahamoud Banga, amesema hakuna tukio la aina hiyo lililotokea katika mkoa huo na kwamba taarifa zinazosambazwa ni za uzushi mtupu.
“Tunakanusha kuwepo kwa tukio hilo. Hakuna askari aliyekumbwa na tukio la kuchomwa moto wala kuporwa silaha mkoani Njombe. Taarifa hizi ni za uongo na zinapotosha jamii,” amesema ACP Banga.
Kamanda huyo ameonya kuwa watu wanaojihusisha na kutengeneza, kusambaza au kushiriki kusambaza taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii wanakiuka sheria za nchi na maadili ya jamii, na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wanaoandaa na kusambaza taarifa za uongo kuacha mara moja tabia hiyo, kwani ni kinyume cha sheria na haina manufaa yoyote kwao, familia zao wala kwa jamii kwa ujumla,” ameongeza.
Aidha, Polisi wameeleza kuwa wanaendelea kuwafuatilia watu waliotumia picha mjongeo (video) ya tukio la zamani lililohusisha askari waliokuwa wakitoa msaada kwa wananchi, na kuliwasilisha kama tukio jipya kwa lengo la kupotosha umma.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe pia limehakikishia wananchi kuwa linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda usalama wa raia na mali zao kwa kushirikiana na wananchi kupitia programu ya Polisi Jamii, sambamba na kufanya doria, misako na operesheni mbalimbali katika maeneo tofauti ya mkoa huo.
Mwisho, Polisi wamewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola na kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo rasmi kabla ya kuzisambaza.



Toa Maoni Yako:
0 comments: