Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Geita.

Jumla ya minara 55 iliyojengwa katika wilaya tano (5) za Mkoa wa Geita kufuatia makubaliano kati ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na watoa huduma za Mawasiliano (MNOs) inaendelea kutoa huduma za Mawasiliano kwa wananchi wa Geita.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bi. Justina Mashiba, amebainisha hayo Julai 17, 2024, mkoani Geita wakati akitoa taarifa ya utendaji wa mfuko huo kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela na viongozi wengine wa mkoa huo.
Bi. Mashiba amesema, ruzuku kutoka UCSAF iliyotumika kujenga minara hiyo ni Shilingi Bilioni 6.44, na watu wapatao 643,354 watanufaika.

Ametaja wilaya zitakazofaidika na minara hiyo iliyojengwa kwa teknolojia ya 2G, 3G na 4G, na idadi ya minara iliyojengwa, kwenye mabano, kuwa ni Bukombe (10), Chato (9), Geita DC (10), Mbogwe (18) na Nyang'wale (8).
Aidha, Mashiba amesema, Mkoa wa Geita ni moja kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara, itakayofaidika na mradi wa minara 758 inayojengwa nchi nzima.

Amesema kwa mkoa wa Geita, minara 17 itajengwa kwa ruzuku ya Shilingi Bilioni 2.2, katika mradi huo utakaowanufaisha Watanzania zaidi ya milioni 8.5 nchi nzima, itakapokamilika mwanzoni mwa mwaka 2025.
Amezitaja wilaya za Mkoa wa Geita inakojengwa minara 17 ya mradi huo, na idadi ya minara kuwa ni Bukombe (6), Chato (4), Geita (2) na Mbogwe (5). Amesema, hadi kufikia mwishoni mwa Juni 2024, jumla ya minara sita (6) imewashwa, na vijiji kadhaa katika kata 16 zikiwemo Busonzo, Iyogelo, Makurugusi, Nyakagonga, Ilolangulu na Nhomolwa.

Kati ya minara hiyo tayari miwili inayojengwa na kampuni ya AIRTEL mmoja katika kijiji cha Luhuha Kata ya Nyakagomba na Busonzo Kata ya Busonzo imekamilika na tayari imeanza kutoa huduma za Mawasiliano kwa wananchi wa maeneo hayo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: