Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Januari 31, 2026 amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ziara rasmi inayolenga kuendeleza juhudi za Serikali katika kukuza uhifadhi na utalii nchini.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mwigulu anatarajiwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Kitaifa za Uhifadhi na Utalii maarufu kama The Serengeti Awards, tuzo zinazotolewa kwa wadau waliotoa mchango mkubwa katika kulinda maliasili na kukuza utalii.

Mbali na kushiriki katika hafla hiyo, Waziri Mkuu pia anatarajiwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha, ziara itakayolenga kujionea hali ya uhifadhi na shughuli za utalii, pamoja na kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Rais Dkt. Samia katika kuitangaza Tanzania kimataifa kama kitovu cha utalii barani Afrika.

Tuzo za Serengeti ni miongoni mwa tuzo muhimu zinazotambua mchango wa taasisi, mashirika, sekta binafsi na watu binafsi katika kuhifadhi mazingira, wanyamapori na vivutio vya utalii, huku Serikali ikiendelea kusisitiza ushirikiano wa wadau wote katika kulinda rasilimali za taifa.

Ziara ya Waziri Mkuu inadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha sekta ya utalii kama nguzo muhimu ya uchumi, ajira na maendeleo endelevu kwa Watanzania.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: