Na Mwandishi Wetu.

Morogoro, Aprili 1, 2026 — Serikali imesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta mbalimbali katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Afya Moja, ikilenga kuboresha afya ya binadamu, mifugo na mazingira kwa pamoja.

Akizungumza katika kikao kazi cha tathmini ya mpango huo wa mwaka 2022–2027 kilichofanyika mkoani Morogoro, Mkurugenzi Msaidizi wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Salum Manyatta, alisema mafanikio ya mpango huo yanategemea utekelezaji shirikishi unaojumuisha sekta zote muhimu.

Alieleza kuwa tathmini hiyo inalenga kuangalia kwa kina utekelezaji wa shughuli mbalimbali kuanzia ngazi ya uratibu wa taasisi hadi utekelezaji katika mikoa na serikali za mitaa, ili kubaini mafanikio na maeneo yanayohitaji kuboreshwa.


“Tathmini hii itatusaidia kuandaa mpango mkakati ujao utakaoanza mwaka 2028 kwa kuzingatia uzoefu na changamoto zilizojitokeza,” alisema Dkt. Manyatta.

Kikao hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Afya Moja kwa kushirikiana na CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani.

Kwa upande wake, Mratibu wa Afya Moja na Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Kizoonotiki kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Gwakisa John, alisema sekta ya afya imeendelea kushirikiana na sekta nyingine katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko na yale yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Alitaja magonjwa kama kichaa cha mbwa na kimeta kuwa miongoni mwa yale yanayodhibitiwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya sekta za afya, mifugo na mazingira.

Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa changamoto ikiwemo mifumo ya ubadilishanaji taarifa, akisema juhudi zinaendelea kuunganisha mifumo hiyo ili kuongeza ufanisi wa mawasiliano serikalini.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Afya Moja na Mratibu wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani kutoka CIHEB Tanzania, Dkt. Irene Masawe, alisema washiriki wa kikao hicho wamefanikiwa kupitia maeneo muhimu ya utekelezaji, ikiwemo uratibu, ufuatiliaji na tafiti.

 Kwa upande wake, mjumbe wa Kamati ya Wataalam wa Afya Moja katika eneo la utafiti na maendeleo kutoka Muhimbili University of Health and Allied Sciences, Dkt. Maurice Mbunde, alisema tathmini hiyo imeonesha mafanikio makubwa yaliyotokana na ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo.

Kwa ujumla, kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha mipango ya kimkakati inafanyiwa tathmini ya mara kwa mara ili kuongeza tija, ufanisi na ubora wa huduma za afya pamoja na usimamizi wa majanga nchini.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: