Na Mwandishi Wetu

MKE wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Neema Mwigulu Nchemba, ametoa wito kwa viongozi na wadau mbalimbali barani Afrika kuweka kipaumbele katika ulinzi wa watoto dhidi ya ukatili wa kidijitali unaochochewa na maendeleo ya teknolojia ya Akili Bandia (AI).

Bi. Nchemba ametoa kauli hiyo Mei 12, 2026 jijini Nairobi, Kenya wakati akizungumza katika Mkutano wa Wenza wa Mawaziri Wakuu wa nchi za Afrika, uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa “Africa-Forward Summit” uliolenga kujenga mazingira salama ya kidijitali kwa watoto wa Afrika.

Amesema mustakabali wa bara la Afrika hautategemea tu maendeleo ya kiuchumi, bali pia uwezo wa watoto kujifunza, kushiriki na kuvumbua katika ulimwengu wa kidijitali bila hofu ya unyanyasaji na ukatili wa mtandaoni.

“Teknolojia ya Akili Bandia imefungua fursa kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na ujasiriamali, lakini pia imeibua hatari mpya zinazohitaji hatua za haraka na za pamoja,” amesema Bi. Nchemba.

Ameeleza kuwa baadhi ya changamoto zinazowakabili watoto katika mazingira ya mtandao ni pamoja na uonevu wa mtandaoni, unyanyasaji wa kijinsia unaochochewa na AI pamoja na matukio ya ulaghai yanayoweza kuathiri ustawi na maendeleo yao.

Aidha, Bi. Nchemba amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha ulinzi wa watoto mtandaoni, ikiwemo kufanya marekebisho ya Sheria ya Mtoto (Sura ya 13) na kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.

Pia alikumbusha kuhusu Kampeni ya Kitaifa ya Ulinzi wa Watoto Mtandaoni iliyoanzishwa Februari mwaka 2024 pamoja na kuundwa kwa kamati maalum inayowajumuisha wadau mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha watoto wanakuwa salama katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali.

Mkutano huo uliandaliwa na kuongozwa na Mke wa Rais wa Kenya, Mama Rachel Ruto, na ulihitimishwa kwa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda pamoja na kuwekwa kwa sheria madhubuti zitakazosaidia kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kidijitali dhidi ya watoto barani Afrika.

















Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: