Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Lutambi akizungumza kabla ya kuzindua Mradi wa Afya ya Macho kwa Watoto unaojulikana kama ‘Mtoto Angaza.’ Mradi huo unaoratibiwa na Shirika la Sight Savers chini ya Ufadhili wa USAID unatarajia kuwafikia watoto wenye matatizo mbalimbali ya macho katika wilaya nne mkoani hapa-wapatao 150,000, sambamba na kuendesha huduma za upasuaji zitokanazo na maradhi ya afya ya macho kwa watoto wapatao 100,000 ndani ya kipindi cha mradi 2021-2023
Katibu
Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Lutambi akikata utepe kuzindua rasmi utekelezaji
wa andiko la mradi wa ‘Mtoto Angaza.’ Kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la
Sight Savers, Godwin Kabalika.
Mganga Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt .Victorina Ludovick akizungumza kwenye tukio la uzinduzi
huo.
Mratibu wa
Macho Mkoa wa Singida, Dkt. Upendo Mwakabalile akieleza namna walivyojipanga
kufikia walengwa waliokusudiwa ndani ya kipindi chote cha mradi.
Mratibu wa
Huduma za Macho kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Charles Kalidushi,
akizungumza kwenye tukio la uzinduzi huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt .Angelina Lutambi akimkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi, Justice Kijazi nakala ya andiko la mradi huo kwa utekelezaji. Wilaya nyingine zilizopokea nakala hiyo ni Manyoni, Iramba na Singida DC.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WATOTO wapatao 150,000 mkoani hapa wanatarajia kufikiwa na Mradi wa Afya ya Macho kwa Watoto ujulikanao kama ‘Mtoto Angaza,’ huku kati yao idadi ya takribani watoto 100,000 watafanyiwa huduma za upasuaji unaotokana na maradhi mbalimbali ya afya ya macho katika kipindi chote cha mradi kuanzia 2021 hadi 2023.
Akizindua mradi huo jana, Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt Angelina Lutambi, mbali ya kupongeza ujio wake, pia aliwataka watendaji wote wanao husika katika utekelezaji wa mradi husika kujitoa kikamilifu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake, ili kuufanya mradi huo kuwaendelevu na wenyetija.
“Nawashukuru sana Shirika la Sight Savers kwa kutushika mkono kupitia mradi huu wa Mtoto Angaza ambao mnauratibu chini ya ufadhili wa USAID, niwasihi watendaji wote tuupe kipaumbele ili uwe na matokeo chanya,” alisema.
Hata hivyo, alihimiza elimu juu ya masuala yote yahusuyo lishe bora yazingatiwe katika kipindi chote cha mradi ili kuimarisha afya ya macho na kuzuia kabisa tatizo la uoni hafifu.
Pia Lutambi alimwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kuweka utaratibu mzuri wa Mpango Kazi utakaoleta ufanisi katika utekelezaji wa shughuli zote zilizopangwa kufanyika ndani ya kipindi cha mradi, ili kuufanya kuwa mradi endelevu, sambamba na kuhakikisha watendaji wa mkoa wananufaika na fursa ya mafundisho yatakayotolewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Sight Savers, Godwin Kabalika, alisema mradi huo umelenga kuboresha utoaji wa huduma ya Afya ya Macho kwa watoto wenye umri wa kuanzia mwaka 0 hadi 16 mkoani hapa ndani ya Wilaya 4 za Iramba, Manyoni, Ikungi na SingidaVijijini.
Aliongeza kuwa mradi huo utakaogharimu Dola za Kimarekani 350,000 utatekelezwa kwa kuhusisha ushiriki wa jopo la wataalamu kutoka Hospitali yaTaifa ya Muhimbili ambao watakuwa na jukumu la kushirikiana na wataalamu wenyeji kwenye utoaji wa huduma mbalimbali, zikiwemo za upasuaji na utoaji ujuzi wa kitaalamu kwenye eneo la macho.
“Lengo kubwa ni kuboresha huduma za macho ndani ya mkoa wa Singida. Na kupitia mradi huu wa miaka miwili tunatarajia kuwafikia watoto laki moja na nusu, na kati yao watoto wapatao laki moja watafanyiwa huduma za upasuaji,” alisema Kabalika.
Daktari Bingwa na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Macho kutoka Hospitali yaTaifa Muhimbili, Dkt Paul Nyaluke, alibainisha ushiriki wao katika mradi huo kuwa pamoja na mambo mengine, Muhimbili watashiriki kwenye eneo la kitaalamu kwa watoto watakao onekana wanamahitaji ya kufanyiwa upasuaji.
Aidha, Nyaluke alisema pia watajikita katika kuratibu usimamizi wa majukwaa yote yatakayo pangwa, huku akisisitiza kwamba kwenye eneo nyeti la upasuaji-hospitali hiyo itakuja na jopo la wataalamu mbalimbali kwa mfululizo wa ziara zisizopungua sita katika kipindi chote cha mradi.
Hata hivyo, akielezea ukubwa wa tatizo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Victorina Ludovick, alisema tatizo la macho kwa mkoa limefikia asilimia 2.8 huku wilaya ya Iramba ikionyesha kuwa na changamoto kubwa zaidi ikilinganishwa na wilaya nyingine.
Alisema serikali kwa kushirikiana na Sight Savers wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo la uoni unaozuilika na lile la uonihafifu-hasa eneo la changamotoya ‘Mtoto wa Jicho’ ambapo zaidi ya wananchi 3000 wamefikiwa na kupatiwa matibabu.
Kitaalamu, imeelezwa walengwa hasa watakaofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya uoni hafifu ambao hutokana na sababu kadhaa, ikiwemo mtoto wa jicho. Tatizo hili ni matokeo ya lenzi ambazo zipo ndani ya macho kupata ukungu na hivyo kutoruhusu mwanga kupita na kuingia eneo la ndani la macho.
Pia kundi lingine litakalotazamwa kwa upekee ni watoto wenye changamoto ya uonihafifu ‘Low Vision’ ambao hata wanapopewa miwani huwa haiwasaidii kutokana na kukumbwa na tatizo la kuwa na kovu sehemu ya kuonea ambayo inapatikana sehemu ya nyuma ya jicho.
Kundi hili litapatiwa vifaa maalumu vya kuwasaidia kuona ‘Visual Aids.’
“Hivyo mradi huu umelenga kuwaibua huko walipo ili waweze kupatiwa huduma za kitiba dhidi ya tatizo la uoni hafifu unaozuilika kwa lengo la kurekebisha uoni wao,” alisema Dkt. Ludovick.
Toa Maoni Yako:
0 comments: