Shirika la Mikono Yetu ambalo limejikiza kuwawezesha wasichana kielimu na kiuchumi limetambulisha rasmi mradi wake wa "Msichana Ni Tai" kwa lengo la kuwajengea uwezo wasichana kutimiza ndoto zao.
Akizungumza kwenye utambulishoi wa mradi huo, Mkurugenzi wa Shirika hilo, Maimuna Kanyamala alisema jumla ya wasichana 300 kutoka Kata ya Buswelu wilayani Ilemela watajengewa uwezo kupitia simulizi za wanawake waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo siasa na uongozi.
Alisema baada ya wasichana hao pamoja na wazazi wao kujengewa uwezo, watakuwa chachu ya mabadiliko kwa wasichana wengine na hivyo kuleta mabadiliko katika jamii tofauti na ilivyo sasa ambapo wasichana wanapitia changamoto kadhaa za usawa katika kutimiza ndoto zao ikilinganishwa na wavulana.
"Dhana ya Msichana ni Tai inatokana na moja ya hotuba za Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere aliyewahi kusema "mwanamke ni tai, si kuku" akimaanisha wanawake wana uwezo mkubwa wa kutimiza malengo yao kama tai anavyoweza kupaa umbali mrefu na si kuku ambaye anafugwa ndani akisubiri kuletewa chakula" alibainisha Afisa Mradi kutoka Shirika la Mikono Yetu, Halima Juma.
Kwa sasa mradi wa "Msichana Ni Tai" unawashirika wasichana 300 walio nje ya shule pamoja na wazazi wao katika Kata ya Buswelu wilayani Ilemela ukitarajiwa kudumu kwa muda wa miaka mitatu baada ya mradi wa majaribio uliozinduliwa mwaka 2018 kufanikiwa.
Tazama video hapa chini
SOMA>>> Habari zinazohusiana
Toa Maoni Yako:
0 comments: