Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Mponda katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wilayani humo jana ambapo aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda. Kulia kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Khalfan Haule.
Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na baadhi ya wanafunzi katika kijiji cha Mponda Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wilayani humo jana. Aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda. Kulia kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Khalfan Haule.
Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipata ufafanuzi kuhusu upandaji wa miti kutoka kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Zawadi Mbwambo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi katika msitu wa Mbizi wilayani Sumbawanga jana. Aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda.
Na Hamza Temba, Rukwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS kuchangia shilingi milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Ametoa agizo hilo kufuatia taarifa iliyowasilishwa kwake na Mtendaji wa Kata ya Majengo, Matage Bikaniko Mjarifu alipotembelea kijiji hicho kinachopakana na Msitu wa Mbizi ambapo amesema wananchi wa kijiji hicho husafiri umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 11 kwa ajili ya kufuata huduma za afya mjini Sumbawanga.
Amesema mpaka sasa wananchi wa kijiji hicho wameshachangia shilingi laki 9 na Mbunge wa Sumbawanga mjini shlingi milioni 5. Hata hivyo amesema jumla ya shilingi milioni 134 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Kufuatia taarifa hiyo, Waziri Kigwangalla alisema Wizara yake kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS itachangia shilingi Milioni ishirini hivyo wananchi wapambane kwa kushirikiana na halmashauri yao ili jengo hilo lisimame na hatimaye fedha hizo ziwasilishwe kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake.
Alisema Falsafa ya Uhifadhi Endelevu ni Uhifadhi Shirikishi Jamii, hivyo wizara yake itaendelea kusimamia sera ya kuhakikisha wananchi hususan wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi wananufaika moja kwa moja na hifadhi hizo kupitia miradi ya maendeleo.
Dk. Kigwangalla ameziagiza taasisi zote za uhifadhi nchini kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii ili wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hizo waone umuhimu wa hifadhi hizo moja kwa moja na hivyo kutoa ushirikiano kwenye uhifadhi.
Katika hatua nyingine, Waziri Kigwangalla amemsimamisha kazi Meneja wa Pori la Akiba Uwanda, katika wailaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Mark Chuwa kwa tuhuma za kushindwa kuondoa mifugo zaidi ya 12,000 iliyopo ndani ya hifadhi hiyo.
Kabla ya uamuzi huo, akisoma taarifa ya mkoa kwa Waziri huyo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Khalfan Haule alisema uvamizi katika pori hilo umekuwa wa kiasi kikubwa ambapo wafugaji huingia na makundi makubwa ya mifugo na kugeuza eneo hilo sehemu ya malisho.
Alisema licha ya na kufanyika kwa opresheni za mara kwa mara za kuondoa mifugo hiyo, baada ya muda mfupi wafugaji hao hurejea na makundi makubwa ya mifugo kwa ajili ya malisho.
Hata hivyo Dk. Kigwangalla alishangazwa na uongozi wa mkoa na wilaya kwa kushindwa kuchukua hatua za kuondoa mifugo hiyo hifadhini wakati sheria za uhifadhi haziruhusu mifugo hifadhini.
Toa Maoni Yako:
0 comments: