Na Mwandishi Wetu, London.

Askofu Lazarus Msimbe S.D.S wa Jimbo Katoliki Morogoro (pichani) amewataka Watanzania waishio nchini Uingereza (Diaspora) kutambua na kuendeleza mshikamano baina ya waumini mahali walipo.

Askofu Msimbe ametoa wito huo wakati akitoa homilia kwenye Adhimisho la Misa Takatifu aliyoiadhimisha tarehe 1 Machi 2025, katika Parokia ya Mtakatifu Petro, Dagenham, London.
Katika mahubiri yake, Askofu Msimbe alisisitiza umuhimu wa kuwa kama watoto wa kweli—wenye uwazi, upendo, na mshikamano, akihimiza waumini kuendelea kushirikiana na kusaidiana.

Miongoni mwa wageni waliohudhuria Misa hiyo ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Ndugu Mbelwa Kairuki, Maafisa Waandamizi wa Ubalozi wa Tanzania na Dada Prudencia Kimiti, MBE, Mtanzania aliyewahi kutunukiwa tuzo na Malkia.
Katika salamu zake, Balozi Kairuki amewapongeza wanadiaspora wakatoliki kwa kuendeleza umoja miongoni mwao.

Aidha Balozi alitumia fursa hiyo kuwatakia Waislamu mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuwaombea Wakristo wanapojiandaa na Kipindi cha Kwaresma, akisisitiza mshikamano wa kidini miongoni mwa Watanzania.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki wanaoishi London, Dr Christian Henjewele, amemshukuru Askofu Msimbe kwa kuungana na jumuiya hiyo na kumhakikishia kuwa umoja wa Watanzania Wakatoliki unaendelea kuimarika.

Amemshukuru pia Balozi Kairuki kwa uwepo wake na kwa kuendelea kuunga mkono Watanzania waishio Uingereza.

Adhimisho hilo pia limewakutanisha waumini kutoka London, Coventry, Cardiff, Birmingham, Milton Keynes, na miji mingine, wakishiriki pamoja katika mshikamano wa kiimani na upendo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: