Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam, Aprili 1, 2026 — Exim Bank Tanzania imeingia ubia wa kimkakati na The Voice TZ kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali na kupunguza utegemezi wa fedha taslimu, hasa katika sekta ya burudani na huduma za chakula.

Kupitia ushirikiano huo, wateja wa The Voice TZ sasa wataweza kulipia huduma kwa kutumia kadi za Exim au huduma ya Lipa ChapChap, hatua inayolenga kurahisisha miamala kwa haraka, usalama na uwazi zaidi.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkuu wa Huduma za Wateja Binafsi wa benki hiyo, Andrew Lyimo, alisema ubia huo unalenga kuboresha uzoefu wa wateja, hasa katika kipindi cha msimu wa sikukuu ambapo maeneo ya burudani hupokea idadi kubwa ya watu.

“Wateja wetu sasa wataweza kufurahia huduma bila usumbufu wa kubeba fedha taslimu, huku wakinufaika na malipo ya haraka na salama,” alisema Lyimo.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, wateja watakaotumia kadi za Exim watanufaika na punguzo la asilimia 10 kwenye bili zao, huku malipo yakithibitishwa papo hapo. Endapo kutatokea hitilafu, marejesho yatafanyika mara moja, na risiti zitatolewa kupitia ujumbe mfupi wa simu au nakala ya karatasi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Stanley Kafu, alisema benki inaendelea kumweka mteja katikati ya huduma zake kwa kuleta suluhisho rahisi na za kisasa.

“Tunataka wateja wetu wapate uzoefu wa malipo ya ‘tap and go’, uwazi wa gharama na uaminifu katika kila muamala,” alieleza.

Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Kiufundi wa The Voice TZ, Deogratius Stephen, alisema ushirikiano huo utaongeza ubora wa huduma kwa wateja wao kwa kuwawezesha kufanya malipo kwa haraka na kwa usalama zaidi.

Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Exim Bank Tanzania wa kuendeleza matumizi ya teknolojia katika huduma za kifedha na kukuza uchumi usiotegemea fedha taslimu nchini.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya burudani na biashara, huku ukitoa fursa zaidi kwa Watanzania kutumia malipo ya kidijitali kwa urahisi na ufanisi zaidi.


 

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: