Dar es Salaam, Machi 30, 2026 — Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetoa ufafanuzi rasmi kwa umma kuhusu matumizi ya kamera za usalama (CCTV), ikikanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa kila mtu mwenye kamera hizo anatakiwa kujisajili na Tume.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, imeelezwa kuwa si kweli kwamba kila mtu binafsi mwenye CCTV anapaswa kujisajili. Badala yake, wajibu huo unawahusu taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi, ikiwemo kupitia kamera za CCTV.
PDPC imefafanua kuwa taasisi husika zinatakiwa kujisajili kabla au ifikapo Aprili 8, 2026, kwa mujibu wa matakwa ya sheria, ili kuhakikisha ulinzi wa taarifa binafsi za wananchi unazingatiwa ipasavyo.
Aidha, Tume imeonya kuhusu matumizi ya CCTV katika makazi binafsi, ikisisitiza kuwa kamera hizo zinapaswa kuelekezwa ndani ya mipaka ya eneo la mhusika pekee. Imeelezwa kuwa iwapo kamera zitakusanya taarifa nje ya mipaka hiyo na kufikia maeneo ya umma, matumizi hayo yatakuwa kinyume cha sheria na mhusika atawajibika.
Vilevile, PDPC imehimiza umuhimu wa kuweka alama maalum (signage) zinazoonesha wazi kuwa eneo fulani lipo chini ya uangalizi wa CCTV inayokusanya taarifa binafsi, hatua inayolenga kulinda faragha za watu.
Tume hiyo imeeleza kuwa itaendelea kutoa miongozo na elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia ya CCTV, ili kuhakikisha haki za faragha zinazingatiwa sambamba na mahitaji ya usalama.



Toa Maoni Yako:
0 comments: