Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) leo Januari 31, 2026 jijini Dar es Salaam limetangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne uliofanyika Novemba 17, 2025, yakionyesha kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kwa asilimia 2.61 na kufikia asilimia 94.98, hatua inayodhihirisha maboresho katika sekta ya elimu ya sekondari nchini.

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, amesema jumla ya watahiniwa 595,810 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 318,910 sawa na asilimia 53.53 na wavulana 276,900 sawa na asilimia 46.47. Kati yao, watahiniwa 526,620 wamefaulu kwa kupata daraja la I, II, III na IV.

Profesa Mohamed amesema ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu umeongezeka na kufikia jumla ya wanafunzi 255,404 sawa na asilimia 46.1 ya watahiniwa wote waliopata matokeo, hali inayoonesha kuimarika kwa ubora wa ufaulu ukilinganisha na mwaka uliopita.

Ameeleza kuwa jumla ya wanafunzi 569,883 walifanya mtihani huo wakiwa wamesajiliwa katika shule 5,864 nchini kote, huku watahiniwa wa kujitegemea wakiwa 25,927 waliosajiliwa katika vituo 813 vya mitihani.

Hata hivyo, NECTA imesema imefuta matokeo ya wanafunzi 77 kutokana na makosa ya kinidhamu ikiwemo kuandika lugha ya matusi katika skripti za mitihani na udanganyifu. Kati ya wanafunzi hao, 47 walitoka katika vituo vya mitihani na 30 walitoka shuleni.

Kwa mujibu wa NECTA, kati ya watahiniwa 526,620 waliofaulu, wasichana ni 278,108 sawa na asilimia 94.26 ya wasichana wote wenye matokeo, huku wavulana waliofaulu wakiwa 248,512 sawa na asilimia 95.79 ya wavulana wote wenye matokeo, jambo linaloonesha ufaulu wa juu kwa jinsia zote.

NECTA imeendelea kuwasisitiza wadau wa elimu kuimarisha maadili na nidhamu katika mitihani ya taifa, huku ikiwapongeza walimu, wazazi na wanafunzi kwa juhudi zinazoendelea kuchangia kuboresha matokeo ya elimu nchini.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: