
Na Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam, Machi 8, 2015 – Serengeti Breweries Limited (SBL) imetambuliwa katika tuzo maarufu za Rising Woman, zilizoandaliwa na Mwananchi Communications Limited, kwa mchango wake mkubwa katika kukuza usawa wa kijinsia na ujumuishi. Tuzo hii inathibitisha dhamira ya SBL ya kujenga mazingira ya kazi yanayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika ngazi mbalimbali ndani na nje ya shirika.
"Kutambuliwa kwa SBL katika tuzo za Rising Woman ni ushuhuda wa juhudi zetu zinazoendelea za kusimamia usawa wa kijinsia. Tunaamini kuwa na nguvu kazi yenye mchanganyiko wa kijinsia na ujumuishi ni msingi wa ubunifu, ukuaji, na mafanikio ya muda mrefu. Tutaendelea kujenga mazingira jumuishi yanayowawezesha wanawake kuongoza na kung'ara," alisema Elizabeth Muro, Mkurugenzi wa Sheria na Uadilifu wa Biashara wa SBL.

SBL imeweka ujumuishi na utofauti kama kiashiria kikuu cha utendaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa ukuaji wa kuwa kampuni inayoaminika na kuheshimika zaidi nchini Tanzania. Ili kuhakikisha usawa wa kijinsia, kampuni imeanzisha sera madhubuti ya ajira inayohitaji kwamba zaidi ya asilimia 60 ya waajiriwa wapya wawe wanawake. Vilevile, wasimamizi wa ajira wanahimizwa kuorodhesha waombaji wa kike kwenye usaili, kuwapa kipaumbele wanawake wenye ujuzi sawa na wanaume, na kuhakikisha nafasi za wanawake waliostaafu au kuondoka zinajazwa na wanawake wengine.
Zaidi ya mchakato wa kuajiri, SBL inaendeleza vipaji vya wanawake kwa utaratibu maalum wa ulezi wa vipaji (mentorship), maendeleo ya uongozi, na mafunzo ya kimataifa. Mradi wa kampuni ujulikanao kama Project BLOOM, ulioanzishwa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Strathmore, unawaandaa wafanyakazi wa kike wenye uwezo mkubwa kwa nafasi za juu za uongozi barani Afrika. Zaidi ya hayo, Mpango wa Uongozi wa Baadaye wa SBL kwa wahitimu wa biashara unajivunia kuwa na ushiriki wa wanawake kwa asilimia 100 nchini Tanzania, kuhakikisha upatikanaji wa kizazi kipya cha viongozi wa kike wa siku zijazo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: