


Ujumbe wa Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassanakiwa kwenye mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya pamoja na Ujumbe wake, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Mei, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya pamoja na Ujumbe wake Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Mei, 2026.
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC pamoja na ujumbe wake, Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi hao walijadili masuala mbalimbali kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto barani Afrika.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kaseya alisema Africa CDC ina dhamira ya kushirikiana na Rais Samia ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, pamoja na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, kwa lengo la kuimarisha huduma za afya katika sekta hiyo muhimu.
Alisema ushirikiano huo unalenga kuongeza juhudi za kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na kuboresha huduma za afya kwa mama na watoto katika nchi mbalimbali za Afrika.
Dkt. Kaseya alieleza kuwa Tanzania imeonyesha mafanikio makubwa katika sekta ya afya, hususan katika upatikanaji wa huduma kwa wananchi, jambo ambalo linaweza kuwa mfano kwa nchi nyingine barani humo.
Alibainisha kuwa asilimia 85 ya wananchi nchini Tanzania wanapata huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano kutoka maeneo wanayoishi, hatua aliyosema inaimarisha ajenda ya Afrika ya usalama wa afya na kujitegemea katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Rais Samia alisema Serikali ya Tanzania ipo tayari kuendelea kushirikiana na Africa CDC katika kuendeleza ajenda ya afya ya mama na mtoto, akisisitiza kuwa utekelezaji wa malengo yaliyowekwa unahitaji mipango madhubuti na uratibu wa karibu.
Aidha, Rais Samia aliiagiza Wizara ya Afya kushirikiana kwa karibu na Africa CDC katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha afya ya uzazi, mama na mtoto nchini na barani Afrika kwa ujumla.




Toa Maoni Yako:
0 comments: