Dar es Salaam.

Serikali imetangaza kuanza utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Bima ya Afya kwa Wote (BAW), mpango unaolenga kuwaondolea mzigo wa gharama za matibabu wananchi wasio na uwezo, wakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao gharama zao zitagharamiwa na Serikali.

Akizungumza leo Januari 23, 2026 wakati wa kikao kazi cha kitaifa cha kujadili utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa amesema kuwa katika awamu hiyo, Kitita cha Huduma Muhimu za Afya kitaanza kutumika rasmi kuanzia Januari 26, 2026, hususan kwa wananchi watakaogharamiwa na Serikali.

Waziri Mchengerwa amesema utekelezaji wa awamu ya kwanza utaenda sambamba na kuanza kutolewa kwa huduma kupitia skimu za Bima ya Afya, kwa lengo la kuhakikisha makundi yaliyo hatarini yanapata huduma bora za afya bila kukumbwa na vikwazo vya kifedha.

“Serikali imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila ubaguzi. Ndiyo maana tumeanza na makundi yaliyo hatarini, ambao gharama zao zitabebwa na Serikali,” alisema Waziri Mchengerwa.

Aidha, alifafanua kuwa gharama ya Kitita cha Huduma Muhimu ni Shilingi 150,000 kwa mwaka kwa kaya isiyozidi watu sita, na kwamba huduma hizo zitatolewa kwa kuzingatia utaratibu wa rufaa katika vituo vya afya vilivyoingia mkataba na skimu za Bima ya Afya.

Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika mageuzi ya sekta ya afya nchini, kwa kuongeza usawa wa upatikanaji wa huduma, kupunguza gharama kwa wananchi na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: