Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakifunua pazia kama ishara ya ufunguzi rasmi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Alhamisi Agosti 1, 2019.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amezindua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jengo la tatu (Terminal 3), jijini Dar es salaam mradi ambao unagharimu zaidi ya Bilioni 720.
Akizumgumza kwenye uzinduzi huo, Rais Magufuli amesema licha ya Serikali yake kutekeleza mradi huo, lakini hadhani kama watakaofuata kwenye nafasi hiyo ya Urais wataweza kuyatimiza anayoyafanya, kwa kile alichokieleza amekuwa akisemwa mara kwa mara.
“Mara nyingi tumeambiwa kuwa Tanzania ni masikini, ninaomba neno hilo tulifute kwani nchi yetu ni tajiri lakini tulitaka kuaminishwa na watu waliotaka kututumia, kuna miradi imetumia matrilioni ya fedha saa nyingine ninajiuliza kweli hili limewezekana, tumeweza maana yake kila palipo na nia Mungu yupo pamoja na sisi,” amesema.
“Siwezi nikasimama mbele za watu nikasema haya ni kwasababu yangu kwani mimi ni dereva tu lakini pia huwa ninajiuliza ikitokea siku Mungu akanichukua hao watakaokuja watayamaliza kweli kwasababu panahitaji moyo, unafanya hivi huku unatukanwa lakini inabidi ufanye kwaajili ya Watanzania, inahitaji kujitoa sadaka ya kweli,” amesema.
“Ninamshukuru Mungu kwa kuendelea kulisimamia taifa hili na ninawashukuru Watanzania wenzangu kwa kuendelea kuniombea na kunipa moyo, nchi yetu sasa imekuwa ya mfano watu wanatuogopa sasa, wapo wanaouliza mnapata wapi fedha mimi ninasema zilikuwa kwa mafisadi sasa zinaenda kwa Watanzania,” amesema.
Toa Maoni Yako:
0 comments: