Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akikata Utepe kuzindua Maadhimisho ya Wiki ya Chanjo kimkoa kwenye viwanja vya Kata ya Muhintiri, Tarafa ya Ihanja, Wilaya ya Ikungi hivi karibuni. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Edward Mpogolo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amewataka Wataalamu wa Afya mkoani hapa kuchanganua na kuainisha hadharani ni kwa namna gani chanjo zinazotolewa zimekuwa na tija kwa jamii ili kuleta msukumo kwa watu kuzipenda, kuzithamini, kuziheshimu na kuendelea kuchanjwa.

Akizindua ‘Wiki ya Chanjo’ kimkoa, kwenye viwanja vya Kata ya Muhintiri, Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana, Nchimbi pamoja na mambo mengine, aliwataka wataalamu hao kufuatilia na kutangaza hadharani matokeo na mazao ya chanjo hizo katika uhalisia wa maisha ili watu wajue.

“Wataalamu msikae kimya tuelezeni mara kwa mara manufaa ya hizi chanjo ni kwa namna gani zimekuwa chanzo cha afya bora na akili timamu kwa ukuaji stahiki wa watoto wetu, vijana, jamii na taifa…tuelezeni zinavyochangia ongezeko la ufaulu mashuleni na manufaa yake kwa ukuaji wa uchumi,”alisema Nchimbi na kuongeza;

“Mkieleza vizuri ubora wa chanjo hizi kwa jamii na tukawaelewa-basi- ubora huo ndio utakuwa msukumo katika kuchochea zaidi kasi ya ongezeko la watumiaji wake.”

Hata hivyo alisisitiza haitakuwa na maana yoyote kama chanjo zinazotolewa hazitaenda sambamba na lishe bora, huku akitumia nafasi hiyo kuhamasisha jamii kuzingatia vyote kwa pamoja, ili kuleta ustawi wa afya ya jamii kwa matokeo ya Taifa bora.

Nchimbi alisema Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha juhudi zilizopo za utoaji wa chanjo zinakwenda sambamba na maboresho katika utoaji wa huduma nyingine za afya-ili kupunguza vifo visivyo vya lazima na kumlinda kila mtanzania dhidi ya maradhi ambukizi.
      
Katika hilo, aliwahimiza wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata dozi nzima ya chanjo zinazotolewa kwenye Vituo vya Afya, kwa kuzingatia chanjo ni chanzo cha afya bora na kinga madhubuti dhidi ya magonjwa hatarishi.

Awali, akiwasilisha taarifa ya mkoa juu ya hali halisi ya utoaji wa huduma za chanjo kwa mwaka 2020, Kaimu Mganga Mkuu mkoani hapa, Ernest Mgeta alisema licha ya mafanikio katika utoaji wa huduma hiyo lakini bado kuna changamoto, ikiwemo ya wengi kutokamilisha dozi.

Mgeta alibainisha kuwa idadi kubwa ya watumiaji wa chanjo huanza vizuri lakini hawakamilishi chanjo. Mathalani katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2020, jumla ya akinamama 8,646 hawakupata au kukamilisha chanjo dhidi ya ugonjwa wa Pepopunda.

Ugonjwa huo ni rahisi kumpata mtoto atakayezaliwa kupitia mama ambaye hana kinga yake, na maambukizi hutokea ndani ya siku 28 tangu kuzaliwa kupitia kovu la kitovuni. Watoto wote ambao hupata vimelea vya Pepopunda huishia kufariki.

Mgeta alitaja changamoto nyingine kuwa ni kasumba hatarishi ya wazazi kuendelea kujifungulia nyumbani ambayo hupelekea watoto kukosa huduma za afya za awali, ikiwa ni pamoja na kupata chanjo dhidi ya Kifua Kikuu na Polio.

Suala lingine lililojitokeza ni watoto kusitishwa kuhudhuria kliniki mapema na kushindwa kukamilisha dozi ya mwisho ya chanjo dhidi ya Surua, mathalani, katika kipindi cha mwaka jana jumla ya watoto 18,583 hawakufika kukamilisha dozi ya pili ya Surua-hali inayoleta tishio la mlipuko wa ugonjwa huo miongoni mwa jamii ya wana-Singida.

Akizungumzia kinga dhidi ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa wanawake hususani kwa wasichana wenye umri wa miaka 14, Kaimu Mganga Mkuu alisema serikali tayari ina chanjo ya kuzuia ugonjwa huo unaosababisha kifo iliyoanza kutolewa tangu mwaka 2018, lakini hata hivyo bado mwitikio ni mdogo.

“Chanjo hii licha ya Serikali kuinunua kwa gharama kubwa lakini huduma zake kwa wananchi hutolewa bure kupitia vituo vyake vyote vya afya...hakuna malipo yoyote,” alisema Mgeta.

Hata hivyo, aliwahamasisha wazazi kujitokeza kuwapeleka watoto kwenye vituo vya afya, hususani wiki hii ya maadhimisho ya chanjo ili kuhakikisha zingatio la mahitaji ya kidozi linafikiwa kwa matokeo chanya ya kiafya, sambamba na kuepuka maradhi na vifo.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu yanasema “Chanjo Hutuweka Huru Pamoja, Kapate Chanjo” ikiwa na maana ya kama tutazingatia ipasavyo upatikanaji wa huduma hiyo basi ni dhahiri itatuweka huru bila ya kuwa na wasiwasi wa kuambukizana magonjwa.

Imeelezwa, kwa aliyechanja akakamilisha dozi yupo huru kutopata magonjwa ambayo yanasababishwa na milipuko na ambayo yanakingwa kwa chanjo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: