

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
Zanzibar, 26 Februari 2025 – Vodacom Tanzania PLC imetia saini ushirikiano wa kimkakati na Shirika la Miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA) ili kuboresha huduma za mawasiliano na kuharakisha mabadiliko ya kidijitali visiwani Zanzibar. Mkataba huu, uliosainiwa katika ofisi za Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, unairuhusu Vodacom kutumia miundombinu ya nyaya za chini ya bahari inayomilikiwa na serikali, hatua itakayoboresha uwezo wa mawasiliano ya sauti na data katika visiwa hivyo.
Hafla ya utiaji saini ilihudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohamed, Mkurugenzi Mkuu wa ZICTIA, Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman, na Mkurugenzi wa Mtandao wa Vodacom Tanzania, Andrew Lupembe, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania.

Aliendelea kwa kusisitiza dhamira ya serikali katika kusaidia waendeshaji wa mitandao ya simu ili kuongeza upatikanaji wa intaneti. "Tunashukuru ushirikiano wa Vodacom katika kutumia miundombinu ya ZICTIA—rasilimali ambayo serikali imewekeza ili kusaidia kufanikisha ajenda ya kitaifa ya TEHAMA na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata faida kutokana na teknolojia ya kisasa.”
Mh Waziri aliongeza kwa kusema, “Uwekezaji huu utahakikisha huduma za intaneti zinakuwa za haraka na za uhakika zaidi, hatua ambayo itasaidia kuimarisha programu za serikali mtandao (e-government), elimu mtandao (e-learning), afya mtandao (e-health), na biashara mtandao (e-commerce).
Mkurugenzi wa Mtandao wa Vodacom, Andrew Lupembe, alieleza dhamira ya kampuni katika kuimarisha mawasiliano Zanzibar. “Kama kampuni inayoongoza katika teknolojia, tunaelewa kuwa mawasiliano ni msingi wa ukuaji wa uchumi na ubunifu. Kupitia ushirikiano huu na ZICTIA, tunahakikisha kuwa biashara, taasisi, na wananchi wa Zanzibar wanaweza kuwasiliana, kupata huduma za kidijitali, na kufanya miamala bila usumbufu.”
Mkurugenzi Mkuu wa ZICTIA, Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman, alisisitiza umuhimu wa waendeshaji wa mitandao kutumia miundombinu ya kitaifa ili kuharakisha maendeleo ya TEHAMA. “Mtandao wetu wa nyaya za chini ya bahari uliundwa kwa lengo la kuingiza Zanzibar katika zama ya kidijitali. Tuna furaha kuona Vodacom ikitumia rasilimali hii ili kuboresha huduma zake, hatua inayosaidia kufanikisha maono yetu ya jamii inayotegemea teknolojia kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.”
Ushirikiano huu ni hatua muhimu katika mageuzi ya kidijitali Zanzibar, ukiweka visiwa hivi katika nafasi bora kama kitovu cha mawasiliano na ubunifu. Kwa kuunganishwa kwa miundombinu ya Vodacom na mfumo madhubuti wa TEHAMA wa ZICTIA, Zanzibar itanufaika na mfumo wa kisasa wa mawasiliano wa kasi ya juu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: