Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Mabloga nchini Tanzania wametakiwa kuhakikisha vinachapisha taarifa za kweli, sahihi na zinazoweza kuthibitishwa, sambamba na kuzingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari, ili kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.
Kauli hiyo imetolewa na Dkt. Egbert Mkoko, Mhadhiri katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), wakati akitoa mada ya Mwongozo wa Habari katika Uandishi wa Habari za Uchaguzi kwenye mafunzo ya wanabloga wa Tanzania (TBN) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, yaliyofanyika katika makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dar es Salaam.
Amesema ni wajibu wa wanahabari na wanabloga kuhakikisha kila taarifa inayochapishwa inatokana na vyanzo vinavyoaminika, kuepuka upendeleo wa kisiasa na kuchochea maudhui yenye kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Dkt. Mkoko amesisitiza kuwa katika kipindi cha kampeni na uchaguzi, taarifa zisizo sahihi zinaweza kusababisha taharuki, hivyo umakini na weledi unahitajika zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Miongoni mwa mada zilizotolewa ni mwongozo wa habari katika uandishi wa habari za uchaguzi, ambapo washiriki walipata elimu kuhusu umuhimu wa uandishi wa habari unaozingatia ukweli, usawa na uadilifu, pamoja na athari za taarifa za upotoshaji katika kipindi cha uchaguzi.
Katika tukio hilo, washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali, kushiriki majadiliano na kubadilishana uzoefu, sambamba na kupewa mwongozo wa namna ya kutumia mitandao ya kijamii kwa njia salama na yenye tija.
Aidha, amepongeza TCRA kwa wapata mafunzo Mabloga wa Tanzania Bloggers Network (TBN) ambayo yataleta mabadiliko chanya katika namna taarifa za uchaguzi zitakavyoripotiwa, na hivyo kusaidia wananchi kupata habari zenye tija na manufaa kwa taifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: