Na Mwandishi Wetu – Dodoma

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua rasmi mfumo mpya wa huduma kwa wateja unaotumia teknolojia ya akili unde (Artificial Intelligence) ujulikanao kwa jina la BWANABOOM, unaolenga kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa wadau wa elimu nchini kwa saa 24 kila siku.

Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika leo Januari 28, 2026 katika ofisi za Makao Makuu ya HESLB jijini Dodoma, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa sekta ya elimu.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), Profesa Daniel Mushi, ambaye ameipongeza HESLB kwa kuendelea kuwa kinara katika matumizi ya teknolojia za kisasa kuboresha huduma kwa wananchi.

“Leo tunaongeza huduma ya akili unde ‘BWANABOOM’ kama njia nyingine muhimu ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wadau wa elimu. Hili ni jambo la kujivunia na linapaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini,” amesema Prof. Mushi.

Amesema mfumo huo ni hatua muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali kwenye sekta ya elimu, na kusisitiza umuhimu wa HESLB kuendelea kuuboresha ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Aidha, Prof. Mushi ametoa wito kwa HESLB kuzingatia kwa makini masuala ya usalama wa taarifa binafsi za watumiaji, kupima kiwango cha kuridhika kwa wateja mara kwa mara, pamoja na kuangalia uwezekano wa kuanzisha huduma za lugha ya ishara kidijitali ili kuwahudumia wadau wenye ulemavu wa kusikia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema BWANABOOM ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa taasisi hiyo wa kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi wa upatikanaji wa huduma kwa wanafunzi na wadau wengine wa elimu.

“Tunataka kuhakikisha huduma za HESLB zinawafikia wadau kwa urahisi zaidi, kwa wakati na kwa gharama nafuu kupitia majukwaa ya kidijitali,” amesema Dkt. Kiwia.

Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bi. Jaqueline Humbaro, amepongeza ubunifu huo na kuahidi kuwa balozi wa mfumo huo miongoni mwa wanafunzi ili wahakikishe wanatumia ipasavyo fursa hiyo mpya.

BWANABOOM unapatikana kupitia tovuti rasmi ya HESLB (www.heslb.go.tz) na pia ndani ya akaunti za wanafunzi kwenye mfumo wa SIPA, na unatarajiwa kupunguza gharama za usafiri, kuokoa muda, na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Uzinduzi wa mfumo huo unaonesha dhamira ya dhati ya HESLB katika kutumia teknolojia ya akili unde kama nyenzo ya kuleta mageuzi chanya katika maendeleo ya elimu nchini.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: