
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi akipewa kifaa cha kuzimia moto na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga(kulia) baada ya kuwasili Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dodoma ikiwa ni ziara ya kwanza baada ya kuteuliwa kushika nyadhifa hiyo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Ayoub Mohamed Mahmoud akipewa kifaa cha kuzimia moto na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga(kulia) baada ya kuwasili Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dodoma ikiwa ni ziara ya kwanza baada ya kuteuliwa kushika nyadhifa hiyo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi akipokea tuzo ya pongezi kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga(kulia) wakati wa ziara ya kikazi, iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi,jijini Dodoma.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahomud akipokea tuzo ya pongezi kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,John Masunga(kulia) baada ya ziara yake ya kwanza ya kikazi iliyofanyika katika Makao Makuu ya Jeshi hilo,jijini Dodoma.Katikati ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Patrobas Katambi.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi akiwa ameambata na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Ayoub Mohamed Mahmoud wakikagua mavazi mbalimbali wanayotumia Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kutekeleza majukumu yao.Ziara hiyo imefanyika Makao Makuu ya jeshi hilo,jijini Dodoma.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Patrobas Katambi, amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kuweka kampeni maalum ya kudhibiti matumizi holela ya ving’ora na namba za magari zisizotambuliwa kisheria, ambazo zimekuwa zikitumika katika magari ya watu binafsi kinyume na Kanuni za Usalama Barabarani.
Waziri Katambi ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuongoza wizara hiyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Katika ziara hiyo aliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud.
Amesema matumizi holela ya ving’ora yamepoteza maana ya dharura, hali inayosababisha vyombo halali vya uokozi kama magari ya zimamoto na ya wagonjwa kushindwa kupita kwa wakati, jambo linalohatarisha maisha ya wananchi. “Gari la zimamoto au la wagonjwa linapowasha king’ora ni kwa ajili ya kutoa huduma ya dharura, lakini kwa sasa madereva wengi hawazingatii kwa sababu kila mtu amefunga king’ora. Serikali imechukua hatua za mwisho kudhibiti hali hii na ving’ora hivyo vitaondolewa,” amesema Waziri Katambi.
Ameongeza kuwa nchi inaongozwa kwa misingi ya sheria na taratibu, na kwamba changamoto ya Jeshi la Zimamoto kuchelewa kufika katika baadhi ya matukio haisababishwi na uzembe, bali na ukiukwaji wa sheria ikiwemo ujenzi holela katika njia za kupita vyombo vya dharura na wananchi kukwepa ukaguzi wa vifaa vya zimamoto kwa sababu ya gharama. “Gharama kubwa zaidi si fedha bali ni kupoteza maisha na mali,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema Serikali inalitambua na kulithamini Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa mchango wake mkubwa katika kulinda maisha na mali za Watanzania, akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kuongeza ufanisi wa jeshi hilo katika utekelezaji wa majukumu yake.
Naye Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga, amesema kwa mwaka 2025 jumla ya matukio ya moto 3,091 yaliripotiwa nchini, ambapo watu 114 walipoteza maisha huku wengine 295 wakijeruhiwa. Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa wananchi kuzingatia sheria, kanuni za ujenzi na tahadhari za kinga dhidi ya majanga ya moto.
Serikali imewataka wananchi kushirikiana kikamilifu na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuzingatia sheria za barabarani, ujenzi na usalama, ili kupunguza majanga na kuwezesha vyombo vya dharura kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.





Toa Maoni Yako:
0 comments: