
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro kupitia ukurasa wake wa Facebook, ambapo alimuelezea Amani kama mmoja wa makocha wenye uwezo wa kipekee na usio wa kawaida ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mtatiro alisema alimfahamu Amani miaka kadhaa iliyopita waliposhirikiana katika mradi wa kuipandisha Biashara United Mara hadi Ligi Kuu, kabla ya kuendelea kufanya kazi pamoja katika timu ya Tunduru Korosho FC, ambapo waliiwezesha kutwaa ubingwa wa Regional Champions League na kupanda daraja.
Aidha, alisema Amani aliwahi pia kuinoa Prisons FC na kufanikiwa kuinusuru kushuka daraja katika msimu wa 2024/25, huku akieleza kuwa kocha huyo ana uwezo mkubwa wa kuwajenga vijana na kuwapa nidhamu, morali pamoja na mfumo bora wa ushindani.
Mtatiro alimalizia kwa kusema kuwa hana mshangao kuona Dodoma Jiji ikitoa ushindani mkubwa dhidi ya timu kubwa kama Young Africans SC, akisisitiza kuwa Amani Josiah ni kocha mwenye uwezo wa kubadilisha kabisa kiwango cha timu ndani ya muda mfupi.


Toa Maoni Yako:
0 comments: