Katika kuendeleza hamasa ya matumizi ya kadi kwa wateja wake na Watanzania kwa ujumla, Benki ya CRDB imepanga kumzawadia mteja atakayekuwa na matumizi makubwa ya kazi zake za TemboCard Visa gari jipya aina ya Ford Ranger.
Sambamba na gari hilo jipya ambalo halijawahi kuendeshwa (kilomita sifuri), Benki ya CRDB pia imezindua kadi za mkopo za TemboCard credit card ili kuwawezesha wateja wake kukamilisha miamala yao hata katika kipindi ambacho hawana fedha za kutosha kwenye akaunti zao.
Akizungumzia kampeni ya kuhamasisha matumizi ya kadi inayoitwa TemboCard ni Shwaa, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema itadumu mpaka Juni ili kuwapa wateja wengi fursa ya kujishindia zawadi tofauti ikiwamo kubwa ya gari jipya.
Raballa amesema kampeni hiyo itatoa jumla ya washindi 30 wakiwamo 24 watakaopata fursa ya kutembelea Mbuga ya Serengeti, watano wataofanya ziara barani Ulaya na mmoja atakayeondoka na Ford Ranger jipya ili kumrahisishia shughuli za usafiri kukamilisha mizunguko yake popote alipo nchini.
“Azma ya Benki ya CRDB siku zote ni kuhakikisha inatoa huduma shindani zinazokidhi mahitaji halisi ya wateja wetu. Tunaamini huduma bora na za kisasa ni muhimu kwa maendeleo ya wateja wetu na Taifa kwa ujumla. Tukishirikiana na wabia wetu Visa International, tumejielekeza katika kurahisisha malipo popote pale duniani,” amesema Raballa akisisitiza kwamba:“Kwa kuzingatia ubora wa huduma, uharaka wa malipo hasa teknolojia ya kugusisha kadi, kampeni yetu imepewa jina la ‘TemboCard ni Shwaaa.’”
Kampeni hii inawahusu wateja wote waliopo na wale wapya watakaojiunga na Benki ya CRDB wakitumia kadi yoyote ile iwe ni TemboCard Gold na Platinum kwa ajili ya wateja wetu wa hadhi ya juu, TemboCard Infinite ambayo ni ya kifahari na ya muundo wa chuma (metal card), au kadi ya wateja wadogo yaani TemboCard Classic Debit.
Akieleza kuhusu ushirikiano wa Benki ya CRDB na kampuni ya Visa International, amesema ni wa kimkakati ukilenga kufungua fursa kwa Watanzania hasa wanaofanya biashara za kimataifa, wanaotalii katika mataifa mengine na wanaoenda kusoma au wanaofanya safari za kiofisi nje ya nchi.
“Ripoti ya karibuni ya Visa International inaonyesha duniani kote sasa hivi kuna watoa huduma za malipo zaidi ya milioni 130 ambao wanatumia mfumo wa malipo wa kadi za Visa. Hivyo Mtanzania mwenye kadi ya TemboCard Visa anao wigo mpana wa kupata huduma mahali popote atakapokuwepo duniani,” amesema Raballa.
Ili kuongeza wigo wa matumizi ya kadi, Benki ya CRDB imezindua kadi za TemboCard Credit ambazo ni maalumu kwa ajili ya kupata mkopo utakaoingizwa kwenye kadi hizo kulingana na sifa za mteja husika pamoja na kutambulisha kadi zake za TemboCard Prepaid ambayo inamruhusu mteja kukamilisha miamala yake bila kuihusisha akaunti yake ya benki.
“Kwa mteja binafsi atakayepata kadi ya TemboCard Credit, ataweza kupata mkopo wa kuanzia shilingi 500,000 na kampuni inafika shilingi milioni 500. Iwapo deni hilo litalipwa ndani ya siku 50 basi hakutokuwa na riba kabisa,” amesema Raballa.
Kuhusu kadi za TemboCard Prepaid, amesema zinafanya kazi kama chombo cha malipo kinachojitegemea zikimuwezesha mteja kufanya malipo bila kuigusa akaunti yake ya akiba.
“Kadi hii imetolewa mahususi ili isaidie kupanga bajeti kwani inakuruhusu kutumia tu kiasi ulichoweka. Kipengele hiki ni muhimu sana kwa watu wanaosimamia matumizi ya kila mwezi au wazazi wanaowapa watoto wao hela ya matumizi shuleni au mahali pengine popote. Wateja wataweza kuweka pesa kwenye kadi hata kupitia mitandao ya simu,” amefafanua Raballa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: