Kigali, Rwanda — Waamuzi wa mpira wa miguu kutoka Tanzania wenye beji za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wameendelea kuipeperusha vyema bendera ya nchi katika mashindano ya FIFA Series 2026 yaliyofanyika Kigali, Rwanda, baada ya kuteuliwa kusimamia michezo ya kimataifa.
Waamuzi hao ni Ahmed Arajiga aliyekuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Mohamed Mkono na Respicus Dismas kama waamuzi wasaidizi, huku Nasir Salum akihudumu kama mwamuzi wa akiba. Timu hiyo ya waamuzi ilikuwa miongoni mwa waliochezesha mchezo kati ya Kenya na Grenada katika mashindano hayo.
Mashindano ya FIFA Series 2026 kwa upande wa Kituo ‘A’ yalizikutanisha timu za taifa za Rwanda, Kenya, Grenada na Estonia, yakifanyika katika Uwanja wa Amahoro, jijini Kigali. Ushiriki wa waamuzi hao unathibitisha kiwango chao cha juu na imani waliyopewa na FIFA kusimamia michezo ya kimataifa.
Kwa mujibu wa matokeo ya mashindano hayo, wenyeji Rwanda waliibuka mabingwa wa Kituo ‘A’, wakifuatiwa na Estonia katika nafasi ya pili, huku Kenya wakishika nafasi ya tatu.
Waamuzi hao wanatarajiwa kurejea nchini leo, huku uzoefu walioupata katika mashindano hayo ukitarajiwa kuleta mchango chanya katika kuboresha viwango vya uamuzi ndani ya ligi za ndani na mashindano mengine ya soka nchini Tanzania.




Toa Maoni Yako:
0 comments: