Na Sixmund Begashe, Dodoma.

Taasisi zinazohusika na uhifadhi chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zimetakiwa kuhakikisha Sheria na Kanuni za uhifadhi zinatekelezwa kwa kuzingatia utu na maslahi ya wananchi, ili kuwawezesha kunufaika ipasavyo na urithi wa maliasili uliopo nchini.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana Kijaji, jijini Dodoma wakati wa kikao chake na wataalamu wa sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Kitengo cha Huduma za Sheria cha Wizara hiyo, pamoja na Idara ya Wanyamapori na Idara ya Utalii.
Kikao hicho kililenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu tafsiri na utekelezaji wa sheria na kanuni zinazosimamia uhifadhi wa wanyamapori na rasilimali nyingine za asili.

Dkt. Kijaji, pamoja na kuwapongeza wataalamu hao kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kulinda maliasili za taifa, alisisitiza kuwa ni dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha uhifadhi unakwenda sambamba na ustawi wa wananchi.
“Rais wetu, ambaye ni mhifadhi namba moja wa rasilimali za taifa, anatamani kuona Watanzania wananufaika moja kwa moja na utajiri wa maliasili waliobarikiwa. Hivyo, mapitio yoyote ya sheria na kanuni yazingatie pia maslahi ya wananchi,” alisisitiza Dkt. Kijaji.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Utalii, Bw. Nkoba Mabula, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, alimhakikishia Waziri Kijaji kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kwa kuhakikisha uhifadhi na utalii vinaendelea kwa misingi ya maendeleo endelevu.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: