Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza mara baada ya kupokea maelezo kuhusu ujenzi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano inayomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambapo alipongeza NSSF kwa mradi wa hoteli hiyo.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu (kushoto)Mhe. Protobas Katambi akitoa maelezo kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu taratibu za kupitisha miradi mbalimbali ambayo hupitia Benki kuu ya Tanzania (BOT) ili ishauri na ofisi ya Waziri Mkuu inasimamia na kuwa lengo kuu la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kuwekeza kulinda fedha za mifuko
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ( NSSF) Masha Mshomba, akitoa maelezo kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu ujenzi wa mradi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano inayomilikiwa na NSSF iliyopo jijini Mwanza, ambapo alisema ujenzi huo unatarajia kukamilika ifikapo mwezi Juni 2024 baada ya kupatikana muendeshaji wa hoteli mwishoni mwa mwezi huu.
Meneja Usimamizi wa Miradi NSSF, Mhandisi Helmes Pantaleo akitoa maelezo kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania namna mradi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano utakavyokuwa. Mradi huo una ghorofa 16, vyumba 168 vya kulala vya aina mbalimbali ikijumuisha sehemu ya kupumzikia Rais (Presidential Suite), migahawa, sehemu za vinywaji na michezo (sports bar).

MATUKIO KATIKA PICHA

Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipotembelea ujenzi wa mradi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano inayomilikiwa na NSSF iliyopo eneo la Capripoint, jijini Mwanza.
:
Na MWANDISHI WETU, MWANZA

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amesema katika ujenzi wa hoteli za nyota tano muendeshaji wa hoteli mwenye hadhi ya kimataifa ni kigezo cha msingi katika kukamilisha mradi wa aina hiyo.

Mshomba alieleza hayo tarehe 14 Juni, 2023 mbele ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyetembelea mradi wa hoteli ya nyota tano inayomilikiwa na NSSF iliyopo jijini Mwanza.

“Katika ujenzi wa hoteli za nyota tano kwa uzoefu ambao tuliupata kutoka kwa wenzetu wa Mifuko kama sisi ya nchi jirani, kwa mfano Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe ni kwamba huwezi kumalizia hoteli kama hii kabla hujampata yule muendesha hoteli,” alisema Mshomba.

Alisema kwa vile jambo hilo halikuwezekana ndio maana mradi wa hoteli hiyo ulisimama na kwamba mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi huu ea Juni 2023 wanatarajia kumpata muendeshaji wa hoteli na ujenzi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2024.

Kwa mujibu wa Mshomba, mwaka 2019 walienda kujifunza nchini Zambia na Afrika Kusini ili kupata uzoefu jinsi wanavyopata waendeshaji hoteli ya kitalii ya nyota tano.

“Kule tuliweza kuwapata kampuni kama Hilton Hotels Worldwide ambao walikuwa wanaendesha hoteli kule, lakini pia Radissons Hotels na Legacy Hotel, ambapo tuliongea nao lakini kwa bahati mbaya mwishoni mwa mwaka 2019 ukazuka ugonjwa wa Corona (Covid 19) uliosababisha mambo mengi kusimama.

Hata hivyo, Mshomba alisema ilipofika mwezi Machi 2021, shughuli za ujenzi ziliendelea na walianza kumtafuta msanifu wa kuandaa michoro na mahitaji muhimu kwa ajili ya kumalizia kazi za ndani kwa viwango vya kimataifa (interior designer Architect) M/s SOURCE IBA toka Afrika Kusini.

Alisema mwezi Septemba 2022 walitangaza zabuni ya kumpata muendesha hoteli wa kimataifa, na kwamba kipindi hicho zile kazi ambazo zinahitajiwa kuendelea kabla ya kuwa na muendesha hoteli zilikuwa zinaendelea kama vile ujenzi wa vyoo na madirisha.

Mshomba alisema baada ya kutangaza zabuni wamewapata waendesha hoteli watatu ambao waliomba zabuni ikiwemo kampuni ya Hilton Hotels Worldwide, Radissons Hotels na Legacy Hotel, ambapo mwishoni mwa mwezi huu wanatarajia kupata mshindi.

Akizungumza katika mradi huo, Mhe Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema miradi ya vitega uchumi inayofanywa na NSSF itaongeza tija kwenye Mfuko.

Mhe. Rais Dkt. Samia aliipongeza NSSF kwa mradi wa hoteli hiyo kuwa ni kitu kizuri ambapo itakapokamilika itachochea sekta ya utalii na kuongeza tija kwenye Mfuko.

“Hongereni sana NSSF kwa kweli mradi huu ni kitu kizuri ,” alisema Mhe. Rais Dkt. Samia.

Kwa upande wake, Mhe. Protobas Katambi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, alisema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inawekeza kwa lengo la kulinda thamani ya michango ya wanachama na kuahidi kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaendelea kushirikiana na Mfuko katika kuangalia maeneo mengine ya uwekezaji.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: