Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele akimkakabidhi mkoba wenye fomu za kuomba kuteuliwa kuwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Makini (MAKINI), Mhe. Coster Jimmy Kibonde. Mgombea huyo wa MAKINI aliambatana na Mgombea Mwenza, Mhe. Aziza Haji Suleiman (kushoto) alichukua fomu hizo leo Agosti 10, 2025 ambapo Tume inataraji kufanya uteuzi Agosti 27 mwaka huu. (Picha na INEC).
DODOMA – Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele, leo Agosti 10, 2025, amemkabidhi mkoba wenye fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Makini (MAKINI), Mhe. Coster Jimmy Kibonde.
Makabidhiano hayo yalifanyika katika Ofisi za Tume, Njedengwa jijini Dodoma, na kushuhudiwa na viongozi wa chama na maofisa wa INEC. Mgombea huyo aliambatana na mgombea mwenza wake, Mhe. Aziza Haji Suleiman, ambaye pia alikabidhiwa nyaraka za uteuzi kwa nafasi ya Makamu wa Rais.
Akizungumza baada ya kupokea fomu hizo, Mhe. Kibonde aliahidi kuendesha kampeni zenye kuzingatia amani, mshikamano na ajenda za maendeleo ya Watanzania wote, huku akisisitiza dhamira ya chama chake kuleta mabadiliko chanya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kwa mujibu wa ratiba ya INEC, zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi linaendelea kwa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais, ambapo uteuzi rasmi unatarajiwa kufanyika tarehe 27 Agosti 2025.


Toa Maoni Yako:
0 comments: