Na Mwandishi Wetu, London – Uingereza

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb.), amewasili jijini London kuanza ziara rasmi ya kikazi nchini Uingereza itakayodumu kuanzia Januari 22 hadi 27, 2026, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza.

Mara baada ya kuwasili, Prof. Mkumbo alifanya kikao cha kazi katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini London, akiwa na mwenyeji wake Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Mbelwa Kairuki. Katika kikao hicho, walijadili mikakati ya kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kutumia kikamilifu fursa zilizopo kwa wawekezaji wa Uingereza nchini Tanzania.

Ziara hiyo inaashiria mwanzo wa mfululizo wa mikutano na shughuli mbalimbali zitakazomkutanisha Waziri na wawekezaji, taasisi za kifedha, makampuni ya kimataifa pamoja na wadau wa maendeleo, kwa lengo la kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuendeleza diplomasia ya uchumi.

Katika ziara hiyo, Prof. Mkumbo anaambatana na viongozi wengine waandamizi akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Bw. Gilead Teri.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kutumia diplomasia ya uchumi kama nyenzo muhimu ya kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kuharakisha maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: