Na Mwandishi Wetu, Kihonda
RAIS wa New Covenant Unity International (NCUI) ambaye pia ni Kiongozi wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala amefanya maombi maalum ya kumshukuru Mungu kwa kuwaepusha Watanzania na janga la kimbunga jopo ambacho kama kingepiga hapa nchini kingesababisha madhara mbalimbali katika jamii.
Maombi hayo yamefanyika Machi 2, 2021 kwa nyakati tofauti katika makao makuu ya Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yaliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro.
Nabii Dkt.Joshua amesema kuwa, Watanzania wana kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuendelea kuwaepusha na majanga mbalimbali vikiwemo vimbunga na milipuko ya magonjwa ambayo yamekuwa yakitikisa Dunia.
Maombi hayo yamefanyika baada ya mwishoni mwa mwezi uliopita Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuelezea kuwa, kimbunga Jopo ambacho kilitarajiwa kupiga maeneo ya Kusini na Pwani ya nchi yetu kilipoteza nguvu.
Taarifa ya kimbunga hafifu Jobo iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Aprili 24, 2021ilionyesha kimbunga hicho kilipoteza nguvu yake wakati kikiingia nchi kavu Kusini mwa mkoa wa Pwani na Dar es Salaam usiku wa siku hiyo.
Hali ambayo ilisababishwa na kuendelea kuimarika kwa upepo kinzani katika mwelekeo wa kimbunga hicho hadi kutoweka kabisa bila kuleta changamoto au madhara yoyote nchini.
Nabii Dkt.Joshua amesema, "Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa matendo makuu anayoyafanya kwa Taifa letu na watu wake. Huu ni upendo wa kipekee mno ambao Mungu ametupatia sisi Watanzania, anatupenda, anatujali, anatulinda na anatuokoa wakati wotote. Mungu wetu ni mwingi wa rehema, hivyo tuendelee kumwamini na kumkabidhi maisha yetu na Taifa letu daima na hakika hatatupungukia,"amesema.
Wakati huo huo, Nabii Dkt.Joshua amewataka Watanzania kutambua kuwa, Taifa la Tanzania linahitaji uponyaji kwa maombi ya kila mmoja popote pale alipo ndani na nje ya nchi.
Kupitia Biblia takatifu kitabu cha 1Timotheo 2:16, Nabii Dkt.Joshua amesema kuwa, “Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.
"Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake,” Nabii Dkt.Joshua alinukuu Biblia huku akisema kuwa kuna nguvu ya uponyaji kupitia maombi.
Nabii Dkt.Joshua amesema, moja kati ya balaa ambayo tunaweza kupata kwenye Taifa ni pale kanisa au waumini watakapojisahau kuomba kwa ajili ya Taifa.
Amesema hayo huku akikumbushia kuhusu mwombaji mmoja ambaye ni Nabii Eliya, amesema Nabii huyo pekee yake aliomba mvua isinyeshe juu ya nchi na ikawa hiyo.
Nabii Dkt. Joshua amesema kwa mujibu wa Yakobo 5:17, “Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita,"amenukuu huku akisema kuwa, kama Nabii huyo alikuwa mwanadamu kama sisi, basi kanisa linawajibu wa kufanya kutawala anga la nchi na ardhi na watu wake kwa njia ya maombi na Mungu ataendelea kutupigania.
Amesema, tuna wajibu mkubwa wa kuliombea Taifa ikiwemo kusimama kuomba rehema juu ya viongozi wetu ambao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na viongozi wote wanaowasaidia marais hao kuongoza Taifa.
"Tuombe rehema kwa ajili ya watu wote. Tuombe rehema kwa ajili ya viongozi wetu na tusimame katika zamu zetu kwa uaminifu kuliombea Taifa letu, Mungu anatupenda, hivyo kama anatupenda tusikubali kumpa nafasi shetani ajifanyie mambo yake katika Taifa letu,"amesema Nabii Dkt.Joshua.
Toa Maoni Yako:
0 comments: